21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Uchafuzi wa mazingira kikwazo maendeleo Mto Zambezi

ANDREW MSECHU

KUTOKA katika chanzo chake wilayani Mwinilunga, iliyopo mpakani mwa Zambia, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mto Zambezi unasafirisha maji yake umbali wa kilometa 2700 na kuyamwaga katika Bahari ya Hindi.

Mto huo unaoshika nafasi ya nne kwa urefu barani Afrika, unasafirisha maji yake kupitia nchi nne, ambazo ni Zambia kilipo chanzo chake, Angola, Namibia na Botswana, kisha kuambaa tena katika mpaka wa Zambia na Zimbabwe na kuingia Msumbiji ambapo huenda kukutana na bahari ya Hindi.

Kwa mujibu wa taarifa, chanzo cha mto huo ambao unashika nafasi ya nne baada ya Mto Nile, Mto Congo na Mto Niger kiko katika mwinuko unaofikia meta 1500 kutoka usawa wa bahari.

Mto huo unatajwa kupokea maji mengi zaidi kutoka Ziwa Nyasa ambalo linachangia zaidi ya asilimia 11, maji ambayo yanatoka katika mito minne mikubwa yenye vyanzo vyake kutoka Tanzania inayoingiza asilimia 60 ya maji kwenye ziwa hilo.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, anasema kumekuwapo matatizo mengi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira ambayo yasipodhibitiwa yanaweza kuvuruga kabisa uwezo wa asili wa mto huo.

Anasema ongezeko la watu katika vyanzo vya maji, mabonde muhimu yanayotiririsha maji imekuwa changamoto katika matumizi sahihi ya maji, suala linalohitaji ushirikiano wa pamoja kulitafutia ufumbuzi.

Akizungumza katika Mkutano wa Sita wa Baraza la Mawaziri wa nchi zilizo chini ya Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (ZAMCOM), Profesa Mbarawa anasema changamoto iliyopo kwa sasa inahusu mabonde yote kutokana na ongezeko la watu kwamba, sasa matumizi ya maji yanaongezeka pia.

“Kubwa linalosumbua katika mabonde na mito yote ni uchafuzi wa mazingira ambao umekuwa mkubwa hivyo, kuchangia kupunguza vyanzo vya maji.

“Pia kuongezeka kwa ukakaji miti kumechangia kuharibu mazingira hivyo, tunahitaji kudhibiti na kuzikabili changamoto hizo ili kuhakikisha vyanzo vyote vinalindwa ipasavyo,” anasema.

Anasema jambo linalomsumbua kwenye mabonde yote ni uharibifu wa mazingira kwa sababu uendelevu wa mabonde yote unategemea jinsi serikali za nchi zote zenye vyanzo vya maji na mabonde yanayonufaika wanavyopambana kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Anasema kama nchi hizo zisipopambana vizuri na uharibifu wa mazingira itafikia pahala hata hayo maji yaliyopo yatazidi kupungua na hayataweza kutosha hivyo, ni vyema kupambana ipasavyo na uharibifu huo ili kuhakikisha maji yaliyopo yanatosha sasa na siku zijazo.

Waziri Mbarawa anasema japokuwa Tanzania hainufaiki moja kwa moja na maji ya Bonde la Mto Zambezi, ni nchi muhimu katika ustawi wa bonde hilo kwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa maji yanayostawisha mto huo ambayo hutumika kwa matumizi ya nyumbani, kuendeshea umeme, viwandani na umwagiliaji.

Mbarawa anasema kupitia wizara yake anawajibika kuendeleza ushirikiano na wadau wengine kwenye utekelezaji wa mkataba wa kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (Zamcom) ulioanza kutekelezwa rasmi kisheria mwaka 2011.

Anasema kamisheni hiyo iliundwa kwa lengo la kusimamia rasilimali za maji ya Mto Zambezi ambapo nchi nane zinatekeleza mkataba unaoanzisha kamisheni hiyo.

Nchi hizi ni Angola, Botswana, Msumbiji, Malawi, Namibia, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.

“Shughuli zote za usimamizi wa bonde zinafanywa na Sekretarieti za Zamcom (Zamsec) kwa niaba ya nchi wanachama. Makao makuu ya kamisheni hii yapo mjini Harare, Zimbabwe,” anasema.

Anasema Tanzania ni mwanachama wa kamisheni hii kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Nyasa, ambapo ndiko kilipo chanzo cha Mto Shine ambao maji yake yanaanzia katika Ziwa Nyasa na kuyamwaga Mto Zambezi.

“Kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya Bonde la Ziwa Nyasa kutokana na sababu hii, inakuwa pia sehemu ya Bonde la Mto Zambezi, hivyo kuwa na jukumu la kuhakikisha rasilimali zote za bonde hilo zinasimamiwa vyema,” anasema.

Anasema Tanzania ambayo mwaka huu imeachia uenyekiti wa mzunguko unaopokezana miongoni mwa nchi hizi nane, inaendelea kuwajibika katika nafasi ya usimamizi kwenye ngazi ya wataalamu.

Anasema jukumu lake kuu ni kusimamia na kuongoza sekretarieti ya Zamcom ili itimize majukumu yake kwa kushirikiana na mawaziri wa nchi saba zilizobaki.

Faida za Zamcom

Waziri Mbarawa anasema faida zilizopatikana kutokana na kamisheni ya Zamcom ni kufanya tathmini ya hali ya mazingira ya Bonde la Mto Zambezi inafanyika na kupitishwa.

Jukumu jingine ni kutoa miongozo ya namna ya kubadilishana takwimu, mfumo wa kubadilishana, kutumia na kuhifadhi takwimu za rasilimali za maji na kuandaa mchakato wa kutoa mafunzo kwa nchi wanachama juu ya usimamizi wa rasilimali za maji.

Anasema fainda nyingine ni uandaaji wa mpango mkakati wa Zamcom unaohusisha miradi ya maendeleo ya umwagiliaji, umeme, uvunaji wa maji ya mvua na usambazaji wa maji kukamilika.

“Pia uwapo wa kamati ya kitaifa ya wadau ambayo tayari imeshaundwa na kuundwa kwa jukwaa la wadau kikanda linalohusisha wadau kutoka nchi zote nane wanachama wa Zamcom ni mambo yanayosaidia kuimarisha usimamizi wa maji ya mto huo,” anasema.

Nafasi ya vyanzo vya maji

Waziri Mbarawa anasema katika kuwa na vyanzo vingi vya maji, kwa Afrika nchi inayotajwa kuongoza ni Msumbiji, Zambia, Sudan Kusini na Tanzania inakuwa ya nne, lakini bado wananchi wake hawajafikiwa na maji ya kutosha.

“Kuwa na maji mengi ni suala moja na kuwafikishia watu wengi maji ni suala jingine. Nchi hizo zina vyanzo vingi lakini hayajawafikia watu wengi kwa sababu miradi mingi imejengwa kwa viwango vya chini, hatua ambayo Serikali imeamua kuwekeza fedha nyingi zaidi kuhakikisha sasa inafikia viwango vinavyotakiwa,” anasema.

Profesa Mbarawa anasema wamekuwa wakishirikiana kuendeleza rasilimali watu, miradi midogo inayohusiana na mto huo kupitia mipango endelevu ya miaka 20 ijayo ili kuhakikisha Ziwa Nyasa linakuwa endelevu na Mto Zambezi unaendelea zaidi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Maji, Sylvester Matemu, anasema kwa sasa Bonde la Mto Zambezi linatarajiwa kuhudumia watu milioni 40 katika nchi nne ambazo mto huo unapita.

Anasema kuna tatizo la mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha maji kupungua hivyo, nchi zote zinalazimika kukaa pamoja ili kuwa na mipango ya kulinda rasilimali ya maji hayo.

Matemu anaeleza kuwa kuna mito minne ndani ya Tanzania inayoingiza asilimia 60 ya maji kwenye Ziwa Nyasa na kwamba japokuwa eneo la Tanzania kwenye mto Zambezi ni asilimia 2.7 pekee, ndiyo inayochangia kiasi kikubwa kwenye maji yanayowenda mto Zambezi.

Anasema hiyo ndiyo inayoifanya Tanzania kuwa muhimu katika kamisheni hiyo kwa kuwa wakati wa kupanga mipango ya miradi ya matumizi ya maji katika mito inayoingiza maji Ziwa Nyasa, inatakiwa kuangalia pia athari za maji hayo iwapo itaathiri mtiririko wake.

ends

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,814FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles