25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUCTA yamshukuru JPM, yatoa maombi sita

SARAH MOSES-DODOMA

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limetoa shukrani kwa Rais Dk. John Magufuli huku likiambatanisha maombi  sita.

Katika maombi hayo, TUCTA imemwomba Rais Dk. Magufuli aangalie upya kikokotoo cha mafao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika kipindi hiki cha mpito ili kilingane na iliyokuwa mifuko ya LAPF na PSPF.

Pia limesema kwa kuwa mshahara wa wafanyakazi bado ni mdogo, hata kikokotoo kikiwa kizuri mafao yatakuwa chini na kumwomba Rais mwaka huu aangalie upya suala la nyongeza ya mishara ya wafanyakazi  mwaka huu.

Maombi hayo yalitolewa mjini Dodoma jana na Katibu Mkuu wa TUCTA, Yahaya Msigwa baada ya maandamano ya amani yaliyofanywa na umoja wa chama hicho kwa ajili ya kumpongeza kwa kuweza kulipatia ufumbuzi suala la kikokotoo cha pensheni katika Mfuko wa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Alisema wanaomba uwakilishi wa wafanyakazi kwenye bodi mbalimbali zilizopo na kwenye bodi za utatu wafanyakazi wawe wengi kwenye uwakilishi.

“Tunakuomba ofisi yako kwa kushirikisha wadau katika kipindi hiki cha mpito kusimamia zoezi la kutengeneza kikokotoo kizuri cha pensheni,”alisema.

Pia alisema wafanyakazi wanaotumikia taifa hili katika sekta mbalimbali wamejitolea kuwatumikia wenzao katika nafasi wanazozitumikia.

Hivyo wanapomaliza muda wao wa utumishi kazini,wanaporudi makwao warudi kama mashujaa na waajiri wao wawapatie tuzo ya kutambua na kuthamini utumishi wao.

Naye Makamu wa Rais wa TUCTA, Qambos Sulle alisema wafanyakazi  wamefarijika sana na wameguswa kwa jambo alilolifanya.

“Wafanyakazi wengi waliona kama adhabu yani,kwa usikivu wa Rais wetu ameweza kufanikisha kuiondoa adhabu hiyo,tunamshukuri,”alisema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali iko tayari wakati wote kuyapatia ufumbuzi  matatizo ya wafanyakazi ikiwa ni moja ya njia yakuboresha mishahara na maslahi yao wakati wote wakiwa kwenye utumishi.

“Wito wa Serikali kwa wafanyakazi waendelee kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu,weledi na kujituma, ikiwa ndio chachu ya kufikia malengo ya ustawi wa maendeleo ya nchi yetu,”alisema Majaliwa.

 Alisema hatua ya uunganishwaji wa mifuko ililenga kuimarisha,kukidhi kilio chao cha muda mrefu kuhusu kuunganisha mifuko ya pensheni ,ili kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko tuliyonayo.

Aliwaomba wafanyakazi hao kukubali kushirikiana na mamlaka husika katika kupata muafaka wa jambo hilo kwa siku za usoni kwa kujadiliana kwa njia njema ili kupata kikokotoo sahihi kitakacho tumika baada ya majadiliano hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles