26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

TUIMARISHE ULINZI WAKATI WA SIKUKUU

cktqipsucaafgpj

LEO ni maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi. Waumini wa madhehebu mbalimbali ya kikristo wanaungana na waumini wengine kote duniani kusherehekea kuzaliwa kwa mwokozi wao.

Hapa nchini kama ilivyo sehemu nyingine, watu wanasherehekea na familia, ndugu, marafiki na jamaa zao.

Pia wiki ijayo kutakuwa na shamrashamra za kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.

Wakati watu wakiwa katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, MTANZANIA Jumapili tuna kumbukumbu ya matukio kadha wa kadha ya uhalifu yaliyowahi kutokea miaka ya nyuma katika kipindi kama hiki.

Kwamba imekuwa kawaida kila mwisho wa mwaka baadhi ya wahalifu kuwakaba, kuwaua, kuwajeruhi au kuwapora watu pindi wanaposherehekea sikukuu hizo.

Taarifa za MTANZANIA Jumapili zinaonyesha kuwa katika msimu wa sikukuu hizi ndipo matukio ya uhalifu yanapoongezeka na inasemekana kuongezeka uko kunatokana na ukweli kuwa wahalifu hao huwa wanatafuta fedha za kujikimu katika kipindi hiki.

Kutokana na vitendo hivyo kuongezeka, ambavyo vingi kati ya hivyo vinatajwa kufanywa na vijana wanaodaiwa kutokuwa na ajira, sisi wa MTANZANIA Jumapili tunawaomba wananchi wote kushirikiana kuimarisha ulinzi katika maeneo yao.

Tayari Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwamba uhalifu unaweza kutokea kipindi hiki na wao wamejipanga kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha katika kipindi chote cha sikukuu ili wananchi washerehekee kwa amani na utulivu kutokana na vitendo vingi vya uhalifu kufanywa na watu wenye nia ovu.

Kwahiyo jeshi hilo litaimarisha doria katika maeneo mbalimbali na kupeleka askari katika kila kanisa ili kuhakikisha ibada zinafanyika kwa hali ya amani na utulivu.

Kwamba litatumia askari wenye sare na makachero watakaofanya ulinzi maeneo mbalimbali.

Pia litatumia helkoptia kuimarisha ulinzi zaidi na litahakikisha kila mtaa unakuwa na askari wakishirikiana na mgambo au walinzi shirikishi.

Kwamba jeshi hilo linawataka wananchi kuwa waangalifu kwa kutokunywa vileo kupita kiasi ili kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuzua ugomvi.

Pia watakaokwenda katika fukwe za bahari wanatakiwa kuwa waangalifu na wachukue tahadhari kwa kutowaruhusu watoto kuogelea peke yao na kuepuka kuogelea wakiwa wametumia vileo jambo linaloweza kusababisha madhara.

Jeshi hilo pia linawataka watakaotumia magari binafsi kuhakikisha wanayaegesha katika maeneo salama na kuyafunga vizuri na kuwataka wananchi kutoa taarifa sehemu husika pale wanapoona viashiria vya uhalifu ili wapate msaada.

Kama taarifa ya tahadhari ya polisi ilivyotolewa, sisi wa MTANZANIA Jumapili tunaendelea kuwakumbusha wananchi kuwa makini, hasa watakapokuwa maeneo ya starehe na biashara.

Pia umakini unahitajika zaidi ndani ya vyombo vya usafiri, na barabarani kwa waenda kwa miguu, maeneo yote ya kuabudia na katika mikusanyiko mikubwa ya watu.

Si hivyo tu, pia katika kipindi hiki wananchi wanatakiwa kuwa makini na taarifa zinazosambaa mitandaoni, ambazo nyingine zinakuwa za uchochezi, uongo, upotoshaji, ikiwamo vitendo vya utapeli kwa sababu huwa zinaleta mkanganyiko na taharuki ndani ya jamii.

Tunaliomba jeshi hilo nalo kuimarisha ulinzi kama lilivyosema ili kuhakikisha vitendo vyote vya uhalifu vinadhibitiwa kutokana na taarifa zao za kiintelejensia.

Pia tunalikumbusha kutekeleza amri yao ya kupiga marufuku kufanyika kwa burudani za watoto maarufu kama ‘disko toto’ katika kumbi mbalimbali za starehe wakati huu wa sikukuu kutokana na madhara yaliyowahi kutokea siku za nyuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles