24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Tumbili wamsimamisha kazi kigogo

Profesa-Jumanne-MaghembeVeronica Romwald, Dar na Safina Sarwatt, Kilimanjaro

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori na Matumizi Endelevu, Charles Mulokozi ili kupisha uchunguzi baada ya kubainika kutoa kibali cha kusafirisha tumbili 61 nje ya nchi kinyume cha utaratibu.

Mbali na huyo, Profesa Magembe pia  amewasimamisha kazi watumishi wengine 11 ili kupisha uchunguzi dhidi yao.

Watumishi waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Juma Mgooo, Mkurugenzi wa Rasilimali Misitu, Zawadi Mbwambo na Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Nurdin Chamuya.

Wengine ni Haji Khatib aliyekuwa Kanda ya Ziwa, Halbert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki), Shaban Mwinyijuma (Kati), Casbert Mafupa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi) na Brunal Malya (Nyanda za Juu Kusini).

Akitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana, Profesa Maghembe alisema amechukua hatua hiyo baada ya kubaini mchezo mchafu unaochezwa na baadhi ya maofisa wa Idara ya Wanyamapori, akiwamo Mulokozi ambapo alibariki kusafirisha nje ya nchi kinyume cha sheria nyani 450.

“Nilipata taarifa tangu awali watu hao walipoanza kukimbiza tumbili huko porini, walikuwa wanataka kukamata nyani 450 jambo la kushangaza ninyi maofisa hamjui chochote.

“Walianza kwa kukamata tumbili 21 nikasema mtajua kumbe hamkujua, nashangaa kwanini msijue, na siku iliyofuata tena wakakamata nyani wengine 40 wakafika jumla ya 61, bado hamkujua, na siku iliyofuata wakakimbiza wengine huko Upareni, Manyara na Kilimanjaro wakafika nyani 141, ilipofika hapo nikashtuka.

“Nikamtafuta ofisa wetu wa Arusha, nikamwambia marufuku kutoa kibali cha kusafirisha wanyama wa aina yoyote kwa muda wa siku nane kuanzia jana, kisha nikaenda Moshi nikamuita Dk. Mlokozi na kuzungumza naye ndani ya ofisi ya mkuu wa mkoa huo,” alisema.

Profesa Maghembe alisema alimweleza Dk. Mlokozi juu ya suala hilo, lakini hata hivyo alimwambia  hakuna taarifa za kukamatwa nyani hao.

Alisema pamoja na hayo, alimtaka Dk. Mlokozi kutotoa kibali chochote cha kusafirisha wanyama ili watu hao wanaokusanya nyani bila ya kuwa na kibali wakamatwe.

“Baadaye Dk. Mlokozi alirudi Dar es Salaam na jana (juzi), nikaambiwa wale watu wamekusanya nyani 450 waliokuwa wanawataka, wanatafuta kibali cha kusafirisha nyani 470,” alisema.

Alisema kwa kuwa alikuwa ameshawasiliana na ofisa wa wanyamapori aliyeko Arusha na kumtaka asitoe kibali chochote, ilimlazimu ofisa huyo kuondoka kabisa ofisini kwake.

“Watu hao walikwenda na kumtafuta kwa nguvu zote ili awape kibali hawakumpata, ila hiyo jana (juzi) nikaambiwa wamepata kibali kutoka  hapa makao makuu cha kusafirisha nyani 61, walikamatwa wakiwapeleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kibali walichokuwa nacho kimetolewa na Dk. Mlokozi, yule yule ambaye nilimwambia asitoe,” alisema.

Huku akizungumza kwa hasira na kupiga piga meza yake, Profesa Maghembe alisema: “Ninyi wote mnajua ili mtu aweze kukamata wanyama porini, kwanza lazima aombe na apate ruhusa kisha alipie ndipo apewe kibali husika na ashirikiane na kampuni za Tanzania, taarifa niliyonayo hawakufanya hivyo,” alisema.

Alisema wizara imemshikilia rubani na ndege iliyoingia nchini kwa ajili ya kusafirisha nyani hao na wahusika wote wa ndani na nje.

“Hainiingii akilini, natoa maagizo mtu asifanye halafu anafanya. Yaani namwambia anageuka huko na kufanya yale niliyomkataza… watu wamezoea kusema haya ni mambo ya siasa, nataka mjue ‘this is not politics’ bali ni kwa ajili ya kulinda masilahi ya nchi hii.

“Inaelekea hii biashara ya kuuza wanyama nje ya nchi ni biashara inayofanywa kila siku, naomba Katibu Mkuu (Meja Jenerali Gaudence Milanzi) utusaidie kuchunguza tangu wale twiga waibiwe na kupelekwa nje ya nchi, ni mara ngapi wanyama wametolewa na kupelekwa nje bila kibali,” alisema.

Alimtaka Milanzi kuangalia vibali vyote ambavyo vimetolewa na Idara ya Wanyamapori na kuvikagua ili  ajiridhishe ni vingapi na wanyama wangapi walitolewa.

“Na huu utaratibu wa kutoa vibali vya wanyama kumi halafu wanasafirishwa 20, nataka uuangalie na kujiridhisha pale KIA na maeneo mengine tujue hawa watu wametuibia kiasi gani na nani anasaini vibali hivi…. haiwezekani watu wanakamata wanyama bila ruhusa, yaani mtu anatoka Ulaya anakuja hili ‘shamba la bibi’ anakamata wanyama anaweka kwenye kreti anapeleka kwao kama zawadi ya ‘Easter’, nataka kujua ni akina nani ambao wanajihusisha na biashara hii.

“Nayasema haya yote kwa masikitiko makubwa, ndugu zangu hebu tushirikiane tulinde mali ya mama yetu Tanzania, hata magogo tuliyonayo kama tumeamua kuuza tuuze kwa utaratibu uliopo, kule Kalambo wamekata hakuna hata senti moja iliyolipwa, yanalazwa porini mtu anakuja na kontena anaweka anafunga anapeleka China kama mali ya shangazi.

“Wana kibali kinaonyesha yametoka nchini Zambia… jambo hili nataka lisimame mara moja na hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki kuiba mali za nchi hii au anakaa na kuangalia kando wakati fedha na mali ya nchi zinachukuliwa na kuporwa,” alisema.

Januari 5, mwaka huu katika kikao chake na watumishi wa wizara hiyo, Profesa Maghembe alisema kuna wafanyakazi ambao si waaminifu wamekuwa wakikusanya fedha za Serikali, lakini hawazipeleki benki kama inavyotakiwa.

 

KILIMANJARO

Habari kutoka mkoani Kilimanjaro, zinasema nyani hao walikamatwa  wakati wakipakizwa kwenye gari lenye namba za usajili T 560 CRY aina  ya Toyota Isuzu mali ya mfanyabiashara  Franael Mafie, mkazi wa Bomang’ombe wilayani Hai, juzi saa 1:30 usiku katika Uwanja wa KIA .

Taarifa zinasema wanyama hao walitolewa eneo la King’ori mkoani  Arusha kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchini Albania.

Naye Ofisa Maliasili Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Kiyengi, alisema raia hao walipewa vibali na maofisa wa wizara hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alikiri  kukamatwa kwa raia hao na kwamba wanaendelea kuhojiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles