30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

TUME YA FARU JOHN YAJA NA MAZITO

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM


TUME iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuchunguza kifo cha Faru John, imeibua mambo mengi mazito yanayoendelea katika uhifadhi wa wanyamapori nchini.

Ripoti ya uchunguzi huo uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele, ilikabidhiwa Dar es Salaam kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Faru huyo alihamishwa kutoka katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na kwenda kambi binafsi ya Grumeti iliyoko Serengeti ambako ndiko alikofia.

Akizungumza jana wakati wa kukabidhi ripoti hiyo, Profesa Manyele alisema sampuli na vielelezo vyote vimethibitisha kuwa ni kweli Faru John alikufa Sasakwa Grumeti.

“Sababu za kifo chake ni kukosa matunzo, uangalizi wa karibu, kukosa matibabu na matatizo ya kiuongozi kwa wizara, hifadhi na taasisi zake.

“Kwa lugha nyepesi walimtelekeza yule faru, baada ya kuhamishwa hakukuwa na mpango mkakati wa kufuatilia maendeleo yake,” alisema Profesa Manyele.

Tume hiyo imeshauri hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Dk. Kileo wa Shirika la HIfadhi za Taifa (Tanapa) na wajumbe wa kamati za uongozi na ufundi, akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori kutokana na kushindwa kufuatilia afya ya Faru John.

Awali Dk. Kileo, alikuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, lakini alihamishiwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kazi maalumu ya kumhamisha Faru John, na baada ya kazi hiyo alihamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Profesa Manyele, alisema pia hapakuwapo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kumuhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti.

Pia hapakuwapo kwa mkataba rasmi kati ya Serikali na mwekezaji, unaoonyesha mnyama huyo ametoka serikalini kwenda kwa mwekezaji.

Kutokana na mapungufu hayo, tume hiyo imependekeza hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori na Mhifadhi wa NCAA.

Tume hiyo pia imeshauri Serikali kuunda tume huru kuchunguza migogoro ya kimasilahi kati ya watumishi wa NCAA na wawekezaji ndani ya hifadhi na hatua stahiki zichukuliwe.

Katika uchunguzi huo, tume hiyo imebaini kuwapo kwa migongano ya kimasilahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia masilahi binafsi.

Kwamba kulikuwa na migongano kati ya Patrice Matayi na uongozi wa NCAA.

“Masilahi binafsi yalitawala na kusababisha kuhamishwa kwa baadhi ya watumishi na mengine yalifika ngazi ya wizara, lakini wizara iliingilia kati na kupendelea upande wenye masilahi binafsi.

“Hali hii ilisababisha kutoelewana kwa makundi mawili hadi kufikia hatua ya kushtakiana kwa kutumia kauli ya ‘kuuzwa kwa Faru John’… majungu mengine yalifika kwa Waziri Mkuu,” alisema.

Pia imeishauri Serikali kufanya tathmini ya kina kuona kama uongozi uliopo NCAA kwa sasa unajitosheleza kuendelea kuongoza taasisi hiyo.

Tume hiyo pia imeshauri ujenzi wa Hoteli ya Ndutu uchunguzwe upya kwa sababu inajengwa katika maeneo ambayo ni mapitio ya wanyama (shoroba).

Pia imeshauri kuunganishwa kwa taasisi za TANAPA, NCAA, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na Mkurugenzi wa Wanyamapori (DW) ili kuondoa uwapo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wanyamapori.

Kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za wanyamapori, tume imeshauri kuwe na udhibiti wa watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu za vinasaba vya wanyamapori wa Tanzania dhidi ya mataifa mengine.

“Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe Kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori ili Serikali iweze kupata ushahidi wa kimahakama katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori,” alisema Profesa Manyele.

Tume hiyo imeshauri Mkurugenzi wa Wanyamapori apunguziwe madaraka kutokana na kuwa na maamuzi makubwa kisheria kuhusu masuala ya wanyamapori.

Katika uchunguzi huo, tume hiyo imeshauri viwanja vya ndege vilivyopo ndani ya hifadhi vifanyiwe tathmini ya kina juu ya manufaa ya uwepo wake, kwani vinaweza kuchangia majangili na matajiri kufanikisha ujangili.

“Tume inashauri kuanzishwa kwa ‘database’ ya wanyamapori, ambayo itasaidia kutambua nyara na kuviwezesha vyombo vya uchunguzi katika kufanya upelelezi.

“Kifo cha Faru John kitumike kama fundisho kwa Serikali, wizara na Watanzania kwani yaliyokuwa yanaendelea kwenye hifadhi yalikuwa na mapungufu makubwa,” alisema Profesa Manyele.

 

WAZIRI MKUU

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Waziri Mkuu, Majaliwa alisema ataipitia kwa kina na baada ya hapo atatoa uamuzi wa Serikali.

“Nitaipitia kwa kina ripoti hii nielewe vizuri ushauri na mapendekezo yaliyotolewa, halafu Serikali itatoa maamuzi ya nini kifanyike.

“Tutachukua hatua katika maeneo ambayo tunaona ni muhimu,” alisema Majaliwa.

Alisema wametumia nguvu nyingi katika jambo hilo kwa sababu ni mkakati wa Serikali kuona sekta ya utalii inaimarika, kwa kuwa ni kati ya sekta zinazoingiza fedha nyingi kupitia kwa watalii wanaokuja nchini.

“Miongoni mwa wanyama wanaotoweka kwa kasi nchini ni tembo na faru, lakini tuliweka mkakati wa kuwahifadhi faru hadi tuliwawekea ‘transmitter’, lakini unashangaa anahamishwa kwa utaratibu usiokuwa rasmi kisha anatoweka,” alisema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles