29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Tusimamie Sheria kudhibiti mimba za utotoni- RC Mongella

Na Yohana Paul, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewaagiza wakuu wa wilaya wote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia sheria kuhakikisha wote waliohusika kuwapa mimba wanafunzi wanachukuliwa hatua kwa mjibu wa sheria.

Mongella alitoa maagizo hayo hivi karibuni wakati wa kikao cha maendeleo ya kamati ya mkoa, ambapo alielekeza iwapo mtu amebainika kumpa mimba mwanafunzi na ushahidi umepatikana basi achukuliwe hatua kwa haraka kusaidia kupunguza tatizo hilo.

Alisema viongozi walio kwenye mamlaka za serikali hasa wakuu wa wilaya wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupiga vita tatizo la mimba za wanafunzi kwani linawahusu moja kwa moja pasipo kumtegemea mtu mwingine.

“Kwa hiyo viongozi wenzangu ukisikia mtu kampa mimba mwanafunzi tuache sheria ifanye kazi, tena  jifanye hujasikia, muache apambane na hali  yake, hakuna namna nyingine, kwa sababu watoto wanazidi kuwa wengi wanaopewa mimba, ni shida kweli kweli.

“Siku moja nipo nasikiliza kero za wananchi, vinakuja vitoto vidogo vimebeba watoto, sasa hujui hata unamusaidiaje, yaani huoni kama msaada wako unaenda popote,” alisema Mongela.

Alisema ili kufanikisha zoezi hilo aliwataka viongozi hao kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata wahusika na kuwapeleka magereza na baadaye wapelekwe mahakamani kwa ajili ya taratibu za kisheria.

Alisema kusimamia sheria na kuwakamata watuhumiwa ndiyo mbinu pekee ya kumaliza mimba za utotoni kwani itasaidia wengine kujenga hofu juu ya kutenda uovu huo na  kutambua sheria zipo na zinasimamiwa.

Aidha Mongela aliwataka wakuu wa wilaya kutoishia kuwakamata watuhumiwa pekee bali kufuatilia hatua kwa hatua kesi zinapofikishwa mahakamani ili kuepusha kesi hizo kuchukua muda mrefu badala yake ushahidi unapokamilika hukumu itolewe kwa wakati.

“Na ikiwezekana muwatangaze hawa watu, na hii michakato ifanyike kwa haraka pasipo kusita ukilichelewesha mambo yanaweza kuingiliwa fanya kwa haraka kama kuna mtu wa kumusaidia  anakuja kusikia huyu mtu keshafungwa, lakini mabinti zetu wanaumizwa sana ni lazima sheria itende haki,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles