TUNA IMANI NA TAIFA STARS

0
518

KIKOSI cha timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ mwishoni mwa wiki kilitupa karata yake ya kwanza kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019, nchini Cameroon.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi,  ilishuhudiwa Stars ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho katika mchezo wa kundi L ambalo pia lina timu za Uganda na Cape Verde.

Matokeo hayo yameanza kupoteza matumaini ya Watanzania kuiona timu yao ya taifa ikianza kutoka sare nyumbani kabla ya kwenda ugenini.

Takribani miaka 37 imeweza kupita tangu timu ya taifa ya Tanzania ilipofuzu kushiriki fainali zilizofanyika 1980 nchini Nigeria.

MTANZANIA tunaamini kwamba kushindwa kupata ushindi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Lesotho, kunaweza kuwa funzo kwa timu yetu kuweza kurekebisha makosa yake.

 Matarajio ya wengi yalikuwa ni kuiona  Taifa Stars ikiibuka na ushindi mnono katika mchezo huo, ili kujiwekea nafasi nzuri ya kufuzu na kushinda mechi zijazo.

Matokeo hayo yameonyesha jinsi gani hakukuwa na sababu ya Stars kwenda kuweka kambi ya maandalizi nchini Misri ambako iliweka kambi siku takribani nane.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeonyesha juhudi za kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanikisha ndoto za kukata tiketi ya kucheza fainali hizo, ila ukweli bado tuna kibarua kizito kuhakikisha tunafanikisha mipango tuliyojiwekea.

Stars inakabiliwa na kibarua kizito zaidi katika mechi zake mbili za nyumbani dhidi ya Uganda na Cape Verde, ambapo uhalisia mataifa hayo ya wenzetu yamepiga hatua zaidi kisoka.

Taifa Stars inaweza kupenya kutoka kwenye kundi hilo endapo TFF itaweka mkazo wa kuitafutia mechi nyingi za kirafiki timu hiyo.

TFF inatakiwa kuendelea na mikakati yake ya kuiweka kambini timu hiyo na kuhakikisha inapata mechi za kujipima kwanza kabla ya kushiriki mechi za kufuzu.

Tunaamini kikosi hicho kinaweza kurudisha matumaini ya Watanzania, kushuhudia timu yao ya taifa kwenye michuano mikubwa ya soka Afrika, baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka mingi.

Hivi sasa kumbukumbu pekee inayoendelea kukumbwa na Watanzania ni timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, iliyoshiriki mashindano ya Afcon kwa vijana.

Kama ilivyokuwa kwa Serengeti Boys ambayo iliweka kambi ya mwezi mmoja nchini Morocco kujiandaa na fainali za vijana, pia Stars ni vema ikaandaliwa  kwa muda mrefu.

Stars ilikuwa katika nafasi nzuri ya  kupata pointi tisa nyumbani  kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwenye kundi lake, lakini mipango yao imetibuka kutokana na sare waliyolazimishwa na Lesotho.

Matumaini ya Watanzania wengi ni kuona nchi yetu inasonga mbele kwenye michuano hiyo, lakini TFF ihakikishe  kuweka mikakati mizito itakayoweza kushinda michezo yote itakayofuata.

Bado tumebaki na matumaini kuwa Tanzania itafuzu kucheza fainali za Cameroon.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here