31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

‘Tundu Lissu mgongwa’

Tundu Lissu
Tundu Lissu

* Aenda kutibiwa nchini Ujerumani, Mahakama yaonya

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

WADHAMINI wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), wameonywa na mahakama kwa kushindwa kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani siku ya kesi, huku ikielezwa mshtakiwa huyo ni mgonjwa.

Kutokana na hali hiyo ilielezwa mahakamani hapo kuwa, mbunge huyo ni mgonjwa na amekwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu.

Hatua hiyo iliifanya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba jana kutoa onyo  ambapo juzi alitoa amri kwa Lissu kufika mahakamani hapo ili ajieleze kwanini asifutiwe dhamana kwa tabia ya kushindwa kuhudhuria katika kesi.

Kabla ya Hakimu Simba hajatoa onyo hilo alitoa nafasi kwa wadhamini Ibrahimu Ahmed na Robert Katula kujieleza kwanini walishindwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kuhakikisha waliyemdhamini anafika katika kesi.

Walidai kwa nyakati tofauti kwamba walikuwa wanaamini juzi mshtakiwa angekuwepo mahakamani kisha asafiri kuelekea Ujerumani kwa ajili ya matibabu ndiyo sababu iliyofanya nao wasifike mahakamani.

“Mheshimiwa nitahakikisha siku ya kesi mshtakiwa anafika mahakamani, ikiwezekana hata nimsubiri uwanja wa ndege siku ya kurudi nije naye mahakamani,”alisema Robert.

Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa Lissu ni afisa wa mahakama ni vema angefuata masharti ya dhamana  na kwamba  hati yake ya kusafiria iwasilishwe mahakamani na awe anaomba kibali cha mahakama kusafiri nje ya nchi.

Wakili wa Lissu, Peter Kibatala  alidai kuwa kila mtu ana haki ya kuaminiwa na kwamba wadhamini  wametoa taarifa kwa wakati na akaihakikishia mahakama kuwa Lissu anaiheshimu mahakama na utaratibu wake na kwamba hali hiyo haitajirudia na atakaporejea ataomba msamaha kwa kilichotokea.

“Natoa onyo, hali hii ikiendelea kujirudia mtaamuriwa kulipa dhamana, mnatakiwa kuhakikisha anafika mahakamani, siwezi kuwauliza suala la kufuta dhamana, hilo anatakiwa kuulizwa mshtakiwa mwenyewe ili ajitetee,”alisema hakimu na kuahirisha kesi hadi Oktoba 4 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wengine  katika kesi hiyo ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na  Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob ambao awali walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa‎ za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam,  walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob  anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala,  Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Alidai mshtakiwa huyo pia  alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016,  Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles