NEW YORK, MAREKANI
UMOJA wa Falme za Kiarabu (UAE) utayaunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mazungumzo mapya ya kutafuta amani Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE, Anwar Gargash, amesema walifanya mazungumzo ya tija na mjumbe maalumu wa UN kuhusu Yemen, Martin Griffiths, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Kauli hiyo ya UAE inakuja wiki mbili baada ya mkutano wa kutafuta amani Yemen uliofanyika mjini Geneva, Uswisi kushindikana baada ya waasi wa Houthi kutohudhuria.
Waasi hao waliushutumu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuwazuia kusafiri kwenda kwenye mazungumzo hayo.