24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Tuwasaidie wanawake kuwa walezi bora

Na CHRISTIAN BWAYA

JUMA lililopita nilieleza, japo kwa ufupi, namna malezi yasivyopewa uzito stahiki katika jamii yetu. Nilitumia mfano wa‘akina mama wa nyumbani’ wanaotumia muda wao mwingi kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao.

Tukasema, wakati mwingine, tumewadharau akina mama hawa, na kuwaona kama watu wasio na kazi ya maana ya kufanya kwa sababu tu hatuoni thamani ya kile wanachokifanya kwa ajili ya jamii yetu.

Kwa upande mwingine, tulisaili athari za mabadiliko yanayotokea katika jamii zetu yanavyoathiri  vile wanawake wanavyotekeleza majukumu yao. Nafahamu, nina hakika, kuwa wanawake kwa hulka na asili yao wanapenda kulea watoto. Tofauti na wanaume, kwa mfano, wanawake wanaweza wasiwe na kipato kinachotosheleza mahitaji yao, lakini bado watafanya kila linalowezeka na kuhakikisha kuwa watoto wanapata mahitaji yao. Huo ndiyo moyo wa mwanamke ninaoufahamu.

Changamoto, hata hivyo, ni nyakati. Tunaishi katika enzi ambazo mifumo ya maisha imemlazimisha mwanamke huyu kubeba majukumu ambayo kwa asili hayakutegemewa yawe yake. Kwa mfano, siku hizi, wanawake nao kama walivyo wanaume, wanalazimika kutoka nyumbani asubuhi kwenda kutafuta mkate wa kulisha familia. 

Pamoja na sababu nyingine, kuna ukweli kuwa wanaume wengi wa kizazi hiki tumeshindwa kutekeleza wajibu wetu wa asili wa kuhakikisha familia zetu zinakuwa salama.

Matokeo yake, wanawake wamejikuta hawana namna nyingine zaidi ya kuingilia kati mkanganyiko huu wa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao. Ndiyo kusema, tunaishi kwenye nyakati zenye misukumo mingi inayofanya jukumu la kubeba familia lianze kuwa la mwanamke.

Wanaume wengi siku hizi wanatumia vipato vyao kulea nyumba ndogo au kufanya starehe na marafiki mitaani wakati familia zao wenyewe zikihangaika. Hali kama hizi ndizo zinazowalazimu wanawake katika jamii zetu kujishughulisha kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kusudi waweze kusomesha watoto wao, kulipakodiyanyumba, kukidhi mahitaji ya kila siku na hata kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika familia,wakati mwingine, kuliko hata wanavyofanya wanaume.

Juhudi hizi zinaleta changamoto nyingine isiyotarajiwa. Nani abaki na watoto nyumbani wakati mama akijaribu kuinusuru familia? Msichana wa kazi? Kituo cha malezi kwa watoto? Nafahamu kwa hakika wanawake wengi wasingependa watoto walelewe na mtu wasiyemfahamu vyema.

Nafahamu wanawake wengi wasingependa watoto walelewe kwenye vituo vya malezi katika umri mdogo. Hiyo ina maana kuwa, kama jamii, tunahitaji kufikiri ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hii inayokinza na jitihada za akina mama kuinua familia zao. Nina mapendekezo mawili;

Mosi, tujitathimini kama jamii kuona ikiwa ni kweli tunalipa uzito suala la malezi. Tujiulize,kwa mfano,tunapotafuta maendeleo tunafikiria kizazi kijacho? Tunaelewa kuwa tusipowalea watoto wetu ipasavyo maendeleo tunayojaribu kuyatafuta hayatakuwa na maana? Tunafahamu bila uwekezaji makini katika malezi, tunaweza kujikuta tunapanua magereza kama namna ya kushughulika na kizazi cha watu wasiojitambua? Hili la kwanza.

Lakini pia kuna masuala ya sera. Tujiulize, mifumo yetu ya kiutawala inatambua umuhimu wa malezi katika kujenga taifa imara lenye watu wanaojitambua? Je, mazingira ya kazi hayawezi kuruhusu akina mama wafanyakazi kulea kama wanavyofanya akina mama wa nyumbani?  Kwa nini mwanamke akijifungua asipewe muda wa kutosha kutulia na kichanga chake?

Je, mama mfanyakazi hawezi kuwekewa utaratibu wa kumnyonyesha mwanaye akiwa kazini? Itaendelea

Christian Bwayani Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano: 0754870815 Twitter @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles