29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

TUKIO LA MWANAFUNZI KUUAWA: WAZAZI WATOA NENO ZITO

 

Na UPENDO MOSHA-ROMBO


KIFO cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam, aliyeuawa kwa kupigwa risasi juzi, Akwilina Akwilini, kimezua simanzi nyumbani kwao, Kijiji cha Marangu Kitowo, Kata ya Olele, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, huku wazazi wake wakitoa ujumbe mzito kwa Serikali.

Kutokana na hali hiyo wameitaka Serikali itoe maelezo ya kina kuhusu mauji ya ovyo ya raia wasiokuwa na hatia sambamba na kutaka uchunguzi huru na waliohusika na mauji ya mtoto wao wachukuliwe hatua za kisheria.

MTANZANIA ilifika nyumbani kwao marehemu jana na kutembelea maeneo mbalimbali ya kijiji hicho, alishuhudia watu walivyokuwa na simanzi na jinsi walivyokuwa wakizungumzia kifo hicho.

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake, mama mzazi wa marehemu, Constansia Akwilini, alisema familia yake imepokea tukio hilo kwa mshtuko wa aina yake.

“Huu ni msiba uliogusa moyo wangu sana na familia yetu kwa ujumla nashindwa nikuelezeeje.

“Kitendo hiki hakipaswi kufumbiwa macho, haya ni mauaji ya ovyo ya raia wasiokuwa na hatia na yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote ili kulinda amani na usalama wa nchi yetu.

“Kifo hiki kimeacha pengo kubwa katika familia yetu kwa sababu huyo ndiye mtoto pekee tuliyekuwa tukimtegemea katika familia yetu kwa siku zijazo kwa sababu ndiye aliyekuwa na mwelekeo wa kusoma,” alisema Constansia huku akitokwa na machozi.

Kwa mujibu wa mama huyo, Akwilini alifikia hatua hiyo kielimu kutokana na ufadhili wa shangazi yake na kwamba alikuwa ni mtoto wa sita kuzaliwa kati ya watoto wanane wa familia hiyo.

BABA MZAZI ATOA NENO

Akizungumzia historia ya marehemu baba mzazi wa marehemu, Akwilini Shirima, alisema Akwilina alizaliwa Aprili Mosi, mwaka 1996, katika Kijiji cha Marangu Kitowo, Kata ya Olele, wilayani Rombo.

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Kitongoria na kuhitimu mwaka 2009.

Baada ya hapo, Akwilina alijiunga na shule moja ya sekondari iliyoko mkoani Iringa ambako alihitimu mwaka 2014.

Baadaye, alichaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Embauwai, iliyoko Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, Akwilina hakumaliza kidato cha sita shuleni hapo kwani baada ya afya yake kudhoofika mara kwa mara kutokana na hali ya hewa ya Ngorongoro, alihamia mkoani Iringa ambako alihitimu kidato cha sita, mwaka 2016

Kuanzia Oktoba mwaka jana hadi alipofikwa na mauti, Februari 16, mwaka huu, alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), akisomea shahada ya kwanza ya ugavi na ununuzi.

TABIA YA MAREHEMU 

Akizungumzia tabia ya binti yake huyo, Akwilini alisema mtoto wake alikuwa ni mtu mwenye misimamo ya kimaisha na alipenda kuzungumza na kucheka na kila mtu.

“Watu wanasema mtu akishakufa ndiyo tunamzungumzia vizuri, lakini mwanangu alikuwa ni mcheshi, asiyependa kugombana na watu.

“Alipenda kazi na kusoma na pia alikuwa na misimamo ya kimaisha na niliamini kama angefanikiwa kuishi zaidi, angetusaidia kuondokana na umasikini kwa sababu ndiye mtoto pekee aliyesoma kati ya watoto wangu wanane,” alisema.

DADA WA MAREHEMU

Naye dada wa marehemu, Teddy Akwilini, alisema alizungumza na mdogo wake, Februari  12 na 15, mwaka huu ambapo walizungumzia masuala ya maisha na kuwaahidi kwenda Rombo kuwatembelea, Julai mwaka, huu baada ya kufunga chuo.

“Aliniambia anatamani sana kuja nyumbani na kasema Julai angekuja kutuona maana alikuwa amewakumbuka baba na mama.

“Nakumbuka aliniambia alikuwa akitafuta sehemu ya kufanyia masomo yake kwa vitendo, lakini inaniuma sana, kwamba amefariki bila kutuona na atakuja akiwa kwenye jeneza.

“Mimi ndiye mtoto wa kwanza katika familia yetu na kwa bahati mbaya mimi na wengine hakutubahatika kusoma zaidi ya darasa la saba kutokana na ufukara wa familia yetu.

“Kwa hiyo, kifo cha mdogo wangu ni pigo kubwa sana tena sana katika familia yetu kwa sababu kila mmoja alikuwa akimtegemea na tulikuwa tukimwombea kila siku kwani alikuwa na ndoto nyingi za kutubadilisha kamaisha,” alisema dada huyo huku akibubujikwa na machozi.

MAJIRANI WAZUNGUMZA

Mmoja wa majirani wa Akwilina, Dismas Shirima, alisema marehemu alikuwa ni mtu wa watu na alikuwa ni mtu wa kupenda kuwasaidia ndugu zake.

Kwa upande wake, jirani mwingine, Fausta Focus, alisema marehemu alikuwa ni mfano wa kuigwa kijijini hapo kutokana na tabia yake ya kupenda kujitolea katika shughuli mbalimbali za kijamii.

SERIKALI KUGHARIMIA MAZISHI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara yake itagharimia mazishi ya mwanafunzi huyo aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 16 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema yeye pamoja na katibu mkuu wa wizara yake, watasimamia shughuli zote za msiba huo.

“Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanafunzi huyu na alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kike waliojipambanua  kwa kujua umuhimu wa elimu, alihakikisha anasoma kwa bidii kwa manufaa yake na familia yake, lakini pia alikuwa miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

“Kifo chake kimeleta simanzi kwa wananchi wote na Serikali kwa ujumla alikuwa katika majukumu yake ya kawaida akipeleka barua yake ya mafunzo kwa vitendo Bagamoyo ndipo umauti ukamkuta,” alisema Profesa Ndalichako.

Kutokana na tukio hilo, Profesa Ndalichako alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni, alisema Serikali haiwezi kuyaacha matukio hayo yapite kama yalivyo, hivyo imeyachukulia kwa uzito unaostahili.

Masauni alisema uchunguzi wa tukio hilo utafanyika haraka iwekezanavyo, kwa weledi na utaalamu ili haki itendeke.

“Tutafanya uchunguzi na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo, Serikali tunasikitishwa na kifo cha mwanafunzi huyu, pia na kujeruhiwa raia,” alisema Masauni.

Alisema uchunguzi huo utakuwa mpana na utakuwa fundisho kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria.

ASKARI SITA WASHIKILIWA

Baada ya tukio hilo la kuuawa kwa mwanafunzi huyo Jeshi la Polisi limtangaza kuwashikilia askari wake sita ambao wanadaiwa kuhusika na tukio hilo la mauaji ya mwanafunzi huyo.

Mwanafunzi huyo, aliuawa juzi jioni kwa risasi wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokuwa wakielekea kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Jimbo la Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro  Mambosasa, alisema mbali na kuwashikilia askari hao, pia wamewakamata wafuasi 40 wa Chadema.

Pia, alisema wanaendelea kuwatafuta viongozi wa chama hicho, walioshiriki kushawishi maandamano hayo.

“Februari 16, mwaka huu, Chadema walikuwa na mkutano wa kufunga kampeni katika Viwanja vya Buibui, Mwananyamala ambapo Mwenyekiti wao Mbowe, alisikika akikatisha mkutano na kuhamasisha wafuasi wao kuingia Kinondoni ili kumshinikiza mkurugenzi awape barua za viapo vya mawakala wa chama hicho.

“Pia Mbowe alisikika akiwatukana viongozi wakuu wa nchi akiwa jukwaani, suala hili linaendelea na uchunguzi wake.

“Kadiri wanachama hao walipokuwa wakisogea mbele, idadi ya waandamanaji iliongezeka na walipofika Barabara ya Kawawa, maeneo ya Mkwajuni, walifunga barabara ya mabasi ya mwendo kasi na ya kawaida na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

“Polisi walifika katika eneo la tukio na kuzuia maandamano hayo, lakini ghafla wafuasi wa Chadema walianza kuwashambulia askari kwa mawe na chupa, fimbo na silaha zingine za jadi na kuwajeruhi askari wawili.

“Katika harakati za kujihami na mashambulizi  yaliyozidi, polisi walitumia silaha za kutuliza ghasia, lakini nazo zilionekana kushindwa kuwatawanya waandamaji hao, ndipo walipiga risasi za moto hewani na kufanikwa kuwakamata watuhumiwa 40 na kutawanya maandamano hayo.

“Siku hiyo hiyo, saa 1:30 usiku, polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilipata taarifa za kiintelijensia, kwamba katika purukushani hizo, kuna mwanamke mmoja alipoteza maisha na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

“Pamoja na kuendelea na uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi huyo, tumepata taarifa zingine, kwamba watu wawili walijeruhiwa maeneo ya miguuni na kitu chenye ncha kali ambao ni Erick John (24) na Innocent Mushi (23),” alisema Kamanda Mambosasa.

JPM AAGIZA UCHUNGUZI

Rais Dk. John Magufuli, amesikitishwa na kifo cha mwanafunzi huyo na kutoa pole kwa familia, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.

“Nimesikitishwa sana na kifo cha mwananafunzi Akwilina Akwilini wa chuo cha NIT, natoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.

“Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili,” aliandika Rais Magufuli katika ukurasa wake wa twitter.

MTANDAO WA WANAFUNZI

Wakati huo huo, Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), umesema utafungua kesi ya madai dhidi ya Jeshi la Polisi nchini kutokana na kifo cha mwanafunzi Akwilina.

Akizungumza jana waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TSNP, Abdul Nondo, alisema watafungua kesi hiyo kwa kushirikiana na wanasheria wa taasisi mbalimbali ili iwe fundisho kwa askari wengine.

Alisema kwamba, sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, sura ya 332, kifungu cha 29, kinaeleza mazingira ambayo polisi wanatakiwa kutumia nguvu kutuliza ghasia.

“Kama mwanafunzi huyu asiye na hatia ameuawa kwa mazingira ya namna hii, TSNP tunaona kuwa hili ni shambulizi dhidi ya wanafunzi nchini bila sababu yoyote.

“Tunataka hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya askari polisi waliotenda unyama huu na kukatisha haki ya kusoma na ya kuishi kwa mwanafunzi mwenzetu.

“Polisi, wamekiuka maadili ya kazi yao katika kulinda amani, Jeshi la Polisi, lijitathmini upya na kujipima namna linavyoenenda na kama lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia,” alisema Nondo.

Mtandao huo pia umemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji.

“Tumeshuhudia watu wakipigwa risasi, kutekwa, miili kuokotwa kandokando ya bahari na haya yote yanatokea pasipokuwapo kwa uchunguzi wa kina.

“Tanzania tumekuwa na chunguzi nyingi zinazoendelea na hadi sasa hazina majibu. Hivyo basi, sisi hatuamini kama uchunguzi pekee ndiyo utakuwa chachu ya kukomesha matendo yanayoendelea nchini.

“Ni muda muafaka sasa, waziri husika (Dk. Nchemba), kujiuzulu kama njia ya kuonyesha uwajibikaji kama alivyowahi kujiuzulu, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

“Lakini niwaambie kwamba, kama matukio ya aina hii yataendelea, basi tutaitisha maandamano ya wanafunzi ya vyuo vyote nchini kulalamikia uvunjwaji wa haki za binadamu,” alisema Nondo.

Naye Mwalikishi wa Klabu za Haki za Binadamu nchini, Alfahad Thabo, alisema hivi sasa wana mashaka na usalama wao kwa sababu vitendo hivyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara.

ACT  WAMVAA MWIGULU

Nayo ngome ya Vijana wa Chama cha ACT Wazalendo, imemtaka Dk. Mwigulu ajiuzulu kutokana na kuongezeka kwa matukio ya mauaji nchini.

Pia, ngome hiyo imewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na Kamanda Mambosasa, nao wajiuzulu.

Aidha ngome hiyo imewataka viongozi wote wa vyama vya upinzani kushirikiana na kuitisha maandamano nchi nzima ili kupinga mauaji, utekaji watu na ubakwaji wa demokrasia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome hiyo, Likapo Likapo, alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa matukio ya mauaji, utekaji na kupotea kwa watu huku jeshi hilo likishindwa kutoa taarifa za kina.

CHADEMA WATUPA MZIGO

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mtu wa kwanza aliyesababisha kifo cha Akwilina ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Kinondoni, Aron Kagurumjuli kwa kukataa kutoa viapo kwa mawakala wao.

Kigaila alisema polisi siku hiyo walilenga kuwapiga risasi viongozi wakuu wa chama hicho kwa sababu majeruhi wote wanne ambao wako hospitali ni walinzi wa viongozi hao.

“Tulikuwa na msafara siku ile kwa sababu tulikuwa tunakwenda kwa mkurugenzi kudai viapo vya mawakala wetu hivyo mtu wa kwanza alisababisha kifo cha huyu mwanafunzi ni msimamizi wa uchaguzi.

“Risasi iliyopigwa ikamwua yule mwanafunzi Mambosasa (Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa) anasema ni moja halafu wamekamata askari sita, sasa askari wote hao walipiga risasi moja na aliyeamuru risasi zipigwe juu ni nani?

“Risasi zile zililenga viongozi wa chadema ndio maana waliopatwa ni walinzi wao. Watu wanne wote waliopigwa risasi ukiachana na huyo mwanafunzi wako hospitali wamepigwa sehemu za nyonga na miguu,”alisema Kigaila.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema chama hicho kinatoa pole kwa familia ya marehemu na kwamba tayari Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Meya wa Ubungo wametangulia nyumbani kwa ndugu wa mwanafunzi huyo eneo la Kibamba.

“Kwa sasa kina Mnyika wametangulia nyumbani kwa ndugu ambao walikuwa wakimlea marehemu baada ya hapo tutawaeleza ushiriki wetu kwenye msiba huu mzito.

“Jeshi la polisi lichukue hatua waache visingizio, tumechoka na mauaji haya…tumechoka viongozi wetu kuwindwa kama digidigi ,”alisema Mrema.

Alieleza kushangazwa kwa hatua ya Kamanda Mambosasa kumtafuta Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wakati hajajificha na kwamba hajapewa wito wowote wa kwenda kuripoti polisi.

“Wanazo taratibu za kumwita mtu polisi, wanafahamu nyumbani kwake, ofisini kwake makao makuu ya chama au ofisi za Bunge,”alisema.

HABARI HII IMEANDALIWA NA UPENDO MOSHA (KILIMANJARO), Asha Bani, Nora Damian, Elizabeth Hombo na Tunu Nassor (DAR)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles