32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO: ABSALOM KIBANDA AMSHAURI JPM KUANZA ALIPOKWAMIA MKAPA

Rais Dk. John Magufuli akiwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa

NA ABSALOM KIBANDA                     |                         


NAANDIKA makala hii wakati Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akiwa nyumbani kwao Chato ambako japo alikwenda kwa sababu ya mapumziko mafupi, lakini amefikwa na msiba mzito wa kumpoteza dada yake, Monica.

Nina kila sababu ya kuungana na Watanzania wenzangu, kumtumia salamu za pole Rais Magufuli kwa kumpoteza dada yake na hivyo kwa kiwango kikubwa kusababisha alazimike kusitisha kwa muda majukumu yake mengine ambayo yumkini angeweza kuyafanya akiwa mapumzikoni. Msiba unaomkuta rais unali- gusa taifa.

Nilihitimisha andiko langu la wiki iliyopita linalotoka kila Jumatano katika gazeti la Mtanzania kwa kueleza namna fikra na tafakuri jadidi za mwanazuoni Issa Shivji, profesa wa Kigoda cha Mwalimu juu ya taswira ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mazingira na mfumo wa vyama vingi.

Hitimisho hilo, liligusia pia japo kwa muhtasari tu, ushauri adhimu wa mwanasiasa kijana, msomi, jasiri na mtukutu, Zitto Kabwe kwa Serikali ya JPM juu ya namna inavyoweza kuiendesha nchi kwa njia ya kumaliza vitendo vya uhasama, chuki, kuumizana na ukatili ambao kwa sehemu umehusisha vyombo vya dola, hususani Jeshi la Polisi.

Andiko langu lile ambalo kichwa chake cha habari kilikuwa ‘Kiporo cha fikra za Shivji na maarifa ya Zitto’ lilipokewa kwa namna na kwa hisia tofauti kutoka kwa wasomaji mbalimbali waliowasiliana nami.

Wako wasomaji wa makala ile waliokubaliana na tafakuri, wako walioshabikia na wako waliohoji na kutofautiana nami kwa maana ya kukosoa hoja mbalimbali ambazo zilibebwa na andiko lile. Bado nasubiri kusoma makala za wachambuzi wengine ambao waliahidi kujibu.

Andiko lile ukijumlisha na maoni na hoja mbalimbali zilizoibuliwa na miye mwenyewe na wasomaji wengine, ndio msingi mama wa andiko langu la leo, nikilielekeza kwa Rais wangu, Dk. Magufuli, ambaye bado naamini anayo hulka yake ile ile ya zama akiwa waziri, ya kufuatilia kwa kina na kwa ukaribu mkubwa maandiko ya namna hii.

Swali moja la msingi ambalo nimekuwa nikijiuliza na limekuwa likiulizwa na watu wengine wengi, kabla na baada ya andiko langu lile ni; ‘Ni nini basi sisi kama taifa na Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM dola tunapaswa kufanya ili hatimaye tufikie ndoto za kuwa na Tanzania njema?’

Tanzania njema ninayoizungumzia ni ile ambayo kila Mtanzania atakuwa na wajibu wa kufanya kazi halali na ambayo kaulimbiu ya Rais ya “Hapa Kazi Tu’ itabeba maana halisi ya wajibu wenye tija na faida kwa wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara.

Tutakuwa tukifanya masihara iwapo tutawaacha viongozi waendelee kuwahamasisha Watanzania kufanya kazi katika mazingira yasiyo na tija wala faida.

Kuruhusu kuendelea kwa hali hii kunaweza kukasababisha kazi ikageuka laana na matokeo yake ule msamiati wa ‘Bongoland’ uliopata kumvuruga rais mmoja mstaafu ukarejea na kutamalaki katika maisha halisi ya leo na kesho.

Kwa sababu hiyo basi, Tanzania Njema ninayoizungumzia ni ile itakayotambua na kuheshimu utawala wa sheria na misingi yote ya utawala bora kwa maana ya kutii mamlaka halali ya dola sambamba na wale walio na nafasi za uongozi kutambua kwamba wamepewa dhamana za uwakilishi na mamlaka ya uamuzi na utendaji ambavyo haviwapi uhalali wa kufanya lolote la kuhujumu au kuumiza wengine au kulihujumu taifa.

Katika hili, watawala na watawaliwa, wote tunao wajibu wa kutimiza wajibu wetu.

Mkwepa kodi, mfujaji wa mali ya umma na mwizi ni mhalifu kwa kiwango kilekile cha uhalifu alichonacho kiongozi muuza nchi, mbinafsi na fisadi anayetumia wadhifa kama fursa aliyonayo kujinufaisha binafsi kwa gharama za kuumiza wengine.

Tanzania Njema ya ndoto za waasisi wa taifa hili, ni ile inayoheshimu haki ya kila mmoja kuishi, kutoa maoni na mawazo yake pasipo kutishwa au kuhofia kuporwa haki za msingi kama uhuru na maisha yake.

Kwa mfano, hatuwezi tukasema tunalo taifa huru, la kidemokrasia na linaloheshimu haki za binadamu wakati kukiwa na Watanzania wenzetu wa aina ya Tundu Lissu, Ben Saanane, Azori Gwanda na kabla yao, Dk. Steven Ulimboka na Daudi Mwangosi, ambao ama waliumizwa, kutoweka na wengine kufa katika mazingira yanayoshawishi kuwapo bayana kwa jitihada za baadhi ya watu au makundi ya kihalifu ndani ya nchi yaliyojipa uhalali wa, kuwaziba wengine midomo kikatili na hata kuamua hatima zao.

Matukio ya namna hii si tu yanaishia katika kuchafua taswira ya kihistoria na mtaji mama wa utanzania wetu unaotumiwa kujitangaza ndani na nje ya nchi yetu, kwamba tunaishi katika taifa linaloenzi amani, umoja na mshikamano kama tunu za kipekee, bali pia yanajenga msingi wa chuki ya kudumu, hulka za kulipa kisasi na kutoaminiana miongoni mwa Watanzania wenye nafasi mbalimbali katika jamii.

Yanapotokea matukio ya kuogofya ya aina hiyo na watu wakabaki vinywa wazi wakishangaa huku wengine wakibakia kuwa ama na majeraha ya kudumu mioy- oni au mwilini pasipo kujua kwa uhakika ni akina nani hasa wako nyuma ya ukatili wa namna hiyo, ndoto ya Tanzania njema inakuwa ni mbali sana kufikiwa.

Tutakuwa tunajidanganya wenyewe, iwapo tutaendelea kujiaminisha au kujidanganya kwa sababu tu ya ulevi wowote wa kifikra, kwamba watu au dunia itasa- hau vitendo vya ukatili dhidi ya wanadamu wengine kadiri muda unavyosonga mbele.

Watanzania tunapaswa kujifunza kutokana na siasa za ushindani na wakati mwingine za kisasi za kule Zanzibar, am- bazo kwa takribani miaka 54 sasa, watoto, wajukuu na vitukuu bado wanaendelea kubeba kumbukumbu ya mema na majeraha yale yale ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na yale ya kabla ya hapo.

Kwa namna ile ile ambayo CCM inajivunia urithi wa kihistoria wa waasisi wake akina Julius Nyerere, TANU na ASP ya Mzee Abeid Amani Karume, ndivyo ambavyo matendo mengine mabaya ya kihistoria kama yale yanayohusishwa na kile kinachoonekana kuwa uporaji wa kura kule Zanzibar, tangu mwaka 1995, yanaendelea kubakia kuwa katika vichwa vya watu pasipo kukoma.

Kwa sababu hiyo basi, Tanzania njema ya ndoto zetu inapaswa kuanza kujengwa sasa kwa viongozi na watawaliwa kuanza kuonesha kwa vitendo kukerwa na kukataa hulka za ‘uMungu mtu’ wa mtu mmoja au kikundi cha watu fulani, au chama cha siasa, kujiona kuwa wenye dhamana isiyohojiwa au kukosolewa juu ya maisha ya Watanzania na hatima ya kesho na keshokutwa ya taifa letu.

Iwapo kwa sababu zozote zile tunapata shida kujifunza kwa makosa yetu wenyewe, basi viongozi wetu wa kisiasa, kisheria na kijamii wanapaswa kujifunza hata kwa makosa yaliyopata kufanywa na ama majirani zetu, marafiki zetu au mataifa mengine.

Afrika Kusini inaweza ikawa darasa zuri la kuponya majeraha yetu, hata kama ukubwa wa vidonda vyetu haufanani na makali na machungu waliyopitia akina Nelson Mandela, Oliver Tambo, Chris Hani, Winnie Mandela, ANC na PAC nyakati za udhalimu wa sera katili za ubaguzi wa rangi.

Shinikizo kubwa dhidi ya ukaburu lililoanzia ndani ya taifa hilo kabla ya kuungwa mkono na jumuiya ya kimatafa, liliwalazimisha makaburu kusalimu amri na hatimaye kumtoa kifungoni Mandela, baada ya jitihada za kumfunga jela kwa miaka 27 ili asahulike kushindwa.

Mandela alipotoka jela na baadaye akafanywa kuwa Rais wa Afrika Kusini, alibaini ukubwa wa majeraha na machungu waliyokuwa nayo ulikuwa hauwezi kumalizwa na rangi na urais wake.

Mara moja aliunda Tume ya Ukweli na Maridhiano iliyoongozwa na Askofu Desmond Tutu, mtu aliyeonekana kukubalika zaidi na watu wa rangi na makundi tofauti.

Tume hiyo ilichimba hadi katika kiini cha machungu na majeraha ya watu mbalimbali na ikahitimisha kazi yake kwa kupatikana mwafaka wa kitaifa.

yaliyoibuliwa na Tume ya Askofu Tutu, yalikuwa yakitosha kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria, makumi au mamia ya raia wa nchi hiyo, ambao wakati wa utawala wa makaburu walikiuka sheria na haki mbalimbali za utu na ubinadamu.

Orodha ya watu ambao makosa dhidi ya ubinadamu waliyofanya wakati wa utawala wa makaburu, iliwagusa watu wengi mashuhuri waliokuwa ndani ya chama cha ANC, ambacho kilikuwa kinara wa mapambano ya kuung’oa ubaguzi wa rangi nchini humo, akiwamo Winnie Mandela ambaye hadi wakati Mandela anatoka jela alionekana kuwa mwanamke aliyestahili kuvikwa taji la ‘Mama wa Taifa la Afrika Kusini’. Yaliyofuata baada ya hapo ni historia.

Tukirejea hapa nyumbani, naweza nikasema, kwamba nilikuwa ni miongoni mwa Watanzania tuliokuwa na imani kubwa na JPM alipoingia Ikulu ya Magogoni katika siku zake 100 za kwanza madarakani.

Hatua mbalimbali alizochukua au kutangaza zilionesha bayana kwamba hatimaye taifa lilikuwa limepata Mandela wake, aliyekuwa ‘amefungwa’ katika gereza la CCM- dola kwa miaka 20 akiwa waziri.

Wakati alipoanza kuunda serikali yake na baadaye akalihutubia Bunge, fikra zangu zilinifanya nifikie hatua ya kumwona pia akibeba zaidi taswira ya Askofu Tutu, hasa baada ya kuonesha aliingia madarakani akiwa amebeba mabegani mwake ajenda ya kuwa kinara wa maridhiano ya kitaifa.

Nachelea kusema moja kwa moja leo iwapo bado naendelea kumwona Mandela yule yule na pengine Askofu Tutu wa ndoto zangu ndani ya Rais JPM.

Hata hivyo, wakati nikijua kwamba, JPM amefikia nusu ya muhula wake wa urais, bado naamini anao muda wa kuchukua hatua mahususi kuweka kila kilichoharibika kabla mwisho haujafika.

Akiwa kiongozi ambaye kwa hulka ni mcha Mungu na msomaji mzuri wa Biblia nina kila sababu ya kumshawishi rais wangu akatae kupoteza ‘upakwa mafuta’ kama ilivyokuwa kwa mfalme Sauli na pengine aanze kuchukua hatua za kuepuka kukutana na mwisho wa Mfalme Daudi.

Ninayasema hayo kwa kuwa, nimekuwa mwanahabari mwenye imani na pengine shabiki mkubwa wa Magufuli tangu akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 1995 -2000.

Bado kumbukumbu zangu ni mbichi ninapokumbuka namna ilivyokuwa wakati Magufuli aliposhinda ubunge kule Biharamulo, tena akipita bila kupingwa mwaka 2000.

Wenye kumbukumbu kama zangu na hususani wanasiasa wa upinzani wa zama zile waliokuwa bungeni, kama Mabere Marando wanaweza wakawa mashahidi wazuri kwamba JPM alikuwa mmoja wa naibu mawaziri vijana maarufu zaidi wakati huo.
Tukio lake la kupita bila kupingwa kama ilivyokuwa kwa William Lukuvi, ambaye naye pia alikuwa naibu waziri, lilipokewa kwa bashasha na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa.

CCM, nadhani kwa maelekezo ya Mwenyekiti wao, Mkapa, iliwaandalia vijana wake JPM na Lukuvi sherehe za pongezi kwa kuiletea heshima Serikali na chama chao.
Shamrashamra hizo hatimaye zilihitimishwa na Mkapa mwenyewe kuwapandisha vyeo na kuwafanya mawaziri kamili ilipoundwa serikali mpya Novemba 2000.

Haikumpa shida Mkapa kumrejesha Magufuli katika wizara ile ile ya Ujenzi na kabla ya kumtaja kuwa miongoni mwa mawaziri hodari katika serikali yake aliowapa jina maarufu zama zile ‘askari wa miavuli’.

Miaka mitano ya kazi akiwa Wizara ya Ujenzi (2000 – 2005), ilikuwa ni ya kazi na mafanikio makubwa kwake mwenyewe JPM na hususani serikali nzima ya Mkapa.

Alikuwa ni Magufuli aliyeanza kwa kusimamia kikamilifu na kwa mafanikio makubwa kazi ya kutandaza barabara za lami katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa Mkapa.

Ni kipindi hicho akiwa waziri zama za Mkapa ndiye hasa aliyekuja na wazo ambalo lilipata upinzani mkubwa la kutumia fedha za ndani kujenga baadhi ya barabara za lami.

Uhodari wake kazini na uwezo wake wa kujibu maswali bungeni kwa takwimu, ulimfanya awe miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi na umaarufu mkubwa.

Itoshe kwa leo kusema, umaarufu huo uligeuka mwiba kwa baadhi ya mawaziri wenzake na harufu yake ikagusa hata hisia za urais kwa mara ya kwanza mwaka 2005.

Ni wazi kwamba mbegu ya uongozi ndani ya JPM ilipandwa na Mkapa kwa muda wa miaka 10 kati ya 1995-2005.

Bado naamini kwamba ili JPM aweze kuifinyanga vyema visheni ya urais wake na hatimaye kufikia kile alichopata kukisema kuwa ni matamanio ya kuja kuwaongoza malaika siku Mungu wake atakapomwita, basi atalazimika kuanza pale alipofundwa na ‘mentor’ wake Benjamin Mkapa.

Itaendelea Jumatano ijayo…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles