29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi KKKT sura ya aina yake

Mwandishi wetu- Arusha

SHAUKU ya kumjua Kiongozi Mkuu wa Kanisa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ilionekana kutanda jana kwa waumini wa dhehebu hilo wakati maaskofu na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 20 wa kutoka pande zote nchini wakipiga kura kumchagua.

Mazingira ya kupatikana kwa kiongozi huyo atakeyeongoza kwa kipindi kingine cha miaka minne ambaye mchakato wake ulianza siku tano zilizopita ndiyo yaliyotoa taswira kwamba uchaguzi wa sasa umekuwa na sura ya aina yake.

Zoezi la kupiga kura jana ambalo lilitanguliwa na lile la kupitisha majina nyakati za mchana lilichukua muda mrefu ambapo hadi saa mbili usiku majina yalikuwa hayajajulikana.

Zoezi hilo lilitanguliwa na vikao vya siku nne vya Halmashauri Kuu vilivyofanyika Chuo Kikuu cha Makumira cha kanisa hilo kilichopo mkoani Arusha ambavyo pamoja na mambo mengine viligubikwa na mijadala mikali na hivyo kutoa taswira hiyo hiyo.

Gazeti dada la hili la MTANZANIA jana lilikuwa na habari kubwa iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Uchaguzi KKKT wa moto’ ikisanifu yale ya yaliyojadiliwa ndani ya vikao hivyo hali kadhalika uamuzi mgumu uliofikiwa wa kuwaondoa baadhi ya viongozi wa sekretarieti akiwamo Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Brighton Kilewa na manaibu katibu wakuu wote.

Gazeti hilo liliripoti taarifa zinazodai kuwa vikao hivyo vya Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo viligubikwa na majadiliano makali kuhusu migogoro ya muda mrefu kwenye baadhi ya dayosisi zake kama Tanganyika na Kusini unayohusisha sharika za Sumbawanga, Mpanda, Mtwara, Mafinga, Makete na Mufindi.

Hoja nyingine ni ubadhirifu wa fedha na mali za kanisa, likiwamo suala la kufungwa kwa Chuo Kikuu cha Makumira cha mkoani Mbeya hali inayotajwa kutishia chuo hicho kupokwa.

WANAWAKE WACHUNGAJI

Jana kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, baadhi ya wajumbe walionyesha kugawanyika kuridhia wanawake kuteuliwa kuwa Wachungaji katika kanisa hilo.

Aidha wajumbe hao kutoka Dayosisi 26 za Kanisa hilo,walikuwa wapitishe ajenda ya kuunga mkono wanawake kuteuliwa kuwa wachungaji katika Dayosisi zote kutokana na mchango wao katika kanisa hilo.

Wakichangia mjadala huo  katika mkutano, baadhi ya wajumbe walilalamikia kupingwa kwa suala hilo ambalo tayari lilishapitishwa na mkutano Mkuu uliofanyika Dodoma.

Dayosisi mbili za Mbulu na Shinyanga zilitajwa kuendelea na msimamo wa kuwapinga wanawake na Dayosisi ya Mara ikidaiwa kutokuwa na wachungaji wanawake wa kutosha.

Aidha baada ya mjadala,  Askofu Dk. Fredrick Shoo alipendekeza hoja hiyo ieendelea kujadiliwa ili kuongeza uelewa na mkutano ujao suala hilo liwe  limekwisha.

Awali kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Dk. Shoo aliujulisha mkutano kuwa Rais Dk. John Magufuli alimpigia simu na kumtakia Mkutano Mkuu wa kanisa hilo wenye baraka.

Aidha taarifa iliyotolewa na Katibu wa Idara ya Mawasiliano Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Mathayo Saruma jana ilieleza kuwa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani, Askofu Mkuu Dk. Panti Filibus Musa kutoka Kanisa la Kristo Nigeria alihitimisha mafundisho ya neno kuu kwa kuwataka viongozi wa kanisa kuwa wanafunzi wa Yesu kristo.

“Kuwa kiongozi wa kundi la Mungu ni kuhakikisha kuwa kuna umoja wa Kundi, kukosekana umoja ni tatizo la ndani ya kanisa na ni moja ya matatizo (mivutano na utengano) makubwa na migumu ndani ya Kanisa na migogoro inapotokea ndani ya Kanisa tunasahau kuwa tu ndugu katika Kristo hivyo tunao wajibu wa kutatua,”alisema.

“Watoto wa baba na mama mmoja hawana budi kutafuta njia ya kuishi pamoja japo wanatofautiana kimawazo, maneno na utendaji,kuwa kiongozi wa kundi la Mungu ni wito wa maisha ya kinabii,”.

“Siyo kweli kuwa wakristo washirikio katika siasa ni wabaya, ninashukuru kuwa nukuu ya leo, ‘Kiongozi mbaya anachaguliwa na raia wema wasiopiga kura’hivyo tunao wajibu wa kufundisha wakristo wajibu wao katika siasa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles