LAGOS, NIGERIA
Benki ya United Bank of Afrika (UBA) imemtangaza Abdoul Aziz Dia, kuwa mjumbe mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo baada ya kuidhinishwa na Benki Kuu ya Nigeria.
Akitangaza uamuzi huo jana Mei 9, Lagos nchini Nigeria, Mwenyekiti wa UBA Tony Elumelu alisema, Dia ambaye ni raia wa Senegal, ana ujuzi wa kibenki wa miaka 25 ambao ameupata baada ya kufanya kazi katika nchi mbalimbali ulimwenguni ikiwamo, Uingereza, Ufaransa, Nigeria, Ghana, Togo, Senegal, Kenya na Ivory Coast. amefanya kazi katika nafasi za juu za uongozi katika Taasisi za fedha za kimataifa kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Citigroup, Standard Chartered, Ecobank na UBA.
Alisema pia Dia amehudumu kama Mkurugenzi Mkuu katika kampuni nyingi Afrika na Ulaya na hivi sasa anajiunga na UBA akiwa hana nafasi yoyote ya juu katika Bodi ya Wakurugenzi. Katika upande wa elimu, Dia ana Shahada ya Uzamili katika Hesabu na Takwimu za Fedha kutoka katika Chuo cha ENSAE cha Paris, Ufaransa, ana uwezo wa kuzungumza lugha sita ambazo ni Kingereza, Kifaransa, KIjerumani, Kirumi, Kiwolof na Kifulani.
“Abdoul-Aziz Dia ni mtu ambaye ana utajiri wa ujuzi mwingi katika sekta ya kibenki, anaungana na bodi ya UBA akiwa na dhamira ya kusonga mbele zaidi na ninatumaini kuwa ana jukumu kubwa la kutekeleza kwa maisha yajayo ya UBA na hiyo itaongeza thamani kubwa katika mipango madhubuti ya ukuaji wa UBA,” amesema Elumelu.
Aida Elumelu alisema, Dia anaungana na bodi hiyo ikiwa ni mwaka mmoja baada ya UBA kuchagua wajumbe wanne wapya ili kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma zao, wamo wajumbe wanawake wawili Erelu Angela Adebayo na Angela Aneke na wengine ni Kayode Fasola na AbdulKadir J. Bello.
Ikumbukwe kuwa benki ya UBA iliasisiwa miaka 70 iliyopita nchini Nigeria na sasa inatoa huduma za kibenki katika nchi 20 za Afrika nan je ya Afrika katika nchi za Uingereza, Marekani na Ufaransa. UBA inahudumia wateja milioni 17 duniani kote ikiwa na zaidi ya matawi 1000 na vituo vya kuunganisha wateja. Mwaka 2018 benki hiyo ilitunukiwa tuzo ya Benki Bora ya Kidigitali kwa Afrika na Jarida la Bankers.