23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

TSC Yaeleza sababu zinazoweza kuhitimisha kazi ya Mwalimu

Na Veronica Simba – TSC

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), imebainisha mambo kadhaa yanayoweza kumsababishia Mwalimu, hususan aliyeko katika Utumishi wa Umma, kuhitimishiwa kazi yake ya ualimu.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Mectildis Kapinga wakati akiwasilisha Mada kuhusu majukumu ya Tume katika masuala ya ajira na maendeleo ya walimu, wakati wa mafunzo ya Wajumbe wa Kamati za Wilaya zinazoshughulikia ajira na maadili ya walimu, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mectildis Kapinga, akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Tume  katika masuala ya ajira na maendeleo ya walimu wakati wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za TSC, zinazoshughulikia masuala ya ajira na maadili kwa walimu, zilizoko Kanda ya Ziwa, mwishoni mwa juma jijini Mwanza.

Kapinga alieleza kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 9(1) (a) – (g) ya Kanuni za Utumishi wa Walimu za mwaka 2016, mambo yanayoweza kumsababishia Mwalimu ahitimishe kazi yake ya Ualimu ni pamoja na kustaafu kwa kutimiza umri kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa, sababu nyingine ni kustaafu kwa ugonjwa, kuachishwa kazi kwa masuala ya kinidhamu, kufariki, kuacha kazi kwa hiari, kustaafishwa kwa manufaa ya umma, kufutwa kwa Ofisi na kugombea nafasi za uongozi hususan wa siasa.

Akielezea kuhusu utaratibu unaotumika wakati Mwalimu anapohitimisha utumishi kwa kustaafu kwa lazima au hiari, Mkurugenzi Kapinga alisema ni pamoja na Ofisi za TSC, Ngazi ya Wilaya kuandaa maoteo ya kustaafu kazi walimu kwa kila mwaka wa fedha na kuwasilisha nakala Makao Makuu ya Tume pamoja na kwa Mwajiri.

Vilevile, alieleza kuwa utaratibu mwingine unaotakiwa kufanyika ni kwa Mwalimu anayetarajia kustaafu kwa hiari au lazima, kutoa taarifa miezi sita kabla ya tarehe ya kustaafu kwake, ikiwa ni kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma.

Aliongeza kuwa, Katibu wa Tume ngazi ya Wilaya, anatakiwa kuandika kibali cha kustaafu kazi na kibali hicho kipitishwe na Mwajiri kabla ya kukabidhiwa kwa Mwalimu husika.

Katika hatua nyingine, Kapinga alieleza kuwa kustaafu kwa lazima au kwa hiari kunategemea tarehe ya kuzaliwa kwa mwalimu, ambapo anaruhusiwa kustaafu kwa hiari afikishapo umri wa miaka 55 na atalazimika kustaafu kwa lazima afikishapo miaka 60.

Aliongeza kuwa, endapo itatokea kwenye kumbukumbu za kuzaliwa, Mwalimu akawa alijaza mwaka bila tarehe, basi tarehe yake itakayotumika itakuwa Julai Mosi ya mwaka atakaostaafu.

“Aidha, ikitokea kuwa alijaza mwezi na mwaka bila tarehe, basi tarehe yake ya kuzaliwa itahesabika kuwa tarehe 15 au 16 ya mwezi huo,” alifafanua Kapinga.

Alihitimisha kwa kueleza kuwa, endapo kutakuwa na mgongano wa tarehe ya kuzaliwa kwenye kumbukumbu za kiutumishi za mwalimu husika, tarehe itakayotambuliwa kuwa ni tarehe yake sahihi ya kuzaliwa ni ile inayompa umri mkubwa.

Mafunzo hayo yalihusisha wilaya zote za mikoa ya Kanda ya Ziwa na yalilenga kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati husika waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,244FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles