26.7 C
Dar es Salaam
Sunday, December 15, 2024

Contact us: [email protected]

‘Tunataka rais mwenye hofu ya Mungu’

Pg 1Na Debora Sanja, Dodoma
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amewataka Watanzania kuhakikisha rais watakayemchagua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, lazima awe na hofu ya Mungu.
Dk. Bilal, alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana, wakati akizungumza katika hafla ya kusimikwa kwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya.
Alisema kiongozi huyo, mbali na kuwa na hofu ya Mungu, lazima pia aweze kuongoza nchi bila kuwa na ubaguzi wa aina yoyote.
“Wakati tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu, viongozi wa dini liombeeni taifa, ili wananchi waweze kufanya uamuzi sahihi kwa kumchagua kiongozi atakayeongoza kwa misingi ya amani, haki na upendo.
“Tuwakemee wale wanaotaka uongozi kwa migongo ya wanyonge, Serikali itahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na upendo,” alisema.
Aliwataka waumini wa dini zote kuzidi kupendana na kuvumiliana kwa kuwa hakuna dini bora kuliko nyingine.
“Ni marufuku kwa mtu yeyote kukashifu dini au imani ya mtu mwingine, anayefanya hivyo ajue anavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano na hatakuwa salama katika vyombo vya sheria,” alisema.
Aliwataka Watanzania kutolipa ovu kwa ovu, ikiwamo kutolipiza visasi kwa kuwa Mwenyezi Mungu katika maandiko yake matakatifu alishasema visasi ni juu yake.
“Viongozi wa dini himizeni upendo, watu wapendane na kumpenda Mungu, huwezi kuwa na amani bila kumpenda Mungu,” alisema Dk. Bilal.
Akihubiri katika misa hiyo, Askofu Kinyaiya mbali na kuhimiza amani, pia alihimiza suala la uboreshaji na utunzaji mazingira.
“Mungu aliumba dunia akatupa tuitunze, suala la uboreshaji wa mazingira bado lipo nyuma ikiwamo kukithiri kwa uchafu katika miji.
“Suala la biashara ya meno ya tembo bado ni tatizo, lazima tutambue tukiua tembo leo hawarudi, nchi nyingine zilishawaua tembo wote, leo hii wanakuja kwetu kuwaangalia,” alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Tarcisius Ngalelakumtwa, mbali na kumpongeza Askofu Kinyaiya, alimtaka kutumia vipaji vyake kutatua changamoto za kiimani na za kijamii katika jimbo lake.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles