25.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

TUMEPANGA KUCHAGUA NJAA MWALIMU MAISHA ANATUNYOOSHA

mtz26-2

NA INNOCENT NGANYAGWA,

METHALI hutufundisha mambo mengi ya busara, methali ni mtoto wa mwalimu maisha ambaye ni mkali kuliko mwalimu wa shuleni.

Tofauti ya mwalimu huyu na wa shule ni kwamba, shuleni unapewa somo na zoezi la kufanya, ukishindwa au kuzembea ndipo mwalimu hukuadhibu. Lakini mwalimu maisha yuko tofauti ukikosea anakuadhibu kwanza kisha anakufundisha na utajifunza kutokana na adhabu aliyokupa si vinginevyo.

Majuma mawili yaliyopita niliandika katika safu hii kuhusu makosa ya hesabu tunayofanya katika kuendesha siasa nchini kwa usimamizi wa sera ambazo hunadiwa katika ilani za vyama wakati wa kuomba ridhaa ya uongozi kwenye uchaguzi.

 Kuna fundisho jipya kutoka kwa mwalimu maisha anayeifundisha nchi yetu ambalo tunarudiwa kuadhibiwa kila mara kutokana na kushindwa kuzingatia somo, ndiyo maana kila mara tunatumikia adhabu na ikishapita tunajisahau na hatukumbuki katika makosa yaleyale.

Tujikite kwenye methali katika mfumo rasmi wa lugha, lakini pia katika mfumo usio rasmi, tukianza kwenye mfumo rasmi methali hizi mbili zina maana kubwa kwa muktadha wa tafakuri ya leo:

“Kupanga ni kuchagua” lakini pia “Kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa” katika muktadha usio rasmi wa lugha tohozi ambayo wengi huiita ya mtaani lakini kwa jina lake halisi huitwa ‘misimu’ ikiwa mtu anatajwa kuwa na njaa na jambo fulani maana yake ni kuwa ana usongo, yaani dhamira iliyopitiliza kufanikisha azma yake.

Mathalani, kwenye kandanda tunaweza kusema: “Mshambuliaji fulani ana ‘njaa’ ya kufunga goli” ni sawa na tukisema kuwa Rais wetu wa sasa JPM ana ‘njaa’ ya kutufanya tuwajibike kwa kutenda kazi ili tubadilishe maisha yetu yageuke neema badala ya shida na mahangaiko ya kila siku.

 Sasa tujikite katika tafakuri kamili tukianza na methali rasmi, tumepanga kugubikwa na shida ya njaa isiyokauka inayojirudia kila baada ya miaka kadhaa. Kwa sasa imebadilisha hesabu kwa kuwa awali kihistoria miaka takribani yote iliyoishia na tarakimu nne tulikabiliwa na njaa na hiyo ni tangu kabla hatujapata uhuru.

Wengi mtakumbuka vyema njaa ya mwaka 1974 ambapo tulihimizwa kujikita katika kilimo cha kufa au kupona, mahindi na mtama vililimwa hadi katika mizunguko ya barabarani (keep-left) na kwa kuwa wakati huo wananchi hawakuwa na ubishi na matamko ya viongozi, wito uliitikiwa vyema na tukaiondosha njaa hiyo kwa urahisi.

Kwa sasa kuna mabishano yanayoendelea kuhusu hali ya chakula nchini huku wenye mamlaka wakidai kuwa hali ni shwari, lakini vyombo vya habari vikiangaza maeneo ambayo tayari watu wake wanashindia ‘vinogesho’ ambavyo kwa kawaida si vyakula kamili bali viburudisho tu kutokana na ukosefu wa nafaka.

 Hali ya hewa inajulikana, mipango ya kuachana na kilimo cha kutegemea mvua kama ‘mana’ inayodondoka kutoka mbinguni imeimbwa miaka mingi lakini imekwama na haina utekelezaji kamili, kwa kushindwa kutumia vyanzo vya maji yanayotuzunguka pande zote za mipaka ya nchi.

Nakumbuka kuna wakati tulitaka hata kununua mvua nchini Thailand japo ilikuwa kwa ajili ya kujaza mabwawa ya umeme lakini ikagundulika kuwa ni mvua ya kulimia bustani.

Kimsingi tumepanga kuchagua njaa na mwalimu maisha anatuadhibu kila tunapokosea na fundisho likishapita tunabweteka na kurudia uzembe ule ule na wimbo njaa usiochuja ubora wake kwa Watanzania, unaendelea kukamata chati ya juu kwenye maisha yetu.

Tukijinasibisha na methali ya pili kwamba tunashindwa kupanga na hivyo tunapanga kushindwa kama ambavyo inatutokea mara zote, walau wakati wa Mwalimu Julius Nyerere kulikuwa na kuthamini kuwa na hodhi ya chakula katika hifadhi na kilimo kilichofanywa na mashirika mahususi ya umma (NAFCO na NMC). Licha ya yote yanayotukabili kwa sasa kwa njaa iliyoanza kurindima na njaa ijayo bado hatujajifunza.

 Nikisema njaa ijayo ni kutokana na hali mbaya ya hewa na hiyo ikimaanisha kuwa tusipokaa sawa hata mwaka ujao utatubadilishia zaidi tarakimu za miaka yenye historia ya baa la njaa hapa nchini.

Tukijikita katika methali ya lugha ya ‘misimu’ inavyoelekea hatuna ‘njaa’ ya kukabiliana na njaa bali tuna ‘njaa’ ya kutumia janga la njaa kama mtaji wa kisiasa, kulumbana na kurushiana maneno lakini pia kuambiana ukweli mchungu ambao ukishapita hautageuka kuwa ukweli mtamu kwa kuwa njaa haikabiliwi kwa hotuba za jukwaani bali mikakati inayoweza kugawanywa katika vipindi tofauti ikiwemo ‘mpito’ kwamba tunafanyaje kubadili hali ya sasa, pili ‘mwendelezo’ tunafanyaje ili hali hii isijirudie tena na tatu ni ‘kudumu’ yaani kuzuia isijirudie tena siku zijazo na kuzua hamkani inayotufundisha kwa kutuadhibu kila mara kutoka kwa mwalimu maisha. Huu si wakati wa kulumbana, tushikamane kuikabili njaa inayotukabili!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles