22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

TUKIO LA UJAMBAZI KARIAKOO KAMA SINEMA

Na AGATHA CHARLES,

MASHUHUDA wa tukio la kurushiana risasi baina ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na watu wanne wanaodaiwa kuwa majambazi waliouawa, wamesimulia mapambano yalivyokuwa.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku katika maduka yaliyopo Kariakoo, Mtaa wa Aggrey na Livingstone limeelezwa kudumu kwa takriban dakika 10.

Majambazi hayo manne yaliuawa yakijiandaa kufanya uvamizi katika maduka hayo na kusababisha watu wengine wanne kujeruhiwa.

Mashuhuda wa tukio hilo, walisema wakati majambazi hayo yaliyokuwa na silaha yakijiandaa kufanya uvamizi huo, ghafla walijitokeza polisi na kuanza majibizano ya risasi.

“Hao majambazi walikuwa wanne wakiwa na pikipiki mbili aina ya Boxer. Pikipiki moja ilikuwa na wawili na nyingine alikuwa amepanda mmoja na mwingine alikuja akiwa anatembea kwa mguu,” alisema shuhuda huyo.

Alisema baada ya majambazi hayo kukutana, yule aliyekuwa akitembea kwa miguu alielekea dukani na kabla hawajafanya lolote walisikia milio ya risasi.

Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ally Rajabu, alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea,  alikuwa akila mishikaki upande wa pili, ambako aliwaona vijana hao tangu walipofika eneo hilo.

“Wakati naendelea kuwafuatilia, mmoja aliingia dukani na hapo nikasikia mlio wa risasi, nikalala chini. Kuna watu walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali jana (juzi) hiyo hiyo usiku,” alisema Rajabu.

Alipotafutwa kwa simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro ili kuthibitisha tukio hilo, alisema kuwa yuko nje ya kituo chake cha kazi na kutaka atafutwe Naibu Kamishna wa Polisi na Mkuu wa Operesheni za Kipolisi wa kanda hiyo, Lucas Mkondya.

Hata hivyo, MTANZANIA Jumapili lilipofika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ili kuonana na Mkondya, hakuweza kupatikana kwa maelezo kuwa alitoka ofisini.

Jitihada zilifanyika ili kumpata ama msaidizi wake, lakini bado hazikuzaa matunda.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles