23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

TUKITAKA UCHUMI WA VIWANDA TUANZE NA KILIMO

Na ESTHER LEMA (OUT)


UCHUMI wa viwanda ni moja kati ya sera zinazopiganiwa na Serikali ambapo hata Rais John Magufuli aliwahi kuahidi katika kampeni zake kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Ni wazi kuwa, kupitia sekta ya viwanda uchumi wa nchi utaimarika na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ambao ndilo kundi kubwa zaidi kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Ili nchi ipige hatua kiuchumi, inapaswa kujiimarisha katika viwanda ili iweze kusafirisha bidhaa nje na kuepuka kuagiza bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa nchini.

Kwa kufanya hivyo, ni wazi kuwa itasaidia kuinua uchumi wa wawekezaji wazawa na kulisaidia taifa kupata fedha za kigeni sambamba na kutoa ajira kwa Watanzania wa kada tofauti.

Ili kufikia malengo ya kuwa nchi ya viwanda, Serikali haina budi kuhakikisha sekta zote rasmi na zisizo rasmi zinachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.

Kwa mtazamo wangu, naona sekta ya kilimo inapaswa kupewa kipaumbele zaidi kutokana na kuwa ndiyo sekta inayoajiri Watanzania wengi, huku ikitajwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Ikiwa Serikali inataka kweli kufikia uchumi wa viwanda, haina budi kuhakikisha sekta hii inachangia walau asilimia 40 ya pato lote la taifa na hilo litafikiwa ikiwa yatawekwa mazingira mazuri ya kuendesha shughuli za kilimo kwa kuhakikisha inakizika kilimo cha jembe la mkono na kuhamia katika kilimo kinachotumia nyenzo za kisasa, hasa trekta.

Hapa serikali inapaswa kuhamasisha jamii, hususan vijana, kuwa na vikundi vya kilimo vitakavyowezeshwa kwa kupewa ruzuku ya mtaji na vifaa vya kufanyia kilimo cha kisasa kisichotegemea mvua za misimu.

Kadhalika Serikali haina budi kuhakikisha inaanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao yanayozalishwa kwa lengo la kuyaongezea thamani kabla ya kuingizwa sokoni.

Uanzishwaji wa viwanda hivyo pia utategemea upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo ambayo shughuli za kilimo zinafanyika kuwezesha viwanda kuzalisha kwa kiwango cha juu na kwa ufanisi.

Miundombinu ni moja ya mambo yanayopaswa kupewa uzito wa hali ya juu ili kurahisisha maeneo ya mashamba kufikika  kirahisi na kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa huko.

Ni wazi kuwa, ikiwa hakuna miundombinu, hasa ya barabara inayoruhusu maeneo ya uzalishaji kufikiwa kwa urahisi, bado hakutakuwa na mafanikio katika sekta hiyo, kwani pamoja na uzalishaji kuwa mkubwa, hakuna atakayekuwa na uwezo wa kwenda kununua mazao katika maeneo hayo.

Pamoja na hayo, Serikali inatakiwa kuhakikisha yanapatikana masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi ili kuwezesha kuuzwa kwa urahisi kwa mazao hayo, kwani hakutakuwa na maana yoyote ikiwa mazao yatakayozalishwa yatakosa soko na kuharibikia kwenye maghala.

Upatikanaji wa masoko ni suala la lazima, kwani tumekuwa tukishuhudia mara kadhaa wananchi wakilalamika kukosa masoko ya kuuza mazao kama mahindi pale wanapojaaliwa kuzalisha kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha wakulima kutoona umuhimu wa kuzalisha mazao mengi wakati hakuna soko la uhakika.

Wakati haya yakifanyika, Serikali haina budi kuhakikisha inahamasisha utunzaji wa mazingira ili kuwezesha kuendelea kuwa na maeneo mengi yenye rutuba na yanayofaa kwa kilimo kwa kukabiliana na janga la ukame linaloinyemelea Afrika kwa kasi ya aina yake.

Hii itasaidia kulinda vyanzo vya maji vilivyopo ambavyo vitasaidia kuendesha kilimo cha umwagiliaji ambacho ndicho kinachostahili kufanyika zaidi kama nchi inataka kupiga hatua za kiuchumi kwa kutumia sekta hiyo.

Naamini Tanzania inaweza kufikia uchumi wa viwanda kwa kutumia sekta ya viwanda, kwani siamini kwamba kwa sasa nchi inao uwezo wa kuanzisha viwanda vya kutengeneza magari wa ndege.

Sina hakika kama Serikali imejipanga kuanzisha viwanda vya aina hiyo, kwa sababu uchumi wetu bado uko katika hatua za kutambaa, hivyo unahitaji kuongezewa nguvu ili uweze kutembea japo kwa kasi ya kawaida.

Naamini kwa kila mwenye mtazamo chanya kupitia kilimo anaweza kuyatambua haya kwa kulinganisha hali halisi iliyopo sasa na hali yetu ya uchumi bila kusahau malengo ya Serikali ya mwaka 2015-2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles