NA WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Twaha Kiduku amesema ushindi ni ushindi uwe wa pointi au K.O, kitu kikubwa kwake ni kwamba ameiwakilisha vizuri Tanzania na kuwapa raha mashabiki na wadau wa ngumi.
Kiduku ambaye jana aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Alex Kabangu wa DR na kutwaa ubingwa wa UBO Afrika katika pambano la raundi nane la uzito wa kati lilipigwa kwenye Ukumbi wa Tanzanite, mjini Morogoro.
Pambano hilo lililoandaliwa na kampuni ya Peak Time Media, limeshuhudiwa na mashabiki na wadau mbalimbali wa ngumi kutoka mikoa tofauti walioujaza ukumbi huo, huku Watanzania wengine wakifuatilia kupitia runinga.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Kiduku amesema alichokuwa anaomba ni kushinda kwa sababu anajua wadau wake wamesafiri kutoka sehemu mbalimbali kwenda kumsapoti.
Ameeleza kuwa ugumu ulikuwa kwa mpinzani wake ambaye muda mwingi alicheza kwa kukumbatia kumbatia lakini kikubwa ameshinda.
“Watu wametoka mikoa mbalimbali, Dodoma, Tabora, yote kwa ajili ya kunisapoti mimi, sina cha kuwalipa ila Mungu awabariki, nawapenda wadau wangu wote,” amesema Kiduku.
Naye kocha wa Kiduku, amesema ushindi huo ni zawadi kwa wakazi wa Morogoro kwa sababu muda mwingi alicheza nje ya mkoa huo.
“Kama mtu anaubeza huu ushindi atakuwa hajui ngumi, watu wamezoea kuwa kushinda ni kumpiga mtu K.O, sisi tulisema hatuji kupigana bali kucheza boxing kuonesha radha.
“Leo Twaha amecheza boxing iliyotulia jambo mpinzani alikuwa anatumia maguvu mengi, lakini kijana katulia. Maandalizi yalikuwa ya muda mfupi mwezi mmoja lakini tuliwaambia watu tunakwenda kucheza ngumi na tulimuandaa Twaha kisaikolojia na mbinu kutokana na muda.
Kwa upande wake Kabangu, amelalamika kutotendewa haki na majaji katika pambano, akisema ndiye alistahili kushinda kwa kuwa amecheza vizuri na mwisho wa siku kapewa ushindi Kiduku.
Tofauti na pambano hilo yalikuwepo mengine ya utangulizi, huku George Bonabucha akifanikiwa kutetea ubingwa wake wa PST kwa kumtwanga Juma Fundi.
Naye Karim Mandonga amechezea kichapo cha K.O raundi ya kwanza kutoka kwa Magambo Christopher, Pascal Manyota amemchapa John Luwa, Ally Furahisha amempiga Edga Kiduku.
Kwa upande wa wanawake, Stumai Muki ameibuka mshindi dhidi ya Lulu Kayage,Najma Isike alimpiga Halima Mandola.