25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

‘UBAKAJI NDANI YA NDOA UTUNGIWE SHERIA’

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

MASHIRIKA 19 yanayotetea haki za binadamu na wanawake nchini, yamependekeza suala la ubakaji katika ndoa litambuliwe kisheria kutokana na kile walichosema linaendelea kusababisha wanawake wengi kuteseka.

Akiwasilisha tamko la kikosi kazi cha mashirika hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Naemy Sillayo kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alisema asilimia 50 ya wanawake walio katika ndoa wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Ubakaji ndani ya ndoa unaendelea, lakini ukatili huu bado haujatambuliwa kisheria, hivyo kusababisha wanawake kuendelea kuteseka ndani ya ndoa. Kuna ongezeko kubwa la matukio ya ukatili dhidi ya wanawake, vitendo hivi vinaathiri ushiriki wao kwenye shughuli za kiuchumi,” alisema Sillayo.

Tafiti zilizofanywa na LHRC zinaonyesha matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yaliyoripotiwa mwaka jana ni 7,475 huku 2,859 yalihusu ubakaji katika kipindi cha miezi sita ya kwanza.

Mashirika hayo pia yamependekeza kutungwa kwa sheria ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuanzishwa kwa mahakama ya familia, lengo likiwa ni kudhibiti vitendo hivyo ambavyo alisema vinamdidimiza mwanamke na kumkwamisha kiuchumi.

Mbali ya ukatili wa kijinsia, mambo mengine yaliyotajwa kumdidimiza mwanamke ni kuwapo kwa sheria kandamizi, kukosekana kwa fursa ya elimu, nafasi finyu za wanawake katika uongozi, huduma duni za kijamii, changamoto za ajira na kukosa mitaji kutokana na masharti magumu kwenye taasisi za fedha.

“Ufinyu wa idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi na hasa uongozi wa kisiasa, unasababisha kutungwa kwa sheria, sera na mikakati ya kitaifa isiyozingatia misingi ya usawa kijinsia na haki za wanawake,” alisema.

Kwa mujibu wa Sillayo, ushiriki wa wanawake katika uongozi ni chini ya asilimia 20.

Alisema wanawake walioko bungeni ni asilimia 30, mawaziri wakiwa ni wanne kati ya 19, wakuu wa wilaya wako 25 kati ya 134, wakurugenzi wa halmashauri 33 kati ya 185 na wakuu wa mikoa ni wanne kati ya 26.

Sillayo alizitaja sheria kandamizi zilizomo nchini kwamba ni Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 14 au 15 na sheria ya kimila ya mwaka 1963 inayomnyima mwanamke fursa ya kumiliki ardhi na kurithi mali.

Alisema sheria hizo zinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ni kinyume na mikataba ya kikanda na kimataifa inayolinda haki za wanawake ambayo Tanzania imeridhia.

Mashirika hayo yameiomba Serikali kuhuisha mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kuweza kutambua haki za wanawake na hivyo kumlinda dhidi ya vitendo vyote vya ubaguzi na udhalilishaji.

Pia yalipendekeza kuboreshwa kwa huduma za kijamii ili kumwezesha mwanamke kukabiliana na changamoto za mahitaji muhimu kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, nishati na huduma za afya.

Matamko hayo yalitolewa kwa ushirikiano na LHRC, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na Chama cha Wajane (TAWIA).

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambaye ni Rais wa Vicoba, Devotha Likokola, alisema maadhimisho hayo ni njia mojawapo ya kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani na kupima utekelezaji wa maazimio na matamko mbalimbali ya kimataifa na kikanda yanayohusu masuala ya wanawake.

“Wanawake ndio wazazi, wafanyakazi majumbani, shambani na ofisini, ndiyo maana natamani kila siku ingekuwa ya mwanamke kwa sababu hakuna siku ambayo hatujishughulishi,” alisema Likokola.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema changamoto nyingi zinazowakabili wanawake ni za kimfumo na kwamba watatumia mbinu mbalimbali kupambana nazo ili kumwezesha mwanamke kwenda mbele na kuleta mabadiliko.

“Tuthubutu kuyakabili mabadiliko, mwanamke pale alipo ajiongeze, asisubiri, azikimbilie fursa na pale zilipo zielekezwe kwa wanawake ili waweze kushiriki vizuri katika Tanzania ya viwanda,” alisema Dk. Bisimba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles