Na Asifiwe George, Dar es Salaam
MBUNGE Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), jana alijisalimisha polisi na kuhojiwa zaidi ya saa moja kuhusu habari iliyosababisha kufutwa kwa gazeti la Mawio kwenye daftari la Msajili.
Akizungumza Dar es Salaam jana baada ya mahojiano na polisi, Lissu alisema alifika kituoni hapo baada ya kupokea wito kutoka kwa maofisa wa jeshi hilo kumtaka ajisalimishe Kituo Kikuu cha Polisi.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema alifika kituoni hapo saa 4:00 asubuhi akiwa amefuatana na mawakili wake watatu, Peter Kibatala, Fredeli Kihwelo na Hekima Mwasibu.
Mawakili hao pamoja na mteja wao walikaa kwa muda mrefu kituoni hapo bila kuambiwa chochote kabla ya kuwauliza maofisa wa polisi sababu za wito huo.
Lissu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi walimwambia aliitwa kituoni hapo kama mtuhumiwa wa uchochezi baada ya kufanyiwa mahojiano na gazeti la Mawio na kunukuliwa katika habari iliyopewa kichwa cha habari kwamba ‘haki isipotendeka Zanzibar upo uwezekano wa kumwaga damu’, habari ambayo ilisababisha gazeti hilo kufutwa.
“Rais Magufuli amevalishwa mzigo wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete hivyo kwa sababu yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu anahusika moja kwa moja hivyo suluhisho la siasa Zanzibar lisipopatikana Rais wetu anaweza kuburuzwa katika Mahakama za kimataifa (ICC).
“Waliofuta uchaguzi Zanzibar walitumia nguvu za jeshi, sasa polisi nao wanataka kutumia nguvu za kutuziba midomo …bado ninaendelea kusisitiza kuwa suluhisho la Zanzibar lisipopatikana upo uwezekano wa kumwaga damu hivyo hatutakubali kuzibwa midomo kuhusu uchaguzi wa Zanzibar,” alisema Lissu jana.
Lissu alisema baada ya kumaliza mahojiano na polisi alielezwa kuwa jalada lenye maelezo yake litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na endapo atahitajika atapewa taarifa.
Alisema miaka 15 iliyopita polisi waliwahi kumuhoji kwa saa sita kuhusu mgogoro wa madini kati yake na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.