23 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: KESI YA WAPINZANI YATISHIA KUAHIRISHWA UCHAGUZI

NAIROBI, KENYA

JAJI Mkuu nchini Kenya, David Maraga, amesema licha ya muungano wa upinzani kufungua kesi mahakamani kutaka Tume ya Uchaguzi kuachana na zabuni iliyotoa kwa kampuni ya Dubai kuchapisha karatasi za kupigia kura, mahakama itahakikisha kuwa uchaguzi huo hauahirishwi, licha ya dalili hizo kujionyesha sasa.

Tume ya Uchaguzi nchini humo imeonya kuwa, huenda uchaguzi huo utaathirika ikiwa upinzani ungewasilisha kesi hiyo katika kipindi hiki ambacho umebaki mwezi mmoja tu kabla ya kufanyika uchaguzi.

Mgombea wa urais kupitia muungano huo, Raila Odinga, anasema kampuni hiyo haiwezi kuaminiwa kwa sababu ina ushirikiano wa karibu na familia ya Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa vikali na serikali na kusema hawajali ni kampuni gani itakayopewa zabuni ya kufanya kazi hiyo.

Odinga amekuwa akidai kuwa kampuni hiyo itachapisha karatasi zaidi ili kumsaidia Kenyatta kutangazwa mshindi katika Uchaguzi wa mwezi Agosti.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, Ezra Chiloba, alikanusha madai hayo kuwa aliwahi kukutana na Rais Kenyatta na kukubali kutoa zabuni hiyo kwa kampuni hiyo ya Dubai.

Aliongeza kuwa, uchapishaji wa karatasi hizo ni lazima uanze wiki hii, kwa sababu ya muda mfupi unaosalia kuelekea siku ya kupiga kura.

Viongozi wa dini wakiongozwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki wameitaka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na haki.

Wagombea wamwaga ahadi kwa wapigakura

Wanasiasa wanashindana huko na huku kumwaga orodha ya ahadi ambazo watazitekeleza mara baada ya kuchaguliwa.

Mgombea wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinga na mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, wamemwaga ahadi nyingi tangu walipozindua kampeni zao rasmi jijini Nairobi.

Odinga amesema ikiwa atashinda urais, atapambana na ufisadi na wale wenye doa hawataruhusiwa kufanya kazi katika serikali yake.

Aidha, amesema serikali yake itahakikisha kuwa inashusha gharama ya maisha kwa muda wa siku 90 watakazokuwa madarakani, lakini pia kupunguza kodi ya nyumba kote nchini humo.

Kwa upande wake Rais Uhuru Kenyatta, akiwa na mgombea mwenza wake, William Ruto, ambao wanawania kwa muhula wa pili, wamesisitiza kuwa kuna mafanikio makubwa kwenye serikali yao, hivyo wananchi waichague tena Jubilee ili wamalizie kile kilichobaki.

Kenyatta na Ruto walizindua kampeni zao katika uwanja wa michezo wa Nyayo, jijini Nairobi. Mbali na wagombea hao wawili wakuu, Odinga na Kenyatta, ambao wanapewa nafasi kubwa ya kupambana katika kinyang’anyiro hicho, wamejikuta kwenye vita vya maneno ambapo wafuasi wao wamejitahidi kuwa wastahimilivu kuliko ilivyokuwa mwaka 2007.

Wagombe wengine nane waliojitosa kwenye uchaguzi huo wakiwa wagombea binafsi nao wameendelea kuzunguka huku na huko kuomba kura.

Masuala muhimu yanayojiri katika kampeni

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anatetea kiti chake, anasema anataka kuendeleza rekodi anayosema ni ya maendeleo nchini humo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli ya kisasa na mradi wa umeme kuwafikia idadi kubwa ya Wakenya hadi kijijini.

Kenyatta anajivunia ujenzi wa reli ya kisasa atakayoizindua wiki ijayo kutoka Mombasa hadi jiji kuu, Nairobi.

Mradi huu unatarajiwa kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya miji hiyo miwili, ambayo ni muhimu kibiashara na uchumi wa nchi hiyo.

Rais Kenyatta na mgombea mwenza wake, William Ruto, wanatarajiwa kutumia mafanikio hayo kujitafutia uungwaji mkono kutoka kwa wapigakura katika kanda nane walizozigawa kwa lengo la kupata kura za kutosha.

Hata hivyo, upinzani umeendelea kuishutumu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kujihusisha na ufisadi na kukopa fedha kupita kiasi kutoka nje ya nchi.

Ukosefu wa usalama pia ni suala ambalo upinzani unasema serikali ya sasa imeshindwa kushughulikia.

Kundi la Al Shabab limekuwa likiwashambulia raia wa kawaida na maofisa wa usalama kama polisi na wanajeshi, tangu kuingia madarakani mwaka 2013.

Kupanda kwa gharama za maisha, hasa siku za hivi karibuni, uhaba wa unga wa mahindi na sukari, serikali imelazimika kuingilia kati na kuamua kununua mahindi kutoka nchini Mexico, ili kuwawezesha wananchi kupata unga kwa bei nafuu.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema ushindani mkubwa wa kisiasa unatarajiwa kati ya Rais Kenyatta na Odinga.

Siasa za Kenya bado hazijaegemea sera, lakini zinaendelea kuegemea ukabila na ukanda.

Uchaguzi wa Kenya ni muhimu EAC?

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zinafuatilia kwa karibu kampeni za kisiasa nchini Kenya.

Je, uchaguzi huo ni muhimu kwa nchi hizo? Jibu ni muhimu kwa nchi hizo kufahamu kinachoendelea katika uchaguzi wa Kenya, kwa sababu zinaitegemea Kenya kiuchumi, kisiasa na katika masuala ya usalama.

Kenya, inayoongoza kiuchumi na katika sekta ya mawasiliano na teknolojia, lakini pia miundombinu kama viwanja vya ndege na safari za anga, ni muhimu pia kwa mafanikio ya nchi jirani.

Wageni mashuhuri, wakiwamo watalii wanaokwenda katika nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekuwa wakifikia jijini Nairobi kupitia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, kabla ya kuendelea na safari nyingine.

Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini kwa muda mrefu zinategemea Bandari ya Mombasa kuingiza na kusafirisha bidhaa zake.

Wakati wa machafuko ya baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007, wafanyabiashara walipoteza kiasi kikubwa cha fedha baada ya mali zao kuharibiwa na kuchelewa kufika sokoni.

Hasara hiyo imewafanya wafanyabiashara hao kuendelea kuidai Serikali ya Kenya Dola za Marekani milioni 50, kutokana na uharibifu walioupata.

Mamia ya wakimbizi kutoka nchini Kenya walikimbilia nchini Uganda wakati wa machafuko ya mwaka 2007/8. Uganda inakabiliwa na mzigo wa kuwapa hifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Somalia.

Kenya ni muhimu sana kwa Tanzania, kwa sababu ya soko la bidhaa zake ambapo wafanyabiashara kutoka nchi hiyo kubwa ukanda wa Afrika Mashariki, haitaki kupoteza biashara kwa sababu ya machafuko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles