30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tukatae hulka ya kutosumbua akili zetu

UKIAMUA kukaa bila kusumbua akili yako kutafuta kitu cha kufanya, utaendelea kubaki hivyo hivyo na kama ukiamua kufanya jambo la maendeleo pamoja na changamoto utakazokutana nazo usipokata tamaa, ni wazi utajifunza, utafikiri zaidi na hata kusonga mbele. 

Tumelazimika kuzungumzia haya kutokana na ukweli kwamba, miongoni mwetu wengi tumejenga hulka ya uvivu pasipo kujua kwamba tunatengeneza bomu la hatari katika Taifa letu.

Uvivu maana yake ni kutokuwa tayari kufanya kazi au kutumia nguvu zetu, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo. 

Wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema mara nyingi hii hutokea kutokana na mawazo yetu potofu au mabaya. 

Kwa upande wa dini zetu, tabia ya uvivu ni dhambi na ndiyo maana watu wenye tabia hizi wengi wao, si wote, mara nyingi huishia kuvuta dawa za kulevya, kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu n.k kwa sababu ya uvivu hukusababisha ushindwe kufanya vitu vya muhimu unavyovihitaji katika maisha.

Leo hii na hasa nyakati za mvua  si ajabu ukapita katika maeneo fulani ya nchi (si yote bali mikoa fulani fulani), licha ya kubarikiwa kuwa na ardhi nzuri, ukashangaa kuona mashamba yao hayajalimwa wala kupandwa chochote, ukiuliza  sababu utakazoelezwa unagundua msingi wake ni uvivu.

Si hilo tu, kuongezeka kwa wimbi la vijana wenye elimu na wasio na elimu katika vijiwe mbalimbali na hata kujiingiza katika matendo yasiyofaa, hili nalo limebeba sura tofauti.

Licha ya serikali kwa upande wake kushutumiwa kutokuwa na mipango bora ya kuwapatia ajira, lakini wapo baadhi ya vijana ambao huogopa kutumia fursa zilizopo kwa sababu tu haziendani na hadhi zao za kielimu au kuogopa changamoto na pengine uvivu.

Hili tunasema ni tatizo jingine 

Tangu Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani, pamoja na mambo mengine yote amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kukerwa na kitu kinachoitwa uvivu.

Mara kadhaa Rais Magufuli amekaririwa akisema kuwa, katika utawala wake hakutakuwa na vitu vya bure. 

Kwamba wakati wa kukaa kwenye magenge na kupiga maneno umepita.

Pamoja na kwamba kauli kama hizo zimekuwa kikiwakera baadhi, lakini huo ndio ukweli mchungu tusioupenda kuusikia baadhi yetu.

Kwa sababu hiyo, sisi tunaona yapo ambayo yanapaswa kufanywa na serikali ili kuwaondoa watu katika dimbwi  hili, kama kutengeneza ajira na fursa ambazo zitawapatia kipato wananchi wake.

Lakini kwa upande wa kila mmoja wetu, tunapaswa kukataa tabia ya uvivu, na msingi wa kwanza ni kubadili fikra zetu, tukifanya hivyo tutaweza kuona fursa kupitia changamoto zilizopo.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles