30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAKAMATA WANYWA POMBE SAA KAZI, VIPI WANYWA VIROBA?

kiroba

JUZI nilipita katika mtaa mmoja Kariakoo, jijini Dar es Salaam, nikawaona vijana kadhaa wakiwa wamekaa kikundi wakipiga stori.

Sijui kwanini nilivutika kuwasogelea, nikajikuta napiga hatua hadi walipo. Walikuwa nje ya duka moja la mtu waliyekuwa wakimuita Mangi.

Vijana hao ambao walikuwa na kati ya umri wa miaka 20 – 32 walikuwa wanakunywa pombe kali zinazohifadhiwa kwenye mifuko ya nailoni maarufu kama viroba.

Wapo hoi, mbaya zaidi mchana kweupe. Kunywa viroba mchana? Jambo hilo lilinisononesha sana. Mchana wa saa nane, badala ya kuwa kwenye chakula, wao wanakunywa viroba!

Wengine walionekana kuwa na biashara zao mikononi. Nikawasabahi, wakaitikia wachache waliotaka. Nikamchagua mmoja na kumvuta pembeni.

Nikaanzisha mazungumzo naye. Kwa sauti ya urafiki, nikataka kujua kwanini walikuwa wakinywa pombe mchana ule, tena pombe ambayo ilianza kuwababua midomo yao na kuharibu nyuso zao zilizoonekana dhahiri kuwa zamani zilivutia sana.

Akanijibu: “Maisha. Maisha braza. Sijasoma, sina kitu. Mimi nabangaiza tu huku mitaani. Mawazo mengi, nikaamua niwe nayapunguza kwa kupiga hii kitu.”

Wakati anamalizia sentesi yake, tayari alishaelekeza kiroba chake tena kinywani mwake. Hakuwa na muda tena na mimi, huyooo akaondoka zake kurudi kwa rafiki zake.

Nikabaki na huzuni zangu, nikaamua kuondoka. Ndugu zangu, naeleza haya kwa dhati ili watu waelewe namna vijana wa taifa hili wanavyoharika.

Ni vizuri tuwape somo hawa vijana. Kama Serikali imeamua kuzuia unywaji wa pombe kwa saa kazi, mbona viroba vinanyweka usiku na mchana?

Siyo Kariakoo pekee, kwenye vituo vya daladala, sokoni nk, viroba vinyweka sana. Vijana nyuso zimewapauka, sura zimevimba. Muda wote wanalewa tu.

Ni kweli haya maduka hayajulikani? Moja lipo Kariakoo, linaangalia na kituo cha Mwendokasi, Msimbazi ya kwanza. Hata ukienda asubuhi saa nne, utakuta watu wanavyogombani viroba pale.

Baa hazifunguliwi mchana, bia haziuzwi na ukikutwa unakunywa bia mchana, wewe na aliyekuuzia mnakamatwa. Sasa vipi kwa wauza na wanywa viroba? Mbona tunawapotezea? Tunajenga taifa la namna gani?

JOSEPH SHALUWA

MHARIRI – JUMA3TATA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles