30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tunazingatia Sheria na haki za binadamu Ngorongoro-Serikali

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Tanzania imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kwamba inaheshimu haki za binadamu pamoja na Sheria za nchi katika suala la Ngorongoro na kwamba kila kinachofanyika ni kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Juni 21, 2022 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati akitoa ufafanuzi kwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuhusu eneo hilo la Ngorongoro kufuatia kuwapo kwa taarifa za upotoshwaji.

“Niuhakikishie umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania inazingatia na kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu na hakuna nanma itaendesha mipango yake kwa kukiuka sheria za haki za binadamu.

“Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mpango wa kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro nchini kwa wananchi kuridhia kuhama kwa hiari yao na hakuna aliyeondolewa katika eneo hilo kwa nguvu kama inavyoelezwa na wale wasiotutakia mema.

“Tanzania siku zote italinda watu wake, maliasili zake na mipaka yake kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amesema Balozi Mulamula.

Awali, akitoa ufafanuzi katika kikao hicho maalum kwa ajili ya kuielezea Jumuiya ya Kimataifa iliyopo nchini, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro amesema kinachoendelea katika eneo la Ngorongoro kwasasa ni uhamaji wa hiari wa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la Ngorongoro na sio kwamba kuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa na serikali.

“Serikali imekuja na mpango wa kulinda eneo la Ngorongoro, imechukua miaka 20 kuandaa na kuratibu mpango huu, ambao unatekelezwa sasa na hakuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa kwa wanachi kama inavyodaiwa, wananchi husika wameshirikishwa vya kutosha na ndio maana wamekubali na kuamua kuhama kwa hiari wenyewe,” amesema Dk. Ndumbaro.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza kwenye mkutano wa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.Mkutano huo umefanyika leo Juni 21,2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema, Katiba ya Tanzania inasema watu wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kuishi popote na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu wananchi wake wote bila ya kujali rangi, kabila au dini zao.

Amefafanua kuwa wananchi wamepewa umiliki kwa miaka kadhaa na endapo itaonekana kuna haja ya kuichaukua ardhi hiyo anayeimiliki hulipwa fidia na kupewa ardhi katika eneo lingine na kuongeza kuwa wananchi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro wanalipwa fidia na kupatiwa nyumba za makazi, maeneo yenye huduma za kijamii na ardhi kwa ajili ya malisho ya mifugo. 

Upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema kwamba katika wilaya ya Ngorongoro kuna maeneo mawili ambayo yamekuwa yakizua mjadala ambayo ni eneo la hifadhi la Ngorongoro ambalo ni urithi wa dunia na Pori Tengefu la Loliondo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza kwenye mkutano wa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwaelezea mpango wa Serikali katika kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro.Mkutano huo umefanyika leo Juni 21,2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amebainisha kuwa serikali imechukua uamuzi wa kutekeleza mpango huo kutokana na changamoto kadhaa ambazo zinatishia uhifadhi wa eneo la Ngorongoro na kuongeza kuwa uhamaji wa hiari unaofanyika katika eneo la Ngorongoro una lengo la kuendelea kuhifadhi eneo hilo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Akizunguma katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amewahahakikishia wanadiplomasia nchini kuwa zoezi hilo lilihusisha wananchi wa jumuiya zote waliokuwa wakiishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuahidi kuwa majadiliano bado yanaendelea ili kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na uelewa wa pamoja katika suala hilo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa azma ya uhifadhi wa hifadhi ya Ngorongoro.

Mkutano huo uliohusisha viongozi waandamizi wa serikali kutoka Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Maliasili na Utalii, Katiba na Sheria pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Arusha na Tanga.

Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakiwa katika mkutano uliowakutanisha pamoja na Mawaziri wa Tanzania leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulilenga kuwafahamisha wanadiplomasia walioko nchini juu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhama kwa hiari kunakofanywa na wananchi waliokuwa na makazi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na hivyo kuondoa sintofahamu iliyokuwepo kuwa wananchi hao wanahamishwa kwa nguvu na serikali na hivyo kukiuka haki za binadamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles