22.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Tunavyoweza kujenga urafiki imara na watu

Multiracial Group of People Jumping at Beach, Backlight

Na CHRISTIAN BWAYA,

KATIKA zama hizi za maendeleo ya kidijitali, ni rahisi mno kufahamiana na watu wengi ambao, hata hivyo, wanaweza wasiwe marafiki. Unaweza kwa mfano, kuwa na ‘marafiki’ 5000 kwenye mitandao ya kijamii, lakini usiwe na rafiki hata mmoja katika maisha halisi.

Marafiki wa kweli ni hitaji la muhimu katika maisha. Tunaweza kuwa na sababu nyingi kuhalalisha kwanini hatuna haja na marafiki wa karibu.  Hata hivyo, zipo nyakati hufika tukajikuta katika maisha ya upweke na msongo wa mawazo kwa sababu hatukutengeneza urafiki wa karibu na watu tunaofahamiana nao.

Rafiki wa karibu ni mtu mnayefahamiana kwa karibu kiasi cha kuweza kuaminiana na hivyo kushirikiana mambo mengi bila wasiwasi wa kugeukana. Urafiki wa karibu humfanya mtu awe tayari kumchukulia mtu mwingine kama ndugu yake na hivyo kumsaidia kufikia ndoto zake. Aidha, marafiki ni watu walio tayari kutuinua tunapopita katika nyakati ngumu. Ndio kusema, si kila mtu anaweza kuwa rafiki wa karibu.

Marafiki tegemezi

Kwa ujumla, tunaweza kuwagawa  marafiki katika makundi mawili makubwa; marafiki tegemezi na marafiki wainuaji. Marafiki tegemezi ni wale tunaowazidi katika mengi na hivyo wanajifunza zaidi kwetu. Katika mazingira ya ubinafsi unaotawala maisha yetu ya kisasa ni rahisi kuwaona marafiki hawa kama mizigo tunayohitaji kuitua pale inapowezekana. Hata hivyo, kadri tunavyozidi kujitambua, ndivyo tunavyoweza kuwachukulia kama sehemu ya mafanikio yetu.

Marafiki wainuaji

Marafiki wainuaji ni wale wanaotuzidi kiroho, kiufahamu na kiuzoefu na hivyo tuna mengi ya kujifunza kwao kuliko wao wanavyojifunza kwetu. Katika hali ya kawaida, ni rahisi mno kuwapenda na kutaka kuwa nao karibu kwa sababu tunajua wametuzidi. Lakini kwa kutumia kanuni ya kuwatendea wengine vile tunavyopenda kutendewa, tunaweza kuona nafasi ya aina zote hizi za marafiki katika kufanya maisha yawe mduara wa kutegemeana.

Kwa hakika, urafiki wa karibu hauwezi kutokea hivi hivi. Urafiki ni kama uwekezaji unaodai gharama kubwa hasa katika hatua za mwanzo kabla ya kufikiria faida. Tuone baadhi ya gharama hizo tunazolazimika kuzilipa ili kujenga ukaribu na marafiki zetu.

Kuwekeza muda

Muda ni gharama ya kwanza kutuweka karibu na watu.  Tunalazimika kutoa muda wetu kuwatafuta na kuwasiliana na watu tunaotaka kujenga urafiki nao pasipokusubiri watutafute. Ni rahisi kujenga urafiki kwa kufanya jitihada za kupatikana hata katika nyakati ambazo hatuoni kama tunawahitaji.

Kwa kawaida watu hawavutiwi na marafiki tegemezi na kwa kweli wanajipenda wenyewe. Tunaposubiri watutafute au watupende, tunaweza kungoja. Kama tunataka kuwapata tunalazimika kufanya bidii ya kuwatafuta. Kuwatafuta watu tunaowaita marafiki wakati tunapokuwa na shida kunazorotesha ukaribu wa kirafiki.

Kuaminika

Watu hawajengi uhusiano wa karibu na mtu wasiyemwamini. Wangependa kuwa na mtu wasiye na wasiwasi naye. Ili kuaminika, tunalazimika kujenga tabia ya kuwa waaminifu kwa mambo yao. Uaminifu ni pamoja na kutunza ahadi zetu na kutovunja makubaliano na watu tunaowaita marafiki.

Kadhalika, kutunza siri za wengine ni jambo la lazima. Tunapotambulika kwa sifa ya kuongea na watu tunaokuwa nao badala ya kuongelea watu wasiokuwepo, tunajenga kuaminika. Kusema mambo ya watu wasiokuwepo, ni kujipunguzia imani bila kujua.

Itaendelea…

Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected], 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles