30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Tunategemea mageuzi makubwa sekta ya biashara

Na MWANDISHI WETU

RAIS  Dk. John Magufuli, wiki iliyopita alikutana na kufanya mazungumzo ya siku moja na wawakilishi wa wafanyabiashara  nchi nzima, Ikulu, Dar es Salaam ili kujadili changamoto zinazowakabili na  jinsi ya kuzitatua.

Mkutano huo, ni  jitihada zinazoendelea kuleta uboreshaji katika sekta ya biashara.

Rais amesema kuna changamoto mbalimbali kwa upande wa Serikali na wafanyabiashara wenyewe ambazo zimekuwa kikwazo katika kufanya biashara zao

Pamoja na mazingira mazuri yaliyopo, Rais Magufuli amesema kuna vikwazo vinavyosababishwa na wafanyabiashara ambavyo ni pamoja na ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi yao na  vitendo vya rushwa ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo.

Amesema kuna kampuni 17,446 zinakwepa kodi kwa njia ya mauzo hewa ya biashara za ndani na nje, manunuzi hewa kutoka kampuni hewa na kuagiza kampuni hizo kuchunguzwa zaidi na zikithibitika kukwepa kodi zitalazimika kulipa kodi hiyo katika kipindi cha siku 30 kuanzia sasa.

Tunakubaliana na rais kuwa yapo matatizo mengi katika sekta ya biashara, lakini tunaamini mkutano wake, utakuwa umefungua ukurasa mpya kwa wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.

Katika hili, lazima watumishi wa Serikali ambao wanatajwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, wafike wakati watambue dhamana waliyokabidhiwa ya kuwatumikia Watanzania.

Tunasema hivyo kwa sababu kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikikemea watumishi na wananchi wenye tabia ya kupokea au kutoa rushwa.

Tunaamini wapo hata baadhi ya wafanyabiashara si waaminifu, wanatoa rushwa kwa maofisa wa Serikali ili wapate mizigo au vibali kwa njia za panya.

 Tumeshuhudia kuwapo na wimbi kubwa la udalali wa biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho.

Lakini pia, wafanyabiashara wengi wanadaiwa kuhujumu uchumi kwa kutokuwa wawazi katika mahesabu yao kwa kuwasilisha vielelezo tofauti vya taarifa za fedha zinazopelekwa benki na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini sasa tunaamini kwa mkutano huu majibu yatapatikana.

Pia tunakubaliana na rais kwamba uwapo wa utitiri wa taasisi za udhibiti kama vile TRA, OSHA, TBS, TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu, Tume ya Ushindani, EWURA na SUMATRA  nako ni chanzo kikubwa cha kusabisha mianya ya rushwa na kuzua mwingiliano kimajukumu na kutoza tozo mbalimbali zinazofanana, hivyo kudhoofisha ukuaji wa biashara.

Umefika wakati sasa, Serikali ikaingilia kati na kupunguza taasisi hizi zikabaki chache kwa manufaa ya Watanzania. Kama kuna taasisi ambazo kazi zake zinafanana basi ni vizuri zikaunganishwa ili kupunguza usumbufu.

Uamuzi wa Serikali kuandaa kitabu cha mwongozo, ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuwabana watumishi wake kuliko ilivyo sasa.

Umefika pia wakati sasa wa mamlaka husika za Serikali kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati kama ilivyofanyika kwa wafanyabiashara wakubwa.

Katika nchi yoyote duniani, wafanyabiashara wadogo na wa kati ndio kitovu cha kukuza uchumi, ni jambo la busara kama  wataendelezwa  na kupewa misingi  madhubuti, kama ambavyo sasa wameanza kupewa vitambulisho.

Sisi MTANZANIA, tunasema baada ya mkutano huu, Watanzania wanategemea kuona mapinduzi makubwa katika sekta biashara. Tunaamini malalamiko ya wafanyabiashara yatafanyiwa kazi vizuri, ikiwamo kubambikizwa kodi na mamlaka zinazohusika.

Pia wafanyabishara nao, watakuwa mstari wa mbele kuhakakikisha wanakuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa wakati na kuachana na njia za panya ambazo mwisho wa siku husababisha biashara zao kufungwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles