27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: WAGOMBEA URAIS WAJIPAMBANUA

Na Mwandishi Wetu,

TUME Huru ya Uchaguzi Kenya (IEBC) imeidhinisha wanasiasa nane watakaowania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.

Walioidhinishwa ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee, anayewania kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili. Mgombea mwingine ni Raila Odinga, ambaye anawania urais kwa mara ya nne sasa.

Odinga amewahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Muungano ya Rais Mwai Kibaki kati ya mwaka 2008 na 2013, anawania urais chini ya umoja wa vyama vya upinzani National Super Alliance (NASA).

Katika uchaguzi huo kutakuwa na wagombea binafsi wanne (ni wagombea huru, hawana vyama).

ABDUBA DIDA

Anawania urais kupitia Chama cha Alliance for Real Change (ARK) na Muungano wa Tunza Coalition. Alikuwa mwalimu wa shule ya upili ya Lenana jijini Nairobi. Hii ni mara yake ya pili kuwania urais baada ya mwaka 2013 ambapo alipata kura 52,848.

CYRUS JIRONGO

Ni mwanasiasa na mfanyabiashara ni mara yake ya kwanza kuwania urais. Anawania kupitia Chama cha United Democratic Party (UDP).

Alipata umaarufu kisiasa mwaka 1992 alipokuwa katika kundi la vijana wa Chama cha KANU, Youth for KANU 1992 waliokuwa wakimfanyia kampeni Rais Daniel Arap Moi, wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka huo.

EKURU AUKOT

Anawania urais kupitia Chama cha Thirdway Alliance Kenya (TAK) na ni mara yake ya kwanza kuwania urais. Aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Wataalamu waliosaidia kutunga Katiba Mpya ya Kenya ambayo iliidhinishwa na kuanza kutekelezwa mwaka 2010.

Asili yake ni Kapedo, Turkana Kaskazini-Magharibi mwa Kenya na amejitangaza kama mtu anayeleta mwamko mpya katika uongozi nchini Kenya. Amekuwa pia akitetea makabila madogo nchini humo.

JAPHET KALUYU

Ni mgombea huru ambaye amerejea nchini Kenya hivi karibuni kutoka Marekani. Amejieleza kama mwalimu, mshauri na mwandishi ambaye ana uzoefu wa kufanya kazi Wall Street, Marekani. Anasema amebobea katika utafiti katika sekta ya afya na msomi. Ni mara yake ya kwanza kuwania urais.

JOSEPH NYAGAH

Ni mwanasiasa wa muda mrefu nchini Kenya ambaye amewahi kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika chini ya Rais Mwai Kibaki na baadaye akawa mshauri wa Rais Kenyatta.

Baba yake ni Jeremiah Nyagah, naye alikuwa waziri wakati wa utawala wa awamu ya kwanza wa mwanzilishi wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta.

Sifa nyingine ya Nyagah kuwahi kuwakilisha Kenya katika Umoja wa Ulaya. Pia amewahi kuwa mbunge eneo la Gachoka katika Kaunti ya Embu Mashariki mwa Kenya kabla ya kuteuliwa waziri.

Anasema ndiye pekee anayeweza kutatua matatizo yanayoikumba Kenya, kutokana na uzoefu wake katika uongozi.

Akihojiwa na runinga ya NTV hivi karibuni baada ya kuidhinishwa, alidokeza kwamba aliacha kazi yake ya kuwa mshauri wa rais baada ya kugundua kwamba ushauri aliokuwa anautoa haukufuatwa.

PROFESA MICHAEL WAINAINA

Yeye ni mgombea huru ambaye amekuwa mhadhiri wa Fasihi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Amekuwa mkosoaji mkuu wa mfumo wa sasa wa kisiasa Kenya na pia mchambuzi wa siasa. Anasema aliamua kuwa mgombea huru kwa sababu vyama haviwapi nafasi vijana na wanawake.

RAILA ODINGA

Ni kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ambaye anawania chini ya muungano wa vyama vya upinzani kwa jina la National Super Alliance (NASA).

Aliwahi kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia Mkataba wa Kitaifa ulioafikiwa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008, ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.

Ni mara yake ya nne kuwania urais Kenya. Mwaka 2013 akiwa bado na mgombea wake wa sasa Makamu wa Rais wa zamani, Kalonzo Musyoka, alishindwa na Rais Uhuru Kenyatta. Alipinga matokeo hayo mahakamani lakini mahakama ikatupilia mbali kesi hiyo.

UHURU KENYATTA

Anawania kwa muhula wa pili kupitia Chama cha Jubilee Party ambacho asili yake ni Muungano wa Jubilee wa vyama vya TNA na URP alioutumia kushinda urais mwaka 2013.

Uhuru Kenyatta ni moto wa mwanzilishi wa Taifa la Kenya, Jomo Kenyatta. Mgombea wake mwenza ni William Ruto kutoka eneo la Bonde la Ufa la Kenya.

Wawili hao wanawaomba wapiga kura kuwachagua tena kuendeleza maendeleo ambayo wanaamini Serikali yao imetekeleza katika kipindi cha miaka minne ambayo wamekuwa madarakani.

Kenyatta aliwania urais mara ya kwanza 2002 dhidi ya Mwai Kibaki kupitia chama kilichokuwa kinatawala wakati huo, KANU cha Rais Moi aliyekuwa anaondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 24.

Alishindwa na akawa kiongozi wa upinzani na kwa pamoja na Odinga wakafaulu kupinga Katiba Mpya iliyopendekezwa mwaka 2005. Mwaka 2007, alimuunga mkono Rais Kibaki kwenye uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles