24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

TUENDAKO: Absalom Kibanda amjibu Lissu

NA ABSALOM KIBANDA                    |                   


NIMELISOMA andiko la Mheshimiwa Tundu Lissu juu ya hili wimbi la wabunge na madiwani wa Chadema kuondoka katika chama hicho na kujiunga na CCM.

Sina shaka hata kidogo kwamba ndugu yangu Lissu amejieleza vizuri akifanya rejea kwa namna yenye ushawishi mkubwa.

Katika andiko lake hilo, Lissu pamoja na mambo mengi, amezungumzia suala la ruzuku ya Chadema ambayo kwa miaka nenda miaka rudi imekuwa ikitumiwa na wahamaji hao kama hoja ya kukinyooshea kidole chama hicho.

Katika hili, Lissu kaeleza hapa safari ngumu sana na ndefu ambayo imeiwezesha Chadema kupata takribani shilingi milioni 250 za ruzuku kwa mwezi kuanzia mwaka 2015 kutoka kiasi cha shilingi milioni 5.6 ambazo walikuwa wakipata kati ya mwaka 2000-2005.

Kwa bahati mbaya katika andiko lake hilo, hata mara moja Lissu hajaeleza namna ambavyo ruzuku hiyo imekuwa ikitumika ukiacha mbali hoja ya ulipaji madeni ambayo imesemwa semwa sana.

Kwa maelezo yake kwa bahati mbaya au kwa sababu mahususi, Mheshimiwa Lissu anatoa maelezo yanayoweza kwa makosa yakatoa tafsiri isiyo sahihi kwamba ni Mwenyekiti Freeman Mbowe peke yake ndiye ambaye amekuwa akitafuta fedha kwa ajili ya kufadhili kampeni kwa maombi yasiyokoma ya Kamati Kuu.

Japo kuna sehemu anaeleza juu ya kuwapo kwa michango ya wabunge ambayo hataji utaratibu wanaotumia katika kuchangishana, haelezi japo kwa muhtasari namna fedha hizo zinavyotumika.

Ukimsoma katikati ya mistari unaweza kuona namna andiko lake linavyojaribu kuuaminisha umma kwamba, Chadema imekuwa ikiendeshwa kwa hekima na utafutaji wa fedha wa mtu mmoja kwa maombi yasiyokoma ya Kamati Kuu.

Katika mazingira ya namna hii aliyoeleza Lissu, ni rahisi sana kwa Chadema kushindwa kukwepa tuhuma kwamba chama hicho kimekuwa kikiendeshwa kama kampuni binafsi ya mtu mmoja anayewekeza fedha, kwangu hili lina ukakasi.

Andiko la Lissu ukiacha ukweli kwamba linashawishi wana Chadema kuendelea kuheshimu na kuenzi mchango wa kipekee wa Mwenyekiti Mbowe, linaonesha udhaifu mkubwa kwa Kamati Kuu ya Chadema katika kuendesha chama katika misingi ya uwajibikaji wa pamoja.

Ni jambo la heri kwamba Lissu anaweza akakumbuka kwa tarakimu halisi kiwango cha ruzuku lakini akashindwa kuonesha ni kiasi gani cha fedha ambacho Mbowe amekuwa akichangia au gharama za makisio ya jumla ambazo chama kimekuwa kikitumia katika shughuli zake mbalimbali za kisiasa.

Katika hilo pia, Lissu haelezi iwapo fedha ambazo zimekuwa zikitafutwa na Mbowe zote zimekuwa zinatolewa na yeye moja kwa moja kutoka mfukoni mwake au zilitoka mifukoni mwa wapenzi wa Chadema na/au pengine wapenda demokrasia.

Haelezi pia iwapo fedha hizo zimekuwa zikitolewa kama msaada isiyo na masharti au mikopo au michango ya hiyari ya marafiki, wapenzi na wapenda demokrasia….

Ukiacha mambo hayo, Lissu anahitimisha kwa kuandika kiungwana kwamba wao katika Chadema si malaika, wana udhaifu wao.

Kwa bahati mbaya katika hili pia, Lissu anakosa ujasiri au amesahau kuutaja huo udhaifu wao kama chama na pengine kutueleza namna ulivyo na uhusiano wa namna moja au nyingine  na haya matukio ya watu wazito anaowataja  kwa majina ambao wamekuwa wakiondoka Chadema ukianzia na Amani Kabourou hadi Julius Kalanga wa usiku wa kuamkia jana.

Hivi Lissu anataka tuamini kwamba vigogo wote hao wamekuwa wakiondoka kwa sababu tu ya ‘kununuliwa’ na kununulika na si kwa sababu nyingine tofauti zikiwamo za huo udhaifu ambao hautaji?

Lissu amesema jambo jingine muhimu na linalofikirisha kwamba, pamoja na kuondoka kwa wote hao aliowataja Chadema kimeendelea kubakia chama imara na kinachokua kila wakati.

Kwa upande mmoja na kwa sehemu kubwa ni sahihi kuyatanabahisha haya mafanikio ya Chadema na uongozi wa Mbowe na wenzake wengine ndani ya chama hicho.

Kwa upande wa pili, ni sahihi pia kuyahusisha matatizo haya ya “ki Yuda Iskariote’ ya hao wanaoondoka na udhaifu na pengine makosa ya kiuongozi ndani ya Chadema.

Haitoshi na naamini haitakuwa sahihi kwa wana Chadema kupuuza kila hoja za waondokaji hao kwa namna ile ile ambayo hatuwezi kupuuza ukweli mwingine kwamba katika haya yote CCM ama ina mikono yake au ni washangiliaji wakuu kwa maana ya kunufaika sana kisiasa na haya yanayoendelea kwa mahasimu wao kwa minajili ile ya adui yako mwombee njaa.

Katika mazingira ya Chadema kuwapoteza wanasiasa wa aina ya Kabourou, Chacha Wangwe, David Kafulila, Zitto Kabwe, Profesa Kitila Mkumbo, Said Arfi, Dk. Willibrod Slaa, Mwita Waitara, Kalanga na wengine, ni rahisi kwa mtu au watu kufikia hitimisho la kukiona chama hicho kuwa chenye matatizo makubwa ya ndani.

Pengine Lissu alipaswa kuongeza katika andiko lake kwamba, pamoja na misukosuko yote ya kupoteza makada na viongozi wake wengi, Chadema bado imeendelea kubaki kama alivyoeleza kwa sababu bado imeendelea kuaminika hata kuwavutia wanasiasa wengine wenye majina kujiunga nacho na kukipa uhai mpya.

Kama hiyo haitoshi Lissu anapaswa pia kutambua kwamba kiu kubwa ya mabadiliko waliyonayo Chadema nayo imekuwa sababu nyingine ya kuendelea kuwapo kwa chama hicho pamoja na upungufu wake wote.

Ni kwa sababu hiyo Chadema imekuwa ‘ikilindwa’ na wapenda demokrasia walio ndani ya vyombo vya dola, CCM, katika taasisi za kielimu, kijamii, kiimani hadi ndani vyumba kadha wa kadha vya habari.

Ni kwa sababu hizo ndiyo maana baadhi ya Watanzania na wasio Watanzania, wana Chadema na wasio wana Chadema, wana CCM na wasio na jumuiya ya wapenzi wa demokrasia wamekuwa wakitumia akili zao muda wao na wengine fedha kukisaidia Chadema kuendelea kuwapo.

Miye naamini kwamba, iwapo Chadema ingekuwa inachukua hatua mahususi za kumaliza matatizo yake mengi ya ndani na kuimarisha taasisi yao katika misingi ya kuweka mbele maslahi mapana ya kidemokrasia idadi ya watoro ingepungua na pengine leo kingeshafikia hatua ya kuwa chama tawala mbadala, safari na ndoto ambayo wapenda demokrasia wengi tungependa kuiona ikitimia.

Lissu kazitaja chopper ambazo tangu mwaka 2005 zimesaidia safari za anga za viongozi wakuu na wa juu wa Chadema ambazo anajua kwamba mara kadhaa fedha za kuzirusha hata kama zilipita kwa viongozi, waliozitoa hawakuwa hata wanachama wa chama hicho.

Itoshe tu kueleza kwamba, japo Lissu kasema ukweli. Alichoandika ni sehemu mojawapo tu ya ukweli mwingi mwingine ambao hakuugusa kwa namna ile ambayo hata miye nimeandika ukweli kwa sehemu tu ninayoijua…

Chadema itakuwa inajipa matumaini yasiyo halisi iwapo itaendelea kujiaminisha kwamba itaweza kuhimili vishindo hata kufikia azma kukamata dola mbele ya safari, wakati kila leo ikipoteza  watu mahiri na wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na kitaifa kwa wingi unaoendelea.

Kwa mwelekeo huu wa mambo, nakubaliana na Lissu kwa asilimia 100 kwamba hata baada ya misukosuko hii,  Chadema itaendelea kubaki, japo uwepo wake utazidi kukichimbia mizizi chama hicho kibakie pengine chama

kikuu cha upinzani kwa miaka mingi ijayo kabla hakijazinduka na kufikiria kukiondoa madarakani  CCM kwa njia ya kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles