23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tuendako: Absalom Kibanda asema tusijidanganye, Mo Dewji kutekwa kunatikisa misingi ya uasisi wa Tanzania ya Nyerere

Na Absalom Kibanda

TUKIO la kutekwa kwa mfanyabiashara mashuhuri na mtu anayetajwa na jarida la Forbes na vyombo vingine mbalimbali vya habari vya kimataifa kuwa bilionea kijana zaidi Afrika, Mohammed Dewji, al-maarufu Mo, bado linaendelea kugusa hisia za watu walio wengi nchini.

Fikra na mazungumzo ya Watanzania walio wengi kwa sasa ukichanganya na habari katika mitandao ya kijamii, magazeti, redio na televisheni vyote vimejaa habari na taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo ambaye hadi sasa hajapatikana.

Kwa namna ambayo si rahisi kuielezea na pengine inayovuka mipaka ya ubinadamu, jambo moja ni dhahiri kwamba tukio la kutekwa kwa Mo Dewji limeonesha namna mfanyabiashara huyo alivyoutikisa ulimwengu wa habari kitaifa na kimataifa.

Kwa mara nyingine, habari ya kutekwa kwa Mo Dewji imethibitisha namna kile ambacho kimekuwa kikielezwa na wachambuzi wa ki-Afrika kwa miaka mingi, kwamba habari mbaya zinazoligusa bara hili ndizo ambazo mvumo wake huwa na kishindo kikubwa kuliko habari njema na za mafanikio na maendeleo.

Nadharia hiyo ya ki-Afrika inakinzana na nadharia ya magwiji wa masuala ya habari na mawasiliano ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisema ‘Bad news is good news’, yaani habari mbaya ndiyo habari inayobeba uzito mkubwa zaidi. Mjadala juu ya uhalisia wa nadharia hizi si wa leo.

Nilimfahamu Mo Dewji mwaka 2000 wakati wa kampeni za urais na ubunge.

Nilikutana naye Singida wakati huo nikiwa katika timu ya waandishi wa habari ambao tulikuwa tumeandamana na Rais Benjamin Mkapa katika kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuongoza taifa kwa muhula wa pili baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza kwa mafanikio makubwa.

Nilikutanishwa na Mo Dewji na mmoja wa waandishi wenzangu wa habari, Mpoki Bukuku, sasa marehemu, ambaye alitangulia kufika Singida kwa mwaliko mahususi wa mfanyabiashara huyo ambaye walikuwa marafiki wa karibu kikazi.

Mo Dewji alikuwa Singida akimsubiri Mkapa kwani mwaka huo wa 2000, akiwa bado kijana mdogo, alikuwa ni mmoja wa wana CCM ambao walichukua fomu za kugombea ubunge wa Jimbo la Singida Mjini na akaibuka mshindi katika kura za maoni, kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho tawala kuliengua jina lake.

Uamuzi wa kamati hiyo kuliengua jina la Mo Dewji katika kinyang’anyiro cha ubunge, ulizusha maneno mengi na taarifa ambazo zilishakuwa zikiripotiwa katika vyombo vya habari, zilikuwa zikionesha kwamba mgombea wa chama hicho tawala aliyepitishwa Juma Nkangaa hakuwa na mvuto.

Ili kufuta maneno maneno hayo, Mkapa alipofika Singida Mjini kwa makusudi alimpandisha jukwaani Mo Dewji ambaye aliposimama uwanja mzima ulizizima kwa shangwe na vigelegele vya kumkubali.

Akihutubia umati mkubwa uliojitokeza kumlaki Mkapa, mfanyabiashara huyo aliwahakikishia wana Singida kwamba alikuwa hana kinyongo na uamuzi wa Kamati Kuu kulikata jina lake na akaahidi kumuunga mkono kwa nguvu zake zote Nkangaa ambaye alikuwa mwanasiasa mkongwe na mwenye jina kubwa wakati huo.

Hotuba ya Mo Dewji si tu kwamba ilimhakikishia ushindi Nkangaa, bali pia ilimwezesha Mkapa kwanza kutoa hotuba ya kumsifu mfanyabiashara huyo kijana ambaye wakati huo alikuwa na takribani umri wa miaka 24 kabla ya yeye mwenyewe kujiombea kura na kuvuta hamasa kubwa kutoka kwa wana Singida.

Alipopata fursa ya kuteta kwa muda mfupi na sisi kabla na baada ya kupanda jukwaani katika Uwanja wa Namfua, Mo Dewji alitueleza kwamba viongozi wakuu wa CCM walikuwa wamemhakikisha yeye ndiye atabeba bendera ya chama hicho miaka mitano baadaye na wakamtaka kutokatishwa tamaa na uamuzi wa Kamati Kuu kuliengua jina lake.

Tukio hilo ndilo ambalo kwa mara ya kwanza lilinikutanisha na Mo Dewji na kumfahamu kama mfanyabiashara mdogo aliyekuwa akizungumza Kiswahili kisichonyooka ingawa alikuwa kipenzi cha wana Singida, hasa vijana kutokana na hulka yake ya kuchanganyika na watu na kuwasaidia wakazi wengi wa huko kimaisha.

Wasifu wa Mo Dewji uliotolewa na Mkapa mwenyewe kabla hatujasikia sifa zake kutoka kwa makada wengine wa CCM wa zama hizo, akiwapo Frank Uhahula, ulikuwa ukimtaja kuwa mpenda maendeleo, anayejali shida za wengine, mtu wa watu, kijana tajiri asiye na makuu na ambaye alikataa katakata kujiona bora kuliko wana Singida wenzake ambao wengi wao walikuwa wakiishi maisha ya dhiki.

Kama ilivyotarajiwa na kupangwa, Mo aliteuliwa na CCM kuwa mgombea ubunge mwaka 2005 na kisha akaibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha uwakilishi huko Singida Mjini.

Akiwa mfanyabiashara, mwanasiasa na baadaye mwanamichezo, hulka ya Mo ya kuwa mtu wa watu, mcheshi, msikivu na mnyenyekevu imeendelea kubakia katika kipindi chote cha miaka 18 nilichomfahamu.

Katika kipindi chote hicho, mara kadhaa nimepata kukutana na kuzungumza naye ofisini kwake, nje ya ofisi yake na mara moja tukakutana Johannesburg Afrika Kusini ambako yeye alikuwa katika shughuli zake kibiashara na mie nikiwa katika mkutano mmoja wa kihabari.

Mo ni mwepesi kuomba, kusikia na kusikiliza ushauri. Ni rafiki si tu wa waandishi wa habari, bali pia wafanyabiashara wenzake na hata wanasiasa wengi vijana wa ndani ya CCM, hata wale wa upinzani.

Akiwa mbunge hadi mwaka 2015 alipoamua kwa hiyari yake kujikita katika biashara na shughuli zake binafsi, Mo ameendelea kuwa mpenda maendeleo mkubwa na mtu aliye wazi kuchochea fikra za maendeleo kwa vijana, akiendesha kampeni zake kupitia vyombo vya habari na mara kadhaa kupitia ukurasa wake wa twitter.

Aina ya maisha ambayo anaishi ndiyo ambayo imesababisha kelele nyingi za kumlilia na za kutaka aachiwe na watekaji wake ambao hadi sasa taarifa au makusudi yao hayajaelezwa si na vyombo vya dola au familia yake.

Tumesikia kauli nzito kutoka kwa wakuu wa polisi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani, familia yake, wanasiasa, wasomi, viongozi wa kiimani na Watanzania kwa ujumla, wote wakitaka kuona mfanyabiashara huyo akirejea salama.

Mfanyabiashara huyo ametekwa na watu wasiojulikana na ambao katika taarifa za awali za kiusalama walihusishwa na watu wanaotajwa kuwa raia wa kigeni ambao waliendesha operesheni hiyo alfajiri ya saa 11:00 katika eneo maarufu la Oysterbay.

Kutajwa kwa raia wa kigeni weupe katika utekaji wa Mo, kumewafanya baadhi ya wachambuzi wa mambo kulifananisha tukio hilo na mengine ya kiharamia ambayo yamekuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali Afrika na duniani kote.

Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amevishangaa vyombo vya ulinzi na usalama akisema vilipaswa viwe vimeshajipanga muda mrefu kukabiliana na uharamia wa kimataifa wa namna hii ambao tumekuwa tukiuona au kuusikia katika mataifa mengine.

Mzee Malecela hakuishia hapo, pengine akirejea matukio kama yale ya kujeruhiwa kwa Tundu Lissu, kupotea kwa watu kadhaa akiwamo mwanasiasa kijana wa Chadema, Ben Saanane na mwandishi wa habari Azory Gwandu pasipo kuwataja, akasema tusipokuwa makini tunaweza kufikia kiwango cha uhalifu cha Afrika Kusini.

Nina kila sababu ya kuamini kwamba taasisi za ulinzi na usalama zimeyachukulia kwa uzito mkubwa maneno na ushauri wa Mzee Malecela kwani tupende tusipende, kuendelea kusema kuwa eti matukio ya namna hii hayana madhara kisiasa, kibiashara au kiuwekezaji ni kujidanganya wenyewe.

Kila taifa lina utamaduni wake. Msingi mama wa utamaduni wetu ni amani. Kuyaacha matukio haya yaendelee ni kutikisa moja ya tunu za kihistoria za taifa hili ambazo kwa bahati mbaya tumeshindwa kwa miaka mingi kuzitumia kujiletea ustawi wa taifa.

Watu ambao wamekuwa wakishangazwa na aina ya maisha ya mtu wa kawaida aliyokuwa akiishi Mo Dewji, wanapaswa kutambua kuwa msingi wake ni utamaduni wa asili wa amani.

Aina ya maisha ya Mo Dewji wanaishi matajiri wengi hapa nchini na ndiyo maisha ambayo hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyere alipenda sana kuyaishi nyumbani kwake Msasani na mara kadhaa Butiama ambako alikuwa na uwezo wa kutoka mwenyewe wakati mwingine bila walinzi wake kwenda shamba au kucheza bao.

Ni bahati mbaya kwamba tukio la Mo Dewji kutekwa limetokea siku tatu kabla ya maadhimisho ya miaka 19 tangu Baba wa Taifa afariki dunia Oktoba 14, 1999.

Kwa watu wanaomuenzi kweli kweli Baba wa Taifa, ambaye leo hii wengine wanatamani atangazwe Mtakatifu kwa imani ya Wakatoliki, tukio la kutekwa kwa Mo limeongeza wingi wa machozi ya kumlilia na kumkumbuka Mwalimu.

Huu si wakati wa kudai uhuru, hii si miaka ya ukombozi kama ile ya 1960 na 1970. Hizi ni zama za kuimarisha amani, umoja wa kitaifa, undugu, mshikamano, demokrasia, haki za binadamu na upendo. Huo ndiyo hasa maana ya Utanzania.

Haya yanayotokea leo kwa akina Mo Dewji kutekwa yanakinzana na msingi mama wa utaifa wetu. Tukijifanya hatuyaoni au tunayapuuza, basi tufanye hivyo kwa gharama za urithi wetu siku zijazo. Urithi unajengwa leo. Historia itatuhukumu kwa haki huko TUENDAKO.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles