30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TUWE MAKINI NA HOMA YA ZIKA

zika-virus-mosquito

WIKI hii kumejitokeza kile unachoweza kukiita kukinzana kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa ugonjwa wa homa ya zika nchini.

Virusi vya ugonjwa huo tayari vimeleta hofu kubwa katika nchi za Amerika ya Kusini na ile ya Kati, huku athari yake kubwa ikiwa ni akina mama kuzaa watoto wenye vichwa vidogo kuliko ilivyo kawaida.

Hadi sasa msimamo wa Serikali ni kwamba bado virusi vya zika havijathibitika kuwapo nchini.

Kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Serikali imewatoa hofu wananchi juu ya ugonjwa huo.

Ummy aliwataka wananchi waelewe kwamba taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ni matokeo ya awali ya utafiti wa ubora wa kipimo cha ugonjwa huo.

Kwamba baada ya NIMR kumaliza utafiti wao, kitapimwa tena kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika taarifa yake, NIMR ilidai kuwa asilimia 43.8 ya watoto wachanga 80 kati ya watu 533 ambao walichukuliwa sampuli na kupimwa, wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya zika.

Utafiti huo uliofanywa na NMR kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando mkoani Mwanza, ulionyesha kuwa watu hao walipata virusi hivyo kati ya mwaka 2015 na 2016.

Januari mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa taarifa kuwa ugonjwa wa homa ya zika bado haujaingia nchini na sasa imetoa msimamo huohuo wa kuwatoa hofu Watanzania.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi, alisema Serikali inafuatilia kwa karibu matokeo hayo ya utafiti yaliyotolewa na NIMR.

Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi wa NIMR, Dk. Mwele Malecela, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba wamegundua uwapo wa virusi hivyo nchini.

Dk. Malecela alisema matokeo ya awali ya utafiti huo yalionyesha kuwapo kwa virusi hivyo, lakini hata hivyo, watu waliokutwa na virusi hivyo hawakuonyesha dalili wala madhara yanayohusiana na zika.

Kwa sasa uteuzi wa Dk. Mwele umetenguliwa na Rais Dk. John Magufuli siku moja tu baada ya NIMR kutoa taarifa za zika kuwapo nchini.

Si nia ya MTANZANIA Jumapili kujadili sababu za kuondolewa kwa Dk. Mwele, lakini tunaona badala ya kuendeleza malumbano juu ya nani mwenye mamlaka ya kuutangaza ugonjwa huo, ni vyema mamlaka zikajikita katika kutoa elimu kwa wananchi.

Kwa sasa Zika ni moja ya magonjwa yanayotishia dunia. Tanzania si kisiwa. Ugonjwa huu unaweza kuingia wakati wowote, hivyo tunapaswa kuwa makini.

 Homa ya Zika ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus” na unaenezwa na mbu aina ya Aedes.

Dalili za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya Dengue, ambazo ni homa kali, kuumwa na kichwa, maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na kupata vipele vidogo vidogo kama harara.

MTANZANIA Jumapili tunawasihi wataalamu waendelee kufanya utafiti, lakini wazingatie utaratibu husika kuwasilisha matokeo yao.

Pia tunawataka Watanzania wazidi kuimarisha usafi ili kuepuka magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles