25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

TUSICHOKE KUJIFUNZA KUTENDA HAKI

MWENENDO wa mambo katika vyombo vya maamuzi na utendaji umetusukuma kwa mara nyingine tena kukumbusha umuhimu wa kutenda haki.

Vyombo hivi vinapaswa kutambua wajibu wao kuwa ni kutafuta namna ya kutatua matatizo na si kuyaongeza.

Yapo baadhi ya matukio si yote ambayo yamefanywa na vyombo hivyo na hivyo kutoa taswira ya kukomoa au kuumiza baadhi ya watu kwa makusudi.

Matukio hayo ni yale ambayo tumeyashuhudia hasa katika baadhi ya taasisi za kiserikali, vyombo vya ulinzi na usalama na vile vya kisheria.

Kwa bahati mbaya sana matukio haya tunaendelea kuyashuhudia huku kukiwa na ripoti ambazo zinaonyesha kuwa barani Afrika kwa muda mrefu sasa watu wameumizwa na vitendo vya kudhulumiwa haki zao za msingi.

Kwa mujibu wa ripoti hizo hata kutopea katika umasikini wa kimawazo na hivyo wengi kuhadaika na kauli za wanasiasa, viongozi na watu wenye nafasi katika jamii, msingi wake ni dhuluma ya haki zao za msingi.

Kwa misingi kama hiyo sisi kama  chombo cha habari tuna wajibu wa kukumbusha kwamba vyombo hivyo kila vinachofanya kabla ya kutoa uamuzi wowote basi vitambue vina wajibu wa kuchunguza, kusikiliza, kubadilisha na kuboresha.

Zipo nyakati tumeshuhudia vyombo hivi vikichukua uamuzi wa ghafla hata katika masuala nyeti sana katika mifumo ya sheria, utumishi nk.

Vyombo hivi vinapaswa kutambua kwamba chochote kitakachofanyika bila kufuata misingi hiyo tuliyoitaja hapo juu kitakwenda kuathiri mustakabali mwema wa Taifa letu.

Wakati fulani aliyepata kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, alitoa changamoto kubwa kwa watawala wa dunia.

Kwa maneno yake mwenyewe alisema; “jamii yenye haki hujengwa na wanajamii wenye haki.”

Maana yake tukitaka kujenga jamii yenye haki hatuna budi sisi wenyewe kuwa wenye haki.

Kiongozi huyo alikwenda mbali na kusema; wao kama kanisa hawana mbinu za kiufundi wala nafasi ya kuingilia mambo ya siasa moja kwa moja, lakini alibainisha wazi utume ambao alisema kama kanisa haliwezi kuuacha hata kidogo ni ule wa kuutangaza ukweli.

Ukweli si jambo ambalo linapaswa kubebwa na taasisi zetu za kidini tu bali hata katika Serikali zetu na taasisi zake, mahakama zetu, vyombo vya ulinzi na usalama kama Jeshi la Polisi, Bunge nk.

Kuna msemo mmoja kwamba; ukweli ndio utakaowaweka watu wote huru, iwe katika siasa au katika nyanja yoyote ya kijamii.

Kwa sababu hiyo tunaamini ujenzi wa jamii yenye misingi ya haki ni wajibu wetu sote lakini Serikali, mahakama na Bunge linawajibika kujenga dhamira hiyo.

Mahakama itambue kama ni taasisi ya kupigania haki, Serikali ni wakala wa haki vivyo hivyo hata Bunge.

Viongozi wakiwamo wale wa kisiasa na wananchi watambue kuwa wao ni wawajibikaji katika shughuli za kijamii na iwapo wote hawa watauzingatia ukweli ndani ya dhamiri zao zilizojengwa juu ya ukweli na ukweli tupu, basi jamii ina uhakika wa kujenga haki na amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles