*Yaiomba Serikali kuangalia kodi ya mishahara
Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
SHIRIKISHO la Vyama vya Tanzania (TUCTA) limewahimiza wafanyakazi nchini kuhakikisha kuwa wanachapa kazi kwa bidii na ufanisi hatua ambayo itasaidia kuishawishi Serikali kufanya maboresho mbalimbali pindi yanapohitajika.
Wito huo umetolewa leo Mei 5, 2023 Dar es Salaam na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Said Wamba, ambapo amesema kuwa pamoja na maboresho makubwa mabayo yamefanya na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan lakini ameiomba kuangalia upya viwango vya kodi kwenye mishahara.
Wamba ameyasema hayo ikiwa ni siku nne tu zimepita taungu Serikali ya Rais Dk. Samia ilipoahidi kufanya kazi changamoto zinazowakabiri wafanyakazi kauli ambayo aliitoa siku ya Mei Mosi mkoani Morogoro.
“Ni vyema wafanyakazi katika sekta ya umma kuendelea kufanyakazi kwa ufanisi zaidi na kwa tija ilikuweza kuishawishi serikali kufanya marekebisho hayo ya mishahara na kodi.
“Sisi kwa nafasi yetu tutaendelea kuhakikisha kwamb achangamoto zinazowakabili wafanyakazi zinatatuliwa, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanaongeza bidii na tija katika kazi ikiwamo kuzingatia muda wa kazi ili nasi tuweze kupata nguvu ya kudai nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kazi,” amesema Wamba.
Rais Samia alisema nini?
Katika hotuba yake ya Jumatatu Mei Mosi, 2023 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro Rais Samia ametoa ufafanuzi wa nyongeza hiyo.
“Mishahara kwa mwaka huu mbali na upandishaji wa posho nilizosema tumejiandaa pia kupandisha madaraja, vyeo vitaendelea kupandishwa, kutenganisha makundi na madaraja mserereko wale ambao hawakupata mwaka jana watapata mwaka huu.
“Niseme pia kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa, nikaona kwa mwaka huu tuzirudishe kwa wafanyakazi wote kuna nyongeza za mishahara tunaanda na tutaendelea kama tulivyokuwa tunafanya zamani,” alisema Rais Samia.
Kuhusu PEYE
Katika hatua nyingine, TUCTA imeiomba Serikali kutazama upya viwango vya kodi na mishahara katika sekta ya umma na binafsi ili kuboresha masilahi kwa mfanyakazi.
Wamba amesema ni vyema Serikali ikaboresha viwango vya kodi kwa wafanyakazi wa umma sambamba na mikataba ili kuboresha hali bora kwa mfanyakazi wa umma.
“Tunaiomba Serikali ifanyie kazi marekebisho ya Bima ya Afya ili kumnufaisha mfanyakazi wa sekta umma bila kuumia,” amesema Wamba.
Aidha, amesema kuwa ni vyema Serikali ijenge utamaduni wa kukutana na vyama vya wafanyakazi ili kuweza kujadili changamoto za wafanyakazi na kuzitafutia ufumbuzi.