23.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Tungeungana kulaani mauaji, tungeshinda

Usalama (4)SEPTEMBA 11, 2001, wakati magaidi wa kundi la al Qaeda walipotumia teknolojia ya kisasa kulipua majengo pacha ya World Trade Center, pamoja na Pentagon nchini Marekani, dunia ilizizima.  Maelfu ya watu waliripotiwa kuuawa kutokana na mashambulizi hayo na kila bara, kila nchi, kila kundi, kila mtu aliguswa na alilaani.

Septemba 21, 2013, wakati magaidi wa kundi la al Shabaab walipoingia kwenye duka kubwa la Westgate nchini Kenya na kuwamiminia risasi watu kadhaa na kusababisha mauaji ya watu 67 huku wengine 175 wakiripotiwa kujeruhiwa, dunia ilishangaa.  Watu wote waliungana kuyalaani mashambulizi yale na matamko yalitolewa kutoka sehemu mbalimbali duniani kupinga, kukemea na kulaani kile kilichotokea.

Aprili 14, 2014, wakati mabinti zaidi ya 200 wa shule kutoka Chibok nchini Nigera walipotekwa na kundi la Boko Haram, dunia ilizizima.  Kila mtu alisikitika, alikasirishwa na alilaani.  Ilifikia hatua ikaanzishwa kampeni ya ‘Bring Back Our Girls’ ambayo ilihusisha sura nyingi maarufu duniani zikiungana kudai mabinti wale warudishwe kwa wazazi wao.

Septemba 2, 2014, wakati kundi la kigaidi la ISIS lilipotoa video ikimuonyesha “Jihadi John” akifyeka kichwa cha Mwandishi wa Habari mwenye uraia wa Israel na Marekani, Steven Sotloff, dunia ilitaharuki.  Watu walikasirishwa sana na kitendo kile, walishangazwa mno na ukosefu wa utu ule na waliungana kuyalaani kwa nguvu zote na kuyakemea kwa uwezo wote.

Mei 9, 2016, wakati kundi la watu waliojifunika nyuso walipovamia Msikiti wa Ibanda Mkolani (Masjid Rahmani) jijini Mwanza na kuchinja watu watatu waliokuwa katika swala jioni ile, hofu ilitanda.  Mauaji yale yalilaaniwa kidogo, kisha siku mbili baadaye nchi ikasahau kabisa yaliyokuwa yametokea na watu wakaamua kujiwekeza katika mijadala yenye utani kuhusiana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kufukuzwa kazi na Rais kutokana na kulewa akiwa kazini.

Mei 30, 2016, wakati kundi la watu walipoamua kuvamia baadhi ya nyumba za wakazi wa Kijiji cha Kibatini, Kata ya Mzizima mkoani Tanga na kuishia kuchinja watu wanane, hofu ilitawala.  Wakati wengine walijitahidi kulaani na kuwasaka watu ambao wamehusika na mauaji hayo, wengine wenye sauti pia waliamua kuandaa mikutano nchi nzima kuzunguka kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni hadi baadhi ya wabunge wa upinzani kufukuzwa. Hiyo ndiyo tofauti kati ya sisi na wenzetu wa dunia nyingine.

Wiki mbili zilizopita katika ukurasa wangu huu, niliandika makala kuhoji sababu ya Watanzania kuyapuuza mauaji yaliyokuwa yametokea msikitini mkoani Mwanza na nilisema kwamba tunaonekana wa ajabu sana kuwa Taifa linaloshabikia zaidi Waziri aliyefukuzwa kutokana na ulevi na kusahau kabisa kwamba wapo watu, Watanzania wenzetu ambao wameuawa.  Wapo walionisikiliza.

Mauaji yameendelea kutikisa baadhi ya mikoa nchini kwetu  na wiki iliyopita, watu wanane wamevamiwa huko Tanga wakiwa kwenye nyumba zao.  Walichukuliwa, wakacharangwa kama vile sio binadamu, wakaaga dunia.  Mimi najiuliza tu swali dogo:  Watanzania tunafanya nini? Tumeungana? Tunalaani? Tunakemea? Tunapinga?  Tunakasirishwa? Au tunaishia kusoma kwenye vyombo vya habari yaliyotokea na kisha kuamua kuendelea na shughuli zetu kana kwamba maisha bado ni kama jana?

Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu amesema wazi kitu ambacho nilitaka nikisikie kinasemwa.  Kwamba mauaji ya Tanga ni ugaidi.  Sasa, kama ni ugaidi, mbona nchi iko kama vile haijali sana?

Nimesema hapo juu, wenzetu wa nchi zingine wakikumbwa na matukio kama hayo, mambo mengine yote yanasimama. Vipindi vyote vya kawaida vingesimamishwa na vingeanza kwa kuzungumzia yale yaliyotokea, kuyapinga, kuyalaani  na kuahidi kushirikiana na vyombo vya dola mpaka pale waliohusika na mauaji wafikishwe mbele ya haki.

Nauliza tena kama nilivyouliza wiki iliyopita.  Tunasubiri wachinjwe watu wangapi? Tunasubiri watu wangapi wacharangwe mapanga? Tunasubiri damu za watu wangapi ziendelee kumwagika?  Tunataka wafe ishirini?  Au hamsini? Au mia mbili? Mshipa wa kushtuka utafanya kazi pale tu ikitokea mtu mwenye jina kubwa zaidi akishambuliwa?

Mauaji ya namna hii yakitokea, kisha watu ambao tunawatarajia watoe  tamko wakanyamaza, huwa ninapata wakati mgumu sana wa kujua kama wenzetu wale wenye sauti zaidi kuliko wengine huwa wana nia ya kweli na moyo wa dhati wa kuwatetea wananchi, ama ajenda zao ni za kujitafutia umaarufu kwa njia zingine wanazoona wao kwamba huenda zina tija.

Lakini, tuseme ukweli jamani. Mauaji kama hayo yaliyotokea yanapotokea, mimi na nina uhakika watu wengi wengine tulitarajia yale mashirika ya kutetea haki za binadamu, ambayo ikitokea wanasiasa wamefukuzwa bungeni kwa sababu za kinidhamu, huwa wanaamka na kuwatetea kwa nguvu zote, basi na hapa wangesikika sana.  Ni kinyume cha haki za binadamu kwa mtu mmoja kumuua mwingine kinyama kama ilivyotokea na mimi ningetarajia ‘Press Conference’ za maana na kampeni mwendelezo ili kulizungumzia hilo na kulipigia kelele hadi lisijirudie tena.  Hata hivyo, sijasikia.

Nilitarajia pia hata wale wakuu wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga “manyanyaso” yanayofanywa dhidi yao na wanaoongoza vikao vya Bunge, basi wangegundua pia kwamba hili la mauaji ni manyanyaso ya kiwango cha juu kabisa.  Nilitarajia niwasikie wakitaka kuzunguka nchi nzima kuyapinga na kuyalaani mauaji hayo na kwa sauti moja waliyokuwa nayo katika kuitetea Katiba ya wananchi wakati ule, basi nguvu hiyo hiyo itumike kuyatetea maisha ya wananchi hao hao ambao ndio wanaodai kuwawakilisha.

Nilitarajia pia niwasikie hata wasanii wetu, kwa nafasi muhimu kabisa waliyonayo katika jamii, wakitumia matamasha yao mbalimbali kuzungumzia yale yanayotokea.  Yaani nguvu ile ile wanayoitumia kutunga na kuimba tungo zenye kuwalaani wenzi wao wa zamani, itumike pia katika kulaani mauaji yanayotokea kwa Watanzania wenzao.

Tujifunze kwa wenzetu.  Ndo ndo ndo si chururu! Lakini pia, usipoziba ufa utajenga ukuta.  Naomba nitahadharishe tu kwamba huenda tunadharau mauaji yanayoendelea, huenda tunaona wanaouawa si watu wenye majina, huenda tunaona idadi ya wanaochinjwa ni ndogo sana.  Lakini, tusipokabiliana nayo hivi sasa, kama Taifa, litatushinda huko mbele.

Ifike hatua kila mtu atumike kwa nafasi yake na kuona mambo mengine kama haya yanayotokea ni ‘priority’ kuyashughulikia haraka sana.  Ifike hatua, tuone vitu vingine ni muhimu na vinatakiwa kupewa kipaumbele.

Ifike hatua, tujue kwamba jukumu la kupinga, kulaani, kukasirika na kuungana kutafuta kuyakamata haya magaidi yanayotuchafulia nchi yetu, ni letu sote.  Ifike hatua tujivunie Utanzania wetu na kujivunia kuyafichua yale majitu ambayo yanataka kutuchafua.  Kama ni Watanzania wenzetu, wakamatwe na kuchukuliwa hatua stahiki; kama si Watanzania wetu, tuwashughulikie inavyostahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles