27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘Tutokomeze ndoa za utotoni wasichana watimize ndoto zao’

pichaaNa Jamila Shemni – Dare es Salaam

UKOMBOZI wa mwanamke ikiwamo kutupilia mbali mila na tamaduni zilizopitwa na wakati ni jambo muhimu katika ustawi wa jamii.

Ni dhahiri kwamba hakuna nchi itakayoendelea bila kuwajumuisha wanawake katika mikakati mbalimbali. Hii ni pamoja na kuwathamini watoto wa kike na kuwapa elimu stahiki ili kutimiza ndoto zao.

Mtoto wa kike kama alivyo wa kiume, ana haki ya kupata elimu iliyo bora pamoja na mahitaji muhimu katika jamii.

Hii ni pamoja na kuhakikisha jamii inatupilia mbali mila potofu kama kumwozesha mtoto wa kike katika umri mdogo wa miaka 14 au 15.

Ni ukweli usiopingika kwamba hili huchangiwa kutokana na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayotamka umri wa mtoto wa kike kuolewa kuwa chini ya miaka 18.

Asilimia 37 ya wasichana walio na umri mdogo huolewa Tanzania. Wasichana wenye umri wa miaka 14 huozwa kwa idhini ya wazazi.

Wengi wao baadaye huripotiwa kukabiliwa na unyanyasaji nyumbani na hutengwa katika jamii huku wakikosa nafasi za kusoma na kuajiriwa.

Takwimu za ndoa za utotoni duniani zinaonyesha Tanzania ni moja ya nchi zenye viwango vikubwa vya ndoa hizo katika umri mdogo.

Kwa wastani, watoto wa kike wawili kati ya watano, huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Wadau mbalimbali wameitaka sheria hii irekebishwe wakisema inachangia kuwapo kwa ndoa za utotoni.

Mtandao wa Kupinga Ndoa za Utotoni (TECMN), ni moja ya wadau kati ya mashirika zaidi ya 35 yasiyo ya kiserikali ambayo kwa pamoja yana lengo la kutokomeza ndoa za utotoni.

Tangu kuanzishwa kwa mtandao huo mwaka 2012, umefanya juhudi mbalimbali kupinga ndoa za utotoni.

Katika mafanikio ya hivi karibuni, mmoja wa wanachama wa mtandao huo, Rebeca Gyumi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, aliwasilisha kesi mahakamani ya kupinga kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.

Wakati mwanachama huyo akishinda kesi hiyo kwa hukumu iliyotolewa na mahakama ya kutaka vipengele hivyo virekebishwe ndani ya mwaka mmoja, Serikali ilikata rufaa ya kupinga hukumu hiyo.

Mtandao huo ulishtushwa na uamuzi huo wa Serikali na umeanza kujiwekea mikakati katika kuhakikisha ndoa za utotoni zinapungua.

Hivi karibuni, mtandao wa TECMN uliendesha mafunzo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Girls Not Bride lenye mashirika zaidi ya 600 ya kiraia kutoka nchi zaidi ya 80, likiwa na lengo la kutokomeza ndoa za utotoni na kuwezesha wasichana kutimiza ndoto zao.

Mwenyekiti wa Mtandao huo, Valeria Msoka, anasema wameshtushwa na uamuzi uliotolewa na Serikali na kwamba wamekutana ili kupeana uzoefu na kupanga mikakati ya kukabiliana na uamuzi huo.

“Tunataka kujenga hoja ili suala hili liangaliwe vizuri. Lazima tuangalie jinsi gani hatua hii inaweza kutekelezeka,” anasema Msoka.

Anasema moja ya mkakati waliojiwekea katika warsha hiyo ni kutekeleza lengo la kuleta usawa wa kijinsia ambalo ni moja ya Malengo Endelevu (SDGs) ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, Tanzania inakuwa endelevu ikiwamo kuwa na usawa wa kijinsia.

“Kwa upande wa Tanzania, lengo si lazima tufike 2030, kwa juhudi tunazozifanya hata tukiwa karibu na hapo itakuwa vizuri zaidi kwa sababu tunalenga kupunguza athari anazopata mtoto wa kike,” anasema.

Naye mratibu wa mtandao huo, Dorothea Earnest, anasema mikakati waliyojiwekea ni pamoja na kuendelea kuongeza uelewa miongoni mwa jamii, kuongea na viongozi mbalimbali na Serikali ili viungane nao katika kulitokomeza tatizo hili.

“Mtandao huu umeshafanya mambo kadhaa yenye mafanikio, hivyo ni jukumu la Serikali kutuunga mkono kwa pamoja kutokomeza suala hili,” anasema Dorothy.

Ameitaja mikoa inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya ndoa za utotoni kuwa ni Shinyanga (asilimia 59), Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42), Singida (42), Rukwa (40), Ruvuma (39), Mwanza (37), Kagera (36), Mtwara (35), Manyara (34), Pwani (33), Tanga (29), Arusha (27), Kilimanjaro (27), Dar es Salaam (19) na Iringa asilimia nane.

Ofisa Mshirika Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Girls Not Bride, Lara Van Kouterik, anasema ndoa za utotoni zinawanyima uhuru watoto wa kike na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao na malengo waliyojiwekea.

“Kwa pamoja tumeazimia kupanga mikakati endelevu itakayosaidia kila mwanachama kupinga ndoa za utotoni,” anasema.

Kwa upande wake, Wakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Naemy Silayo, anasema licha ya kuwapo kwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inayotafsiri kwamba mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, bado Sheria ya ndoa ya Mwaka 1971, kifungu cha 13, inaruhusu ndoa ya mtoto wa kike chini ya miaka 18 kwa ridhaa ya mzazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles