Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kinatarajia kutoa tuzo za viwanda na biashara kwa wanawake wajasiriamali Tanzania na kutangaza mafanikio yao katika sekta mbalimbali.
Akizungumza leo Februari 19,2025 wakati wa uzinduzi wa maonesho na tuzo kwa wanawake wajasiriamali Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema tuzo hizo ambazo ni msimu wa tano
zitatolewa Machi 22,2025.
Amesema lengo ni kutambua wanawake wajasiriamali wanaoongoza katika sekta ya viwanda na biashara kwa ufanisi wao, ubunifu, na mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

“Hii pia itakuwa ni maadhimisho ya miaka mitano ya utoaji wa tuzo hizi, kwahiyo tunawahimiza wanawake wanaotaka kushiriki katika tuzo hizi kujaza fomu za maombi au kupendekezwa na watu wanaowafahamu na kuwasilisha majina yao kupitia mifumo ambayo tumeweka,” amesema Mwajuma.
Aidha amesema kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kutakuwa na matukio katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuonyesha mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha wanawake kiuchumi na kuunga mkono usawa wa kijinsia.
Amesema sherehe za mwaka huu zinakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mpango wa Beijing hivyo, kutakuwa na shughuli nyingi zitakazoshirikisha wanawake, vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo kutakuwa na kongamano la kuwezesha wanawake kiuchumi litakalofanyika Pemba Februari 22,2025 ambalo linalenga kuimarisha wanawake katika biashara na kutafuta fursa za ukuaji wa kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuongeza nguvu kwa wanawake wajasiriamali.
Tukio lingine ni Usiku wa Mwanamke Mfanyabiashara litakalofanyika Unguja, Zanzibar Februari 26,2025 ambalo linalenga kutambua na kusherehekea michango ya wanawake katika sekta ya ujasiriamali, uongozi, na uvumbuzi.
Vilevile amesema kutakuwa na maonyesho ya wanawake na vijana yatakayofanyika Mlimani City kuanzia Machi 1-5,2025.
“Maonyesho yatafunguliwa kwa biashara zinazoongozwa na wanawake na vijana, huku tukitazama uvumbuzi, miradi ya maendeleo na bidhaa za kipekee zinazotolewa na makampuni ya wanawake na vijana,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema pia katika kutambua na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwezesha fursa kwa vijana, wameanzisha idara maalumu inayoshughulikia masula ya vijana wote wa kike na wa kiume ili kuhakikisha wananufaika na fursa mbalimbali za kibiashara na uchumi.
Naye Rais wa TWCC, Mercy Sila, amesema wataendelea kutoa msaada na kuhamasisha wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kufikia malengo yao.
“Tunapojiandaa kusherehekea mafanikio haya ni fursa ya kutafakari na kuongeza jitihada zetu za kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa katika biashara, viwanda, na kila nyanja ya maisha,” amesema Sila.
TWCC kina wanachama 20,000 na mwaka huu kitasherehekea miaka 20 ya kuanzishwa kwake.