TUME YA UCHAGUZI KENYA YATAKIWA ISAFISHE DAFTARI LA WAPIGAKURA

0
511

NAIROBI, KENYA

VIONGOZI wa kidini chini ya mwamvuli wa Kongamano la Makanisa ya Ufungamano (U-JFRO) wameitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhakikisha daftari la wapigakura limesafishwa ili kuondoa wasiwasi unaoendelea kuhusu uwazi wa uchaguzi ujao.

Wakiwahutubia wanahabari baada ya kuwasilisha mapendekezo yao bungeni, viongozi hao walieleza kuhuzunishwa na habari kuwa bado kuna wapigakura wafu katika daftari hilo.

“Tunaitaka IEBC isiache nafasi yoyote yenye kutiliwa shaka kuhusu maandalizi yake ya uchaguzi. Uchaguzi sharti uwe wa wazi na haki na tunawataka wagombea na wafuasi wao wakubali matokeo bila kuzua vurugu,” alisema Dk. Willy Mutiso ambaye alisoma taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na zaidi ya maaskofu 10.

Viongozi hao waliwataka Wakenya wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowafaa.

“Tunawashauri Wakenya wote waliojisajili kusitisha shughuli zao Agosti 8 na kujitokeza kupiga kura ili kuhakikisha wamewaajiri viongozi wanaowataka,” aliongeza Dk. Mutiso.

Aidha waliwashauri wapigakura wasiuze kura zao kwani hatua hiyo itaathiri kwa kiasi kikubwa mustakabali wao.

“Wakenya wasikubali kuhongwa au kupiga kura kwa misingi ya kikabila kwa sababu watajilaumu wenyewe kipindi cha miaka mitano baada ya uchaguzi kukamilika,” ilisema taarifa ya viongozi hao.

Walivitaka vyombo vya habari kusaidia kueneza amani na kupuuza taarifa za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here