LEONARD MANG’OHA Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema kuwa hatua ya Rais Dk. John Magufuli kusema hatapandisha mishahara mipya kwa wafanyakazi, limezua taharuki na kushusha hamasa ya kazi.
Kauli hiyo ya Tucta imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kusema kuwa tangu alipoingia madarakani hakupandisha mishahara ya watumishi wa umma na kamwe hatapandisha, bali anawatumikia kwanza Watanzania.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, alisema kauli hiyo ya Rais Magufuli, si miongoni mwa mambo waliyokubaliana naye yatekelezwe katika mwaka huu wa fedha 2017/18.
“Inaumiza sana wafanyakazi na leo hii kila mtu anayetaka kufanya lake kundi linaloonekana la kukanyagwa ni la wafanyakazi na mengine ni ahadi yake mwenyewe wakati akiomba kura kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015. Kwa kweli sisi kama Tucta tumeumia na kusononeshwa.
“Mambo tuliyokubaliana yatekelezwe ni kutolewa kwa ‘annual increment” (ongezeko la mshahara la kila mwaka),” kupandishwa madaraja na kulipwa kwa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi.
“Hilo suala la nyongeza halikuwa miongoni mwake, lenyewe tulikubaliana lianze mwakani, labda kitu kinacholeta shida na watu ni ‘tone’ aliyoitumia Rais ndiyo imeshindwa kueleweka kwa wengi, sisi tulikuwa tunalifahamu hilo,” alisema Nyamhokya.
Kuhusu makubaliano waliyofikia alisema kuwa mengi hayajatekelezwa, lakini anaamini yatatekelezwa kama walivyokubaliana, huku madai ya wafanyakazi akisema kuwa baadhi ya tayari wameanza kulipwa malimbikizo yao.
ACT
Naye Katibu, Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema kauli hizo zisipokemewa watu wanaaminishwa na kuzikumbatia kama sheria.
Alisema licha ya kuwa Tanzania ni nchi ya utawala wa sheria, wapo watu miongoni mwa watawala na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaishi na fikra kuwa uongozi wa nchi hii ni wa kifalme.
“Tunao wajibu wa kuwakumbusha watu hao kufuata Katiba ya nchi, kuacha kauli zisizo za kiuongozi pamoja na kutokujiona kuwa ni wafalme wanaoweza kufanya chochote watakacho.
“Swali la kujiuliza baada ya kauli hiyo ni je, wafanyakazi wa Tanzania wanapaswa kufanyiwa hivi na Serikali wanayoihudumia? Jibu bila shaka ni hapana. Serikali inatoa wapi jeuri ya namna hii dhidi ya wafanyakazi nchini wakati kiuzalishaji na kimapato inawategemea? alihoji Shaibu.
Alisema licha ya mchango wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali pia ndiyo wanaochangia zaidi katika mapato ya Serikali kuliko watu wenye mitaji (waajiri).
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2014/15 hadi sasa, wafanyakazi ndiyo wamekuwa wakichangia robo tatu ya kodi zote za mapato ya Serikali huku waajiri wao wakichangia robo pekee.
“Kutokana na mchango wao, imetazamiwa kwamba mkuu wa nchi angetanguliza mbele masilahi yao hasa ulipwaji wa mishahara bora badala ya kuwapuuza,” alisema Shaibu.
Shaibu aliongeza kuwa kauli hiyo ya Rais inakinzana na ile aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ya kuhakikisha Serikali inaimarisha masilahi ya wafanyakazi ikiwamo mishahara bora.
Alilitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kuhakikisha linatimiza wajibu wake kwa kusimama imara kupigania haki za wafanyakazi ambao ni wanachama wa shirikisho hilo.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wafanyakazi kukumbuka kile alichokiita dharau za Serikali kwao na kuzitumia kama tiketi ya kuiondoa Serikali madarakani katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.
MEYA WA UBUNGO
Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, alisema halmashauri zikae mkao wa kutegemea madudu zaidi kufanyika.
Alisema wakati wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, walikuwa na unafuu na kila mwaka wakipandishiwa posho na ndiko kulikokuwa kunawafanya waendelee kulinda fedha za halmashauri, rasilimali na kutumika vizuri.
Alisema iko haja ya madiwani wote nchini kukutana na kulijadili kwa kina suala hili ili kujua wanaliendea vipi katika utekelezaji na si kujiuzulu.
“Rais asifikirie kwamba watu watajiuzulu kama alivyosema, bali watakachofanya ni kuongeza wizi wa mapato katika halmashauri, usimamizi utakuwa mbaya ..na hilo alilosema Rais kuhusu madiwani halipo katika nchi yoyote duniani ndio kwa mara ya kwanza kumsikia yeye,’’ alisema Jacob.