23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI -7

Na CHRISTIAN BWAYA


TUMEKUWA tukijadili faida na hasara za shule za msingi za bweni kwa makuzi ya watoto wadogo. Kiini cha mjadala huu kimsingi ni kuibuka kwa utamaduni mpya wa kuwapeleka watoto kusoma kwenye shule za bweni katika umri mdogo. 


Mjadala huu umetumia matokeo ya tafiti mbalimbali zilizochunguza kwa kina tabia za watoto wa bweni kiakili, kimahusiano na hata katika uwezo wa kujitegemea. Sambamba na tafiti hizo, moja wapo ya rejeo ni utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya uliolinganisha watoto wa bweni na wa kutwa katika shule kadhaa hapa nchini. 

Mambo yanayojitokeza
Kwa mhutasari, tunaweza kusema shule za msingi za bweni zina faida na hasara zake. Kwa upande wa faida, tumeona, mtoto anakuwa kwenye mazingira yenye unafuu zaidi yanayomhamasisha kujifunza kwa ufanisi kuliko nyumbani. 


Mtoto wa bweni, kwa mfano, anabanwa na ratiba inayomlazimisha kutumia muda wake vizuri. Hii, kimsingi, ndiyo sababu kubwa inayowafanya wazazi wengi kuamua kuwapeleka watoto wadogo kwenye shule za bweni.


Faida hiyo, hata hivyo inaambatana na hasara kadhaa. Kwanza, mazingira ya shule za bweni kwa kiasi kikubwa yanamnyima mtoto kujifunza ujuzi na stadi za maisha. Kama tulivyoona, watoto wengi wa bweni hawaonekani kuwa na uwezo wa kufanya mambo mengi bila usaidizi wa karibu wa watu wazima.


Lakini pili, mazingira ya shule ya bweni yanaonekana kukuza tabia hasi. Mifano mikubwa inayotajwa ni upweke wa nafsi unaotokana na mtoto kukosa ukaribu na watu wa familia yake. Upweke huu ndio unaochipusha tabia zisizofaa kwa mtoto kama vile kudeka, kulia lia, kukosa kujiamini, hasira, ugomvi na hata uongo. Kadhalika, mtoto wa bweni anakuwa na uwezekano wa kujifunza tabia zisizofaa na wakati mwingine zinazomzidi umri ukilinganisha na mwenzake anayeishi nyumbani.


Shule za msingi za bweni hazifai kwa ukuaji mzuri wa watoto wadogo. Ingawa ni kweli wakati mwingine mazingira ya nyumbani yanaweza kuwa mabaya na hatarishi, bado hata hivyo, mazingira hayo yana unafuu mkubwa kuliko mazingira ya bweni.


Unafuu wa mazingira hafifu ya nyumbani unatokana na ukweli kuwa katika mazingira hayo, angalau mtoto anaweza kukutana na watu anaowafahamu. Kuishi na watu anaowaamini, hata kama hawapatikani, ni msingi wa kukuza tabia njema kwa mtoto.


Hitimisho la pili ni kuwa faida ndogo inayoweza kumshawishi mzazi kumpeleka mtoto kusoma kwenye shule za bweni katika umri mdogo haizidi hasara zinazoambatana na uamuzi huo. Kwa mfano, ingawa ni kweli kuwa mtoto wa bweni anakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri kitaaluma, tofauti hiyo ina uwezekano mkubwa wa kupungua kadri mtoto anavyoongezeka kiumri. 


Kadhalika, mzazi anayeishi na mwanae nyumbani, anaweza kuweka mazingira mazuri kumwezesha mwanae kujifunza kama –na hata kumzidi– mwenzake anayeishi bweni. Kwa mfano, mzazi akiweza kuhakikisha kuwa mtoto anapata vifaa anavyovihitaji, anaongozwa na ratiba inayoeleweka, hatakuwa na sababu ya kulazimika kumpeleka mwanae bweni.


Pamoja na hayo, ni dhahiri kuwa yapo mazingira yanayoweza kulazimu mzazi kumpeleka mtoto bweni. Wiki ijayo tutaangazia ushauri kwa wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa huduma ya shule za msingi za bweni –pale inapolazimu–haiambatani na matatizo ya kitabia tuliyoyaona.

Itaendelea


Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles