23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ubunge waipasua CCM Kilombero

Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana

Na Mwandishi Wetu, Ifakara

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilombero kimeingia katika malumbano baada ya baadhi ya makada wake kudaiwa kuanza kampeni za kuwania ubunge mwaka 2015 kabla ya wakati.

Hatua hiyo inaelezwa ni moja ya mikakati inayofanywa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ambao wamekuwa wakiwabeba watu wanaotangaza nia ya kulitaka jimbo hilo na kuambatana nao katika mikutano kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Kutokana na kile kinachodaiwa ni kampeni za kutaka kuwania jimbo hilo linaloongozwa na mbunge Abdul Mteketa (CCM), baadhi ya makada wameanza kampeni chafu kinyume na utaratibu wa chama hicho.

Viongozi hao wa wilaya wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu wa wilaya hiyo, Kanali mstaafu Haruni Kondo, wanadaiwa katika ziara ya kuimarisha chama inayofanywa na kiongozi huyo amekuwa akiwataka wajumbe wa CCM kuhakikisha mwaka 2015 wanaepuka kuwa na mbunge anayetoa fedha.

Akiwa katika ziara yake katika Kijiji cha Mang’ula, Ifakara na Utengule na Masagati, Kanali Kondo, aliwaeleza wajumbe wa CCM kuhakikisha wanachagua viongozi wanaokubalika na watu.

“Mwaka 2015 ni Uchaguzi Mkuu lakini kubwa ninalowaomba sana ndugu zangu ni kuhakikisha mnakuwa na mbunge ambaye mtakuwa naye muda wote na sio anayetamba kwa fedha zake,” alisema.

Mbali na MNEC huyo, makada kadhaa wa CCM pia wanatajwa kuanza kampeni za kuwania jimbo hilo mwaka 2015 kinyume cha kanuni za chama na maelekezo ya CCM Makao Makuu.

Mmoja wa wana CCM Mang’ula, Ally Limbanyama, alimtaka Kanali Kondo, kuhakikisha hakigawi chama kwani kauli zake zina lengo la kupinga kazi kubwa inayofanywa na Mbunge Abdul Mteketa katika utekelezaji wa ilani ya chama.

MTANZANIA lilipomtafuta Kanali Kondo, ili kuzungumzia madai ya kuanza kampeni kabla ya wakati alikanusha na kusema kuwa hajawahi kumpinga Mteketa ila alichokifanya katika ziara yake ni kuimarisha mshikamano miongoni mwa wana CCM.

“Nilisema kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuimarisha mshikamano na kujiandaa na sio kumpinga mbunge kwani nami ni mbunge wangu. Nitakuwa kiongozi wa ajabu kutoa kauli za kugawa watu,” alisema Kanali Kondo.

Kwa upande wake Mteketa, alisema kila mtu ana haki ya kugombea ubunge lakini ni lazima kanuni na taratibu za chama zifuatwe kwa sasa.

“Wanaotaka ubunge watambue muda bado, sasa waniache nifanye kazi wasubiri kwanza. Na niwaombe nitumie fursa hii kwa wana Kilombero wote Oktoba 10-14 taasisi ya Bilal Muslim itakuwa Ifakara na watapima macho na kufanya upasuaji bure wajitokeze,” alisema Mteketa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles