26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI

Na Christian Bwaya,

SIKU hizi shule za msingi za bweni zimekuwa maarufu mno. Kimsingi, si tu shule za msingi, lakini hata shule za awali za bweni. Hivi sasa, miji karibu yote katika nchi hii inazo shule kadhaa zinazopokea watoto wadogo na kuwasomesha kwa mfumo wa bweni.

Takwimu rasmi za hivi karibuni hazipatikani. Lakini kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, mwaka 2012 nchi yetu ilikuwa na shule za msingi 684 zenye huduma ya bweni. Shule hizi zinafahamika pia kama shule zinazotumia Kiingereza kama lugha rasmi ya kufundishia, yaani English Medium, zikimilikiwa na watu binafsi au taasisi zisizo za umma.

Kufikia mwaka 2013, mikoa yote kwa Tanzania bara, isipokuwa Lindi ilikuwa na shule hizi. Hata hivyo, mikoa inayoongoza kwa wingi wa shule za bweni ni Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Mwanza.

Ongezeko kubwa la mahitaji ya shule hizi za bweni linaweza kuelezeka kwa sababu kadhaa. Mosi, ni matarajio makubwa waliyonayo wazazi kwa elimu ya watoto wao. Ukubwa wa matarajio hayo unachochea kufanyika kwa jitihada za kila namna katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora pengine kuliko ile waliyoipata wazazi.

Kwa kuwa mzazi angependa mwanae afanye vizuri kitaaluma, shule ya bweni inakuwa sehemu ya jawabu mujarabu. Kwa kumpeleka mtoto kwenye shule ya bweni, mzazi anaamini huko mtoto atajengewa mazingira ya kumsukuma kujifunza bila bughudha.

Aidha, kuna suala la changamoto za kimalezi wanazokabiliana nazo wazazi. Migororo ya kifamilia inayozorotesha uhusiano baina ya wazazi, huweza kusababisha uhitaji wa shule ya bweni kwa nia ya kumlinda mtoto na matatizo yasiyomhusu. Katika mazingira haya, inawezekana wazazi wasingependa kukaa mbali na watoto lakini wakijikuta hawana uchaguzi mwingine bora zaidi ya kumpeleka mtoto katika shule ya bweni.

Kadhalika, yapo mazingira ambayo wazazi hawawezi kuwa karibu na watoto wao. Aina ya kazi wanazofanya wazazi pia zinaweza kuwafanya washindwe kuwapa watoto huduma za karibu. Katika mazingira ambayo wazazi wanalazimika kuwa nje ya familia kwa muda mrefu kwa sababu za kikazi, shule ya bweni inakuwa mbadala wenye unafuu.

Shule hizi, hata hivyo, zimepigwa marufuku kwenye nchi nyingi ikiwamo Rwanda. Hata hapa kwetu, mwaka 2015, serikali kupitia Wizara ya Elimu iliwaonya wazazi juu ya hatari ya kuwapeleka watoto wadogo kusoma kwenye shule za bweni. Hoja ni uwezekano wa watoto hawa wadogo kiumri kupatwa na madhara anuai ya kitabia yanayotokana na mazingira ya bweni. Tamko hili rasmi lilizingatia ukweli kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwapo ongezeko kubwa la shule za bweni.

Tunapozungumzia shule za msingi za bweni, kimsingi, tunazungumzia shule zinazopokea watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi 12 wanaotengwa na familia zao kwa lengo la kuwapatia elimu inayokwenda sambamba na malezi.

Mtoto huyu, kwa kawaida hukabidhiwa kwa mamlaka za shule na hukaa mbali na familia yake kwa muda unaoweza kufikia na hata kuzidi miezi saba kwa mwaka. Katika kipindi chote hiki, mtoto huishi na watoto wenzake shuleni chini ya uangalizi wa walezi na walimu. Wazazi na ndugu wanaotambuliwa na uongozi wa shule ya bweni huruhusiwa kumtembelea mtoto.

Itaendelea wiki ijayo…

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles