Na Mwandishi Wetu,
UKATILI wa nyumbani ni aina ya tabia inayotumika kujenga uwezo wa mtu mmoja kummiliki mwingine kwa kutumia vitisho na woga.
Athari ya ugomvi nyumbani pamoja na mambo mengine hutokana na kipigo cha wazi au cha kisiri, kuitana majina yasiyofaa, kutumia fedha kwa madhumuni ya kumiliki wengine, kutumia lugha ya matusi, kubaka watoto ndani ya nyumba, kuwamiliki watoto, kutenga na kutumia vitisho.
Niliwahi kuhudhuria kongamano moja lililoendesha mada za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya mtoto wa kike.
Binti mmoja aliinuka na kuweka bayana namna alivyokosa elimu baada ya kukataa kufanya mapenzi na kaka yake wa kuzaliwa na baba na mama mmoja.
Binti huyo alitoa ushuhuda wa nini kilichotokea baada ya kufiwa na wazazi wao. Kwamba alilazimika kuishi na kaka yake aliyekuwa na uwezo mkubwa wa fedha.
Tofauti na mawazo ya binti huyo, alijikuta akiangukia katika manyanyaso ya hali ya juu kutoka kwa kaka yake ambaye ni tajiri. Alichohitaji ni elimu na si mapenzi.
Cha kushangaza ni kuwa kaka yake huyo akampa masharti kwamba kama anataka kuendelea na masomo basi awe tayari kufanya naye mapenzi. Wakati huo binti huyo alikuwa kidato cha pili. Kitendo hicho kilimfanya ashangae kama kweli kaka yake wa damu angeweza kumtaka kimapenzi.
Baada ya kutofautiana katika suala hilo, binti akawa hana namna nyingine. Akashikilia msimamo wake wa kutokubali kulala na kaka yake wa kuzaliwa. Kilichoendelea baada ya hapo ni vitisho na vipigo vya mara kwa mara na hata kula yake ikawa ya shaka.
Hakuna ndugu wa karibu aliyejaribu kuingilia suala hilo kutokana na mfumo dume unaoendelea sehemu nyingi ndani ya Tanzania. Kilichotokea ni kuwa binti huyo akakosa masomo na kuamua kuingia mtaani kusaka vibarua ili apate mkate wa kila siku japo kwa mateso makubwa.
Kwa hiyo unaweza kuona kuwa tatizo la unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji limeendelea kushuhudiwa si Tanzania tu bali hata katika baadhi ya nchi za Afrika linatajwa kuwa ni changamoto kubwa kwa wateteaji wa haki za wanawake na hasa wasichana. Pamoja na mambo mengine, naamini tukidhamiria tunaweza kumaliza tatizo hili.
Wakati fulani, maofisa usalama kutoka nchi zote za Bara la Afrika walikutana jijini Kigali, Rwanda kupanga mikakati ya kulikomesha tatizo hilo.
Walijadili masuala mengi hasa changamoto na jinsi ya kufuta kabisa tatizo hilo linatokana na mila potofu katika bara hilo.
Ubabe wa kidume na usiri wa kutotaka kutoa ushirikiano na taasisi zinazokemea unyanyasaji. Makabila au jamii nyingi zimekuwa zikitishwa kuwa kuachana na mila zao ni sawa na kuwaudhi mizimu ya mababu jambo ambalo si sahihi.