23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TSHISHIMBI ATUA PEMBA KUIWAHI SIMBA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MASHABIKI wa Yanga sasa roho kwatu, baada ya kiungo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi, kutua nchini na kuungana na wachezaji wengine wa timu hiyo walioko kambini kisiwani Pemba.

Yanga imejichimbia kisiwani humo ikijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, utakaopigwa Agosti 23, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho cha Jangwani kilielekea Pemba jana asubuhi kikitokea Unguja, ambako juzi usiku kilicheza  mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandege FC na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Tshishimbi, aliyetua Yanga wakati wa dirisha la usajili wa msimu ujao akitokea Mbabane Swallows, alikuwa akisubiriwa kwa hamu kwa mashabiki wa timu hiyo ambao wanamtarajia atamaliza tatizo katika eneo la kiungo mkabaji.

Kiungo huyo anasifika kwa aina yake ya soka la pasi ndefu zenye macho, lakini pia akiwa na uwezo mkubwa wa kusaidia eneo la ulinzi.

Mashabiki wa Yanga wanaamini timu yao ni dhaifu katika eneo hilo kiasi kwamba wapinzani wao, Simba wamekuwa wakiutumia mara kadhaa kupata matokeo mazuri timu hizo zinapokutana.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Dismas Ten, alisema kikosi chao kiliondoka kisiwani Unguja majira ya asubuhi   na kuwasili Pemba mchana, ambapo jioni kilitarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mao.

“Tshishimbi tayari amewasili nchini na mchana huu ataondoka Dar es Salaam na ndege kwenda Pemba, kabla ya kesho asubuhi kuanza mazoezi na wenzake.

“Ratiba yetu inaonyesha tutakuwa tunafanya mazoezi kwa siku mara mbili hadi pale tutakaporejea Dar es Salaam tayari kwa mechi dhidi ya Simba,” alisema.

Hata hivyo, kabla ya gazeti hili halijakwenda mtamboni, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alithibitisha Tshishimbi kuungana naye katika kambi kisiwani Pemba.

“Ni jambo zuri kuona amejiunga na wenzake, ukizingatia yeye ni mchezaji mzoefu na mwenye uwezo mkubwa.

“Ujio wake utanipa fursa kubwa ya kuangalia wachezaji gani wako fiti zaidi kwaajili ya mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema.

Kabla ya kujiunga rasmi na timu hiyo kisiwani Pemba, kiungo huyo alishindwa kuungana mapema na wachezaji wengine wa kikosi hicho, kutokana na kuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ambao hata hivyo sakata hilo lilimalizika baada ya makubaliano ya pande hizo mbili.

Tayari Yanga imeshacheza mechi tatu za kirafiki, ambapo kati ya hizo, ilifanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo miwili, dhidi ya Singida United iliposhinda mabao 3-2 na Mlandege ilipoilaza mabao 2-0, huku ikichapwa bao 1-0 na Ruvu Shooting.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara hawajafanya maboresho makubwa katika kikosi chao, badala yake wamesajili wachezaji wachache wapya.

Wachezaji wapya waliotua Yanga kwaajili ya msimu ujao ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Baruani Akilimali, Pius Buswita, Ibrahim Ajib, Ramadhani Kabwili, Youthe Rostand na Tshishimbi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles