Ubonge tatizo Yanga

0
820

Zainab Iddy – Dar es salaam

KOCHA Msaidizi wa timu ya Yanga, Charles Mkwasa, amesema kuwa katika mazoezi ya siku tano ambayo wachezaji wamefanya mazoezi amebaini uwepo wa nyota walioongezeka uzito jambo lililosababisha awape programu tofauti na wengine.

Mkwasa alisema hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari kabla ya kuanza kwa mazoezi katika  Chuo cha Sheria, Dar es Salaam kwaajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Timu ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC).

Mkwassa alisema sababu kubwa ya wachezaji hao watano kuiongezeka uzito ni kushindwa kujipangilia aina ya vyakula walivyokuwa wakitumia pamoja na mazoezi kipindi  cha mapumziko ya janga la Corona.

“Kuna wachezaji wameongezeka uzito na kushindwa kuendana na aina ya mazoezi ninayoyatoa sasa hii, imetokana na kushindwa kwao kuchagua aina ya vyakula na  kutofanya mazoezi kipindi cha mapumziko ya corona.

“Kutokana na hilo nimelazimika kuwapa programu maalumu ambayo itawapunguza uzito na kuendana na wenzao,bila shaka hadi wiki ijayo watakuwa sawa,”alisema Mkwasa.

Wakati huo huo Mkwassa alisema kesho watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya KMC ambayo kwa upande wao wanatarajia itakuwa ngumu kutokana wapinzani wao kuanza mazoezi mapema.

“Hii itakuwa mechi ngumu kwetu kwa sababu kwanza tuna tatizo la uzito kwa wachezaji lakini pia wenzetu wameanza mazoezi siku nyingi tofauti na sisi, hata hivyo kitakuwa kipimo kizuri kwetu,”alisema.

Katika hatua nyingine kikosi cha Yanga kinatarajia kuingia kambini mara baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya KMC.

“Kambi itakuwepo mara baada ya mchezo na KMC, tayari viongozi wameshafanya mipango ya jambo hilo hili, yote ni kutaka wachezaji wawe katika ‘levo’ moja,”alisema Mkwasa.

Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea Juni 13 mwaka huu, ikiwa ni baada ya Serikali kuruhusu shughuli za  michezo kuendelea.

Awali Serikali ilipiga marufuku shughuli zinazosababisha mikusanyiko ikiwemo michezo, katazo lililoanza Machi 17 mwaka huu, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona.

Ugonjwa wa corona ambao mwa mara ya kwanza ulibainika nchini China, umesababisha vifo vya maelfu ya watu duniani.

Athari za ugonjwa huo zilisababisha ligi za michezo mbalimbali, matamasha ya burudani na shughuli nyingine za michezo kusitishwa na mataifa mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here