23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Tunashtushwa maadili ya walimu kuporomoka

TUMEKUWA tukiandika mara nyingi na kuzishauri mamalaka zinazohusika na walimu kuchukua hatua kutokana na kuwapo kiwango kikubwa cha kuporomoka kwa maadili.

Siku hizi imekuwa kawaida kusikia mwalimu wa shule ya msingi au sekondari kakamatwa na vyombo vya dola kwa kosa la kubaka, kumpa mimba mwanafunzi au kulawiti wanafunzi wa kiume.

Huu ni ukatili hatari kwa watu ambao wamepikwa na kupewa misingi yote ya sheria,taratibu na kanuni za kusimamia wanafunzi.

Leo tumelazimika kusema haya tena, baada ya Serikali kutangaza rasmi kuwafukuza kazi walimu 4,046 wa shule za msingi na sekondari  kutokana na makosa mengi, yakiwamo ya uhusiano wa mapenzi na wanafunzi, utoro kazini na kukiuka maadili.

Katibu Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindurwa tangu TSC ianze kufanya kazi Julai, 2016 walimu 7,123 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu, baada ya kukiuka maadili ya kiutumishi.

Idadi hii ya walimu ni kubwa mno kulinganisha na ukweli wa hali iliyopoa sasa ambapo kila kukicha Serikali imekuwa ikihaha kuongeza walimu

Katika kipindi hiki cha miaka mitatu, makosa 5,447 yalikuwa ya utoro kazini, makosa 1,290 kukiuka maadili, makosa 162 uhusiano wa mapenzi na wanafunzi na makosa mengine kwa ujumla wake yalikuwa 224. Takwimu hizi zinaonyesha wazi kumekuwapo na kasi kubwa ya kuporomoka kwa maadili ya walimu na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa.

Pamoja na tume hii kuchukua hatua mbalimbali za kiutumishi kwa mujibu wa Sheria Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu,walimu  4,046 wamefukuzwa kazi, 930 wamepewa onyo/karipio,284 walipunguziwa mshahara, 244  walisimamishiwa nyongeza ya mshahara, 237 walishushwa cheo na 14 walipewa adhabu ya kufidia hasara. Hili si jambo la kufumbia macho hata kidogo

Ni ukweli usiopingika kwa tume hii bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha walimu wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu za kiutumishi ili wajiepushe na makosa ya kinidhamu.

Hatuamini kama Serikali inajivunia kuwafukuza kazi walimu wake iliyowaajiri yenyewe, ikizingatiwa bado kuna changamoto ya upungufu wa walimu maeneo mbalimbali, lakini kwa hali ilipofika inapaswa kufanya hivyo.

Inasikitisha mno kuona walimu ambao ni watu wazima wameshindwa kuelewa nini ambacho wanakifanya, umefika wakati watumishi wa umma kama hawa wanapaswa kuelewa majukumu hasa nyakati hizi ambazo Serikali inaoneka iko macho mchana na usiku.

Tunaamini sasa kila mtumishi wa umma anapaswa kusoma alama za nyakati ili kuhakikisha anatimiza majukumu yake kama ambavyo mwajiri wake anataka na si vingine.

Alieleza baadhi ya kero hizo kuwa ni kucheleweshwa kwa malipo ya kusafirisha mizigo kwa walimu waliostaafu, walimu waliostahili kupandishwa madaraja kutopandishwa kwa wakati, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kukataa kupitisha barua za walimu wanaoomba kuhama kutoka Wilaya moja kwenda nyingine na walimu kutotendewa haki katika mashauri ya nidhamu.

Sisi MTANZANIA, tunatoa msisitizo kwa tume kuwashughulikia vizuri na kuwasimamia walimu waliobaki kuepukana na  matatizo hayo hasa kubwa  hili la walimu kujihusisha na mapenzi na wanafunzi.

Tunasema hivyo kwa sababu walimu wana miongozo yao ambayo inawazuia kufanya vitendo hivi ambavyo vinadhalilisha Serikali na taaluma yao wenyewe.

Jambo la mwisho, tume iweke utaratibu wa wa wakuu wa shule na walimu wakuu kuwa na utaratibu wa vikao kwa walimu wa ngazi zote kwenye shule ili kuwakumbusha wajibu wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles