27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Tshisekedi azikwa kitaifa DR Congo

KINSHASA, DRC

ALIYEKUWA kiongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Etienne Tshisekedi amezikwa rasmi kitaifa nchini hapa jana, ikiwa ni miaka miwili baada ya kifo chake kilichotokea nchini Ubelgiji.

Mwili wake ulisafirishwa kutoka Ubelgiji na kurejeshwa DRC Alhamisi iliyopita, baada ya kumalizika kwa mgogoro kati ya familia yake na Serikali iliyopita, ambayo haipo tena madarakani.

Mgogoro huo ulimalizika baada ya mwanawe, Felix Tshisekedi kutangazwa kuwa Rais wa DRC Januari mwaka huu, baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita.

Makumi ya maelfu ya watu walihudhuria ibada ya wafu katika Uwanja wa Mashahidi mjini Kinshasa wakiongozwa na Askofu Fridolin Ambongo.

Katika ibada hiyo, Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini hapa liliwataka wafuasi wake kuhudhuria kwa wingi katika mazishi hayo.

Siku ya Ijumaa, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Angola, Joao Lourenco walikuwa miongoni mwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza kutoa heshima za mwisho kwa marehemu, baada ya miaka kadhaa ya uhasama kati ya mataifa yao na DRC.

Tshisekedi alitarajiwa kuzikwa katika makazi yake ya Nsele, umbali wa karibu kilomita 40 mashariki mwa Kinshasa.

Alifariki akiwa na umri wa miaka 84 mjini Brussels na mwili wake uliwekwa katika nyumba ya kuhifadhi maiti hadi uliposafairishwa nyumbani Alhamisi wiki iliyopita.

MAISHA YA UPINZANI

Wakati wa uhai wake, Tshisekedi alihudumu kisiasa kwa miongo kadhaa, lakini akashindwa katika jaribio la kuwa rais wa nchi hiyo.

Alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Mobutu Seseko, kabla ya kujiunga na siasa za upinzani.

Baada ya kutumikia kifungo jela, alianzisha Chama cha UDPS mwaka 1982 na aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Serikali ya Mobutu licha ya kwamba wawili hao walizozana mara ka mara.

Mwaka 1997, Mobutu aliondolewa madarakani katika upinzani ulioongozwa na baba wa Joseph Kabila, Laurent Kabila.

Tshisekedi alikuwa mpinzani wa utawala mpya wa Joseph Kabila baada ya Laurent Kabila kuuawa mwaka 2001.

Alisusia uchaguzi wa DR Congo wa 2006, akidai kwamba ulikuwa umefanyiwa udanganyifu na baadaye alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2011 uliodaiwa kukumbwa na udanganyifu.

Felix Tshisekedi alishinda uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali mwaka uliopita, ikiwa ni mwaka mmoja na nusu baada ya kifo cha baba yake.

Uchaguzi huo, hata hivyo uliadhimisha ubadilishanaji wa uongozi tangu DRC ilipojipatia uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Hata hivyo baadhi ya wachunguzi wa uchaguzi huo waliamini kwamba mgombea mwingine wa upinzani, Matrin Fayulu ndiye aliyefaa kuibuka mshindi.

Tangu alipochukua madaraka, Rais Tshisekedi alikubali kushirikiana na aliyekuwa rais wa zamani, Joseph Kabila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles