27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU DRC: NI ZAMU YA TSHISEKEDI, KATUMBI, BEMBA

NA MARKUS MPANGALA       


DESEMBA 23, mwaka huu, wananchi wa Jamhuri ya Kidemokasia ya Kongo wanatarajia kupiga kura kuchagua rais na wabunge nchini humo.

Uamuzi wa nani awe rais wa nchi hiyo ni mtihani mgumu kwao, kutokana na historia za wanaowania nafasi hiyo, akiwamo Rais aliyepo madarakani, Joseph Kabila.

Mchakato wa kuchukua fomu za kuwania urais na ubunge ulianza mwanzoni mwa juma hili, huku vyama vyote vya siasa nchini humo vikionyesha nia ya kushiriki katika uchaguzi mkuu huo kama ulivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, CENI.

Wasiwasi uliopo ni juu ya Rais Kabila kugombea tena wadhifa huo ilhali Katiba ya nchi hiyo imekataza kuongoza zaidi ya mihula mitatu.

Kwa mujibu wa kalenda iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, inaonyesha kuwa Agosti 8, mwaka huu, itakuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha fomu kwa wagombea wa vyama vyote.

Wagombea wanaotimiza masharti ya kuwania nafasi hizo wamepewa siku 15 kuwa wamekamilisha zoezi hilo, huku sheria ikieleza kuwa atakayeruhusiwa kugombea lazima awe raia wa nchi hiyo.

Hata hivyo, orodha kamili ya wagombea urais itajulikana katikati ya Septemba, mwaka huu, baada ya uhakiki utakaofanywa na CENI, ili kuhakikisha watia nia wote wamekidhi vigezo.

Tayari baadhi ya wanasiasa wametangaza nia ya kuwania katika uchaguzi huo, wakati wengine, kama vile Rais anayemaliza muda wake, akiwa hajatoa msimamo wake wa kuwania au la.

Makamu wa Rais wa zamani, Jean-Pierre Bemba na mfanyabiashara Moise Katumbi Chapwe, mshirika wa zamani wa karibu wa Rais Joseph Kabila, ni miongoni mwa wanasiasa waliotangaza nia yao ya kuwania katika uchaguzi huo, licha ya kuwa nje ya nchi kwa muda mrefu.

Makala haya yanachambua vigezo vya wagombea vilivyowekwa kikatiba katika nafasi ya urais na wanasiasa ambao wanawavutia wapigakura katika nafasi hiyo kabla ya Tume ya Uchaguzi kutangaza rasmi waliokidhi vigezo.

Vigezo vya kugombea

Katiba imekataza rais kuongoza zaidi ya mihula miwili, Joseph Kabila amehitimisha ukomo huo tangu mwaka 2016, hata hivyo, ameongoza miaka miwili ya mpito, yaani mwaka jana na mwaka huu.

Aidha, Katiba inaagiza kuwa mgombea urais anatakiwa kuwa raia halali wa DRC, hata kama atakuwa ametoka kwa wazazi mchanganyiko.

Katiba imeagiza mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi ya urais wa DRC anapaswa kutotiwa hatiani mahakamani kwa makosa yoyote.

Wiki iliyopita Bemba alisema anaamini yeye ndiye mgombea mwenye nguvu zaidi kuweza kuwakilisha upinzani, lakini atakuwa tayari kuachia nafasi yake kwa mgombea mwingine atakayechaguliwa. Je, Bemba ana vigezo vya kugombea urais wa DRC?

Huenda azma yake ya kugombea ikapingwa mahakamani. Bemba anadaiwa kuwa hana vigezo vya kugombea baada ya kutiwa hatiani kwa mashtaka ya kuingilia ushahidi na mahakama ya ICC hata kama hatia yake ya mauaji, ubakaji na uharibifu vilivyofanywa na wapiganaji wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2002 kutupiliwa mbali.

Kubatilishwa kwa ugombea wa Bemba kunaweza kuwakasirisha wafuasi wake, hasa ukanda wa magharibi mwa nchi hiyo, ambako kuna gome yake kubwa ya kisiasa.

Kushindwa kwake na Kabila mwaka 2006 kulisababisha mapambano ya silaha katika mitaa ya Mji Mkuu Kinshasa, kati ya wapiganaji wake na wanajeshi wa serikali.

Mratibu wa chama cha MLC, Denis Vila wa tawi la wanawake wa chama hicho, ameviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa, iwapo kutakuwa na jaribio la kumzuia Bemba kuwania urais, basi litakuwa la kisiasa na amesisitiza kuwa watahakikisha wanampigania mwanasiasa huyo mkongwe katika kinyang’anyiro hicho.

Mgombea mwingine wa upinzani, mfanyabiashara tajiri Katumbi, naye inasemekana kuwa huenda akakosa sifa kutokana na kutiwa hatiani kwa udanganyifu unaohusiana na umiliki wa majumba mwaka 2016.

Kwa mujibu wa kura za maoni zilizochapishwa wiki hii ni kwamba, endapo uchaguzi ungefanyika sasa, Katumbi na kiongozi mwenzake wa upinzani, Felix Tshisekedi, wangeshinda vikali katika kinyang’anyiro cha urais baada ya kila mmoja kupata asilimia 19. Bemba angepata asilimia 17 na Kabila asilimia 9.

Katumbi anachukuliwa kuwa ndiye mgombea wa kambi ya upinzani nchini DRC, ingawa hajathibitishwa na itamlazimu kuchuana na Bemba kwenye muungano huo. Mfanyabiashara huyo amekuwa akiishi Afrika Kusini baada ya kuhofia maisha yake nchini DRC.

Katumbi alizaliwa Desemba 28, 1964 eneo la Kashobwe, anatoka katika kabila la Babemba.    Amewahi kuishi nchini Zambia kwa miaka mingi.

Ana undugu na Katebe Katoto, maarufu kama Rafael Soriano, na mfuasi wa Jenerali Laurent Nkunda. Baba yake ni Padri Nissim Soriano, Mwitaliano mwenye asili ya Kiyahudi. Mama yake ni Virginie Katumbi, anatoka katika familia ya kifalme ya Kazembe.

Nia ya Katumbi ya kugombea urais imechochea kupandishwa kizimbani nchini humo akituhumiwa makosa mbalimbali ya rushwa, udanganyifu na ukosefu wa maadili.

Duru za kisiasa zimesema Katumbi, ambaye ni mshirika wa zamani wa karibu wa Rais Joseph Kabila, mwanasiasa huyo alitarajiwa kurejea nchini DRC kabla ya Agosti 8, mwaka huu.

Wanasheria wa mwanasiasa huyo walieleza kuwa, hakukuwa na sababu inayomzuia mteja wao kurejea nchini humo.

Hata hivyo, Serikali ya Congo imemzuia Gavana huyo wa zamani wa Jimbo la Katanga anayeishi uhamishoni Afrika Kusini kurudi nyumbani.

Katumbi aliomba ruhusa kuingia nchini DRC Agosti 3, ili kuwahi kuwasilisha nyaraka zake za uteuzi wa chama kuwa mgombea urais kwa Tume ya uchaguzi nchini humo.

Maofisa wa polisi mjini Lubumbashi waliweka vizuizi katika barabara kuu na usalama uliimarishwa ndani na katika maeneo yaliyo karibu na uwanja wa ndege.

Duru za kisiasa zimesema kuwa, serikali imepanga kuzifunga njia na kuzuia ndege ya Katumbi isitue DRC. Waziri wa Habari, Lambert Mende, alisema gavana huyo wa zamani kutoka jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini atakamatwa iwapo atajaribu kuingia nchini kwa ndege ya usafiri wa abiria.

Katumbi aliondoka nchini Congo mwaka 2016 baada ya kukorofishana na Rais Kabila, baadaye alishtakiwa kwa udanganyifu wa mali na alihukumiwa miaka mitatu gerezani pasipo yeye kuwepo mahakamani.

Aidha, Katumbi anatarajiwa pia kupanda kizimbani katika Mahakama ya Rufaa Oktoba mwaka huu, kusikiliza kesi nyingine inayomkabili ya upokonyaji wa mali za watu binafsi.

Serikali ya DRC imemshtaki Katumbi mahakamani kwa madai kuwa ana uraia wa Italia. Hata hivyo, Msemaji wake, Olivier Kamitatu, ameviambia vyombo vya sheria vya Italia tayari vimeamua kuhusu suala hilo ambapo vimesisitiza kuwa Katumbi hajawahi kupewa uraia wa Italia.

Kwa upande wake Joseph Kabila, ambaye ameongoza DRC kwa mihula miwili inayoelekezwa kikatiba, lakini tangu mwaka 2016 amekuwa akihusishwa katika mpango wa kuongeza muhula wa tatu, jambo ambalo linapingwa na mataifa mbalimbali ya kigeni, yakiongozwa na Marekani pamoja na vyama vya siasa nchini mwake.

Kabila, aliyeiongoza nchi hiyo tangu Januari 2001, akipokea madaraka siku kumi baada ya kifo cha baba yake, Rais Laurent Desire Kabila, alichaguliwa tena kuwa Rais mwaka 2006/2011.

Tangu alipoingia madarakani amekuwa akikabiliwa na vita katika Jimbo la Kivu Mashariki mwa nchi yake, na vikosi vya waasi wa ndani vinavyoungwa mkono na mataifa jirani ya Uganda na Rwanda.

Kabila alizaliwa Juni 4, 1971 katika Kijiji cha Hewabora, eneo la Fizi, Mkoa wa Kivu ya Kusini, Mashariki mwa DRC. Ni mtoto wa kiongozi wa muda mrefu wa waasi, na Rais wa Congo Laurent-Désiré Kabila (marehemu) na Sifa Mahanya.

Licha ya kutotamka kama atagombea urais au la, lipo kundi la wanaharakati linalomuunga mkono Rais Kabila nchini mwake linalojiita FCC, limezindua mkakati wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Hata hivyo, hawajaeleza iwapo Rais Kabila atawania muhula wa tatu kinyume cha Katiba ya nchi hiyo.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa nchi hiyo, Rais Kabila aliwahakikishia wananchi wa DRC kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika Desemba 23, mwaka huu, kama ilivyopangwa, kauli hiyo imetiliwa shaka na Maaskofu wa Kanisa Katoliki, wakidai kuwa huenda uchaguzi huo usifanyike.

Uchaguzi nchini DRC umepangwa kufanyika huku kukiwa na mivutano ya kisiasa juu ya masuala muhimu ya mpango mzima. Baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanataka uchaguzi huo ufanyike bila Kabila kuwapo kinyang’anyironi, huku wengine wakitaka Rais Kabila ashiriki uchaguzi huo.

Jean Pierre Bemba ameidhinishwa na chama chake cha MLC kuwa mgombea wake atakayechuana na wengine wa upinzani ili kumpata mmoja atakayepeperusha bendera ya kambi hiyo.

Bemba ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa na mtoto wa mfanyabiashara maarufu nchini DRC, Bemba Saolona. Jean alizaliwa Novemba 4, 1962. Mwaka 1998 aliunda chama cha MLC,  ambacho kiligeuka kuwa kundi la waasi. Amewahi kuwa Makamu wa Rais kuanzia mwaka 2003 hadi 2006 chini ya mkataba wa amani. Mwaka 2007 alitoroka kwenda Ubelgiji baada ya mapigano kuzuka Kinshasa, mwaka 2008 alikamatwa mjini Brussels na kuwasilishwa Mahakama ya Kimataifa ya ICC. Mwaka 2016 alipatikana na hatia kwa uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu, hukumu yake ilibatilishwa mwaka 2018, baada ya kukata rufaa.

Serikali ya DRC imemruhusu mwanasiasa huyo kuingia nchini humo tofauti na wasiwasi uliokuwapo awali. Kurejea kwa Bemba kumeongeza msisimko na kutikisa siasa za DRC.

Wapinzani wake, kikiwamo chama tawala cha PPRD, kimetoa tamko kuwa Bemba hana vigezo vya kugombea nafasi ya urais nchini humo, kufuatia makosa na kifungo alichotumikia baada ya kitengo cha mwanzo cha ICC kumkuta na makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, kabla ya kuachiliwa huru katika kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo.

Felix Tshisekedi ni mwanasiasa ambaye ameteuliwa na chama kikuu cha upinzani UDPS kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu huo. Naye  atatakiwa kuvuka vikwazo vya Tume ya Uchaguzi CENI, kulingana na vigezo vya kikatiba.

Felix ni mtoto wa mwasisi wa chama hicho, Etienne Tshisekedi, aliyefariki dunia mjini Brussels nchini Ubelgiji Februari, mwaka jana.

Uteuzi wake ulikuja baada ya mkutano wa wajumbe wa chama hicho uliofanyika usiku kucha katika Mji Mkuu Kinshasa. Tshisekedi pia amechaguliwa kuongoza chama hicho, akiwa amejizolea kura 790 kati ya 803 za wajumbe wa chama.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi CENI, nchi hiyo ina wapigakura milioni 43. Matokeo ya urais yanatarajiwa kutangazwa Januari 9, mwakani na mshindi wa nafasi hiyo ataapishwa Januari 13, mwaka huo.

Hofu juu ya hatima ya Rais Kabila kubaki madarakani si kitu cha kubeza, ikizingatiwa kuwa Katiba inamzuia kuendelea na wadhifa huo kwa muhula wa tatu.

Baadhi ya raia wamekuwa wakiandamana mara kwa mara, huku wakikabiliana na vikosi vya serikali pamoja na baadhi kukamatwa.

Maandamano ya upinzani yanadaiwa kusababisha makumi ya watu kufariki dunia. Kura za maoni nchini DRC zilizotangazwa wiki hii zinaonyesha kuwa, asilimia 69 ya raia hawana imani kwamba Tume ya Uchaguzi nchini humo inaweza kuendesha uchaguzi wa haki na wengine asilimia 80 wana maoni hasi juu ya Rais Kabila.

Endapo uchaguzi ungefanyika sasa, asilimia 66 wangependelea kumchagua mgombea wa upinzani na Kabila angepata asilimia 6 kama angegombea urais huo tena.

Nao upinzani nchini DRC umekuwa ukitawaliwa na mgawanyiko miongoni mwa wanachama wake, huku kila upande ukitaka kuona mgombea wake akipewa kijiti cha kupeperusha bendera ya muungano. Kitendawili hiki kinapaswa kuteguliwa na wananchi wa DRC wenyewe.

Kitendawili cha uchaguzi mkuu huo kitateguliwa na wanasiasa hao ambao kimsingi ni miamba inayopambana.

Kila la heri kwao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles