Brighiter Masaki -Dar es Salaam
CHUO Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (TUDARCo) kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kimeanzisha udahili wa wanafunzi wa masomo ya Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara na Shahada ya Uzamili ya Taaluma ya Habari ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa haba jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza udahili huo, Naibu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Andrew Mollel, alisema wameanzisha mafunzo hayo kwa kuwasaidia walioajiriwa na waliojiajiri ambao hawana muda wa kutosha kusoma asubuhi mpaka mchana, hivyo wataweza kusoma jioni.
Alisema wanajivunia mafanikio yao ya kutoa elimu bora inayowaandaa wanafunzi kujiajiri na kuachana na kutegemea kuajiriwa.
“Tumepewa hadhi ya kutoa shahada ya uzamili ya Taaluma ya Habari na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambapo kutokana na masomo hayo tunakusudia kuwajengea umahiri wahitimu katika uendeshaji wa habari za kidigitalii, miradi ya habari, utunzaji wa habari, mifumo ya huduma za habari.
“Pia, uandaaji wa mifumo ya habari na uendeshaji wake, uchambuzi wa habari na mitandao ya kijamii na kwa upande wa shahada ya uzamili ya Uongozi wa biashara kozi itakuwa na michepuo ya ujasiliamali na masoko, usimamizi wa rasilimali watu, fedha na shughuli za kibenki,” alisema.
Alisema mwombaji wa kozi hizo anatakiwa kuwa na Shahada ya Awali (Bachelor Degree) yenye ufaulu wa wastani wa GPA ya 2.7 kutoka chuo chochote kinachotambulika na Serikali, awe na Stashada ya Uzamili (Postgraduate Diploma) yenye ufaulu wa wastani wa GPA ya 4.0.
“Mwombaji mwenye shahada isiyo bainifu (unclassified degree) kama vile Shahada ya sayansi ya tiba (M.D) anapaswa awe na angalau ufaulu wa daraja B katika somo alilomakinikia (Subject of Specialization).
“Aidha, mwombaji mwenye shahada ambayo ubainifu wake hautambuliki kwa urahisi na chuo itapaswa kupeleka vyeti au sifa zake katika TCU, ili kupata utambuzi kabla hajafikiriwa kutahiniwa. Tunawakaribisha wote kutuma maombi ambapo mwisho wa kupokea ni Februari 28, 2020 na masomo yataanza Machi 16, 2020,” alisema Prof. Mollel.
Naye, Mkuu wa Idara ya Habari na Ukutubi wa chuo hicho, Dk. Getrude Ntulo, alisema anawakaribisha watu wote wenye vigezo ili kujipatia taaluma itakayomsaidia katika shughuli za kihabari.
“Mwandishi anaweza kuwa na habari lakini akashindwa kuifikisha kwa jamii kwa kufuata kanuni na maadili ya Taaluma. Hivyo tutawafundisha vizuri namna ambavyo habari zinatakiwa kufikishwa kwa jamii. Chuo kipo Mwenge Barabara ya Cocacola,” alisema Dk. Ntulo