24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TWCC, TADB KUWAWAWEZESHA WANAWAKE WAJASIRIAMALI

 

Bethsheba Wambura, Dar es Salaam


Chama Kikuu cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), kimeingia makubaliano na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kuwawezesha wanawake kuongeza kushiriki katika kilimo.

Akizungumza na Mtanzania Digital jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Noreen Mawalla, amesema makubaliano hayo yamefikiwa ili kuwapatia wanawake mafunzo na fursa zilizopo katika kilimo na fursa ya kukopa katika benki hiyo.

“Lengo letu kuu ni kuona wanawake wanakomboka kiuchumi, lakini pia tuna fursa ya safari ya kwenda China Oktoba ili waende kujifunza, kupanua biashara zao na kupata mawazo mapya ya ujasiriamali ambapo awamu ya kwanza tulipeleka wanawake 80 na tunategemea kupeleka wengine zaidi ya hapo,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Biashara wa TADB Eunice Mmbando, amesema makubaliano hayo ni kuhamasisha kilimo cha kisasa na kibiashara.

Amesema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), asilimia 69 ya wanawake wanajishughulisha na kilimo idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na wanaume ambao ni asilimia 64.

“Katika kuchukua mikopo mwitikio wa wanawake si mzuri ambapo zaidi ya Sh bilioni 49 zilizokopeshwa kwa wakulima ni asilimia 27 tu zimekwenda kwa wanawake.

“Hivyo tunaamini kupitia makubaliaono tuliyofikia na TWCC tutaweza kuwafikia wanawake wengi kwa sababu ina wanachama zaidi ya 4,000 ni wazi kuwa wakipata elimu watawapatia na wengine,” amesema.

Aidha amesema licha ya wanawake wengi kujihusisha na kilimo ila ni wachache wanajitokeza kutumia fursa zinazotolewa na benki hiyo na hii inasababishwa na wanawake kutoshirikishwa katika kutoa maamuzi, miundombinu duni, mfumo dume na kukosa elimu ya kilimo na biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles